Kocha Mkuu wa Azam, Stewart John Hall amefungiwa mechi tatu na
kupigwa faini ya Sh 500,000 kwa kushusha bukta yake na kumlalamikia mwamuzi
msaidizi wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake na
Kagera Sugar iliyochezwa Januari 26 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko
Chamazi, Dar es Salaam.
Adhabu hiyo imetolewa na TFF, iliyokutana mwishoni mwa wiki
kupitia ripoti za michuano ya VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa
2012/2013 inayoendelea hivi sasa na kufanya uamuzi mbalimbali.
Naye Kocha Msaidizi wa timu ya Mgambo Shooting, Denis
Mwingira ametozwa faini ya Sh 500,000 kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye
mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Oktoba mwaka jana katika Uwanja wa
Manungu.
Ally Jangalu ambaye ni Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro
naye ameangukiwa na rungu la Kamati ya Ligi kwa kupigwa faini ya sh. 500,000
baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kupinga uamuzi wa refa kwa sauti ya juu.
Alitenda kosa hilo kwenye mechi kati yao na Kagera Sugar iliyochezwa Novemba 10
mwaka jana Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Matukio ya aina hiyo kwa kocha Jangalu yamekuwa ya
kujirudiarudia ambapo Oktoba 13 mwaka jana katika mechi dhidi ya Azam
iliyochezwa mjini Morogoro aliondolewa na mwamuzi kwenye benchi kwa kuchochea
wachezaji wa timu yake wacheze rafu.
Naye Kocha wa timu ya Moro United inayoshiriki FDL, Yusuf
Macho amepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumtolea lugha chafu refa baada ya
mechi dhidi ya Transit Camp iliyofanyika Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa
Mabatini mjini Mlandizi.
Pia Kocha wa Burkina Faso, Hasheem Mkingie amepigwa faini ya
sh. 200,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kutoa lugha chafu katika mechi
ya FDL dhidi ya Mkamba Rangers.
Kiongozi wa Majimaji, Joseph Nswila ambaye aliingia uwanjani
baada ya mechi dhidi ya Mlale JKT kumalizika na kuvamia waamuzi amefungiwa
miezi sita.
Vilevile timu ya Azam imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa
kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi kati yao na JKT Oljoro iliyochezwa
Novemba 7 mwaka jana katika Uwanja wao wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es
Salaam.
Pia Coastal Union imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana na
washabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa
mechi yao dhidi ya Simba iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga.
Nayo klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa
timu yake kugoma kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo wakati wa
mapumziko katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga, Oktoba 24 mwaka jana.
Timu ya Burkina
Faso ya Morogoro imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na kuonesha vitendo vya
ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Oktoba 24 mwaka
jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Faini ya ushirikina ya sh. 200,000 pia imepigwa timu ya
Pamba baada ya kuonesha vitendo hivyo kwenye mechi yao dhidi ya Mwadui
iliyochezwa Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Pia Mkamba
Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya washabiki wake kumtolea lugha
chafu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA), Hamis Semka
na kumrushia chupa za maji mwamuzi wa mezani katika mechi dhidi ya Mbeya City
iliyochezwa mjini Morogoro.
Polisi Dodoma imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na
washabiki wake kuvamia uwanjani na kutaka kuwapiga waamuzi katika mechi yao
dhidi ya JKT Kanembwa na kusababisha mipira miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kupotea.
Pia klabu kadhaa zimeandikiwa barua za onyo kwa timu zao
kuchelewa kufika uwanjani au kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi
(Pre-match meeting). Klabu hizo ni Coastal Union, JKT Ruvu, Toto Africans,
Simba, Green Warriors, Majimaji, Mkamba Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa,
Moro United.
Mchezaji Stanley Nkomola wa JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya
Coastal Union alikwenda jukwaani na kuanza kupigana na washabiki. Pia kipa wa
timu ya Transit Camp, Baltazar Makene baada ya mechi dhidi ya Tessema aliruka
uzio na kwenda kupigana na washabiki.
Kwa vile masuala ya wachezaji hao ni ya kinidhamu
yamepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP)
mstaafu Alfred Tibaigana kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
0 COMMENTS:
Post a Comment