INGAWA kila upande umeonyesha
kuwa suala kukutana kwao ni kama sehemu ya mazungumzo, lakini tayari kuna
fununu huenda Yanga ikamvuta kocha wa zamani wa Simba, Milovan Cirkovic.
Uongozi wa Yanga unaamini Milovan
anayehaha kuidai Simba fedha zake ni mmoja wa makocha bora kabisa hasa katika
ngazi ya kukuza wachezaji vijana wanaochipukia katika soka.
Wakati akiwa Simba, alionyesha
kwamba analiweza hilo baada ya kutoa nafasi kwa vijana wengi waliokuwa hawapewi
nafasi kama vile Shomari Kapombe, Jonas Mkude, Haruna Chanongo, Abdallah Seseme
na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Milovan alitoa nafasi kwa vijana
zaidi ya hao na kuwapa majukumu makubwa na mwisho wakaaminika hadi katika
kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, kitu ambacho kilimjengea zaidi jina lake.
Taarifa zinaeleza suala hilo liko
katika mjadala, Ernie Brandts ataendelea kuwa kocha wa timu kubwa na Milovan
akuze vijana ambao atamkabidhi Mholanzi huyo.
Hata hivyo, suala hilo linafanywa
kwa umakini mkubwa na viongozi wa Yanga wamekuwa wagumu kulizungumzia hadharani
huku ikionekana kuwa kuna jambo linafuatia.
Hata hivyo picha zilizonaswa
wakiwa Milovan na viongozi wa sasa na wale wa zamani wa Yanga ni dalili ya
kuonyesha kuna jambo.
Milovan mwenye amesisitiza ni
mazungumzo ya kawaida tu, kama alivyozungumza na gazeti la michezo la CHAMPIONI
ambalo leo limetoka na picha zake akiwa na viongozi hao wa Yanga.
Salehjembe inaendelea kufanya
uchunguzi wa jambo hilo ikiwa ni pamoja na kufuatilia lini Milovan atalipwa na
Simba kwa kuwa viongozi wake wameshasambaratika.
0 COMMENTS:
Post a Comment