FEDHA ZA OKWI SI KAWAIDA, KUNA KITU KINAFICHWA
KUNA shabiki mmoja wa Simba wakati anatoa maoni yake,
aliwahi kuniuliza hivi: “Mara kadhaa unauliza kuhusiana na fedha za Okwi, kwani
ni zako, hazikuhusu, tuachie Simba yetu.”
Wakati naanza kuisoma nilikuwa napigana na uchovu wa
siku nzima, lakini baada ya hapo ilinichangamsha sana kwa kuwa nilianza
kufikiria upya namna watu wanavyofikiria. Yule shabiki anaamini Simba ni yake,
lakini hana uwezo hata kidogo wa kufikiria kuhusiana na klabu yake.
Kizuri kwa shabiki kama huyo na wenzake ambao wana
fikra kama zake ni kuona Simba inashinda, basi. Kuhusiana na maendeleo ya
klabu, kwenda kisasa na kufanya mambo kiteknolojia, hawajali. Inawezekana
kabisa, watu kama shabiki huyo wanahitaji kubadilika, mimi Simba si yangu, ila
nahoji kwa ajili ya faida ya Simba na jamii ya wadau wa soka na michezo kwa
ujumla.
Metodo nyingine, pia bado inaendelea kuhoji kuhusiana
na fedha hizo za Okwi ambazo
zilitangazwa kwamba ni dola 300,000 (zaidi ya Sh milioni 480) ambazo klabu ya
Etoile du Sahel imekubali kuzitoa kumnunua kiungo huyo raia wa Uganda.
Okwi alikuwa ni tegemeo la Simba katika kuanzisha
mashambulizi, ameuzwa kwa fedha nyingi ambazo unaweza kusema Simba walikuwa na
kila sababu ya kushawishika na kumuachia aende na kuchukua fedha hizo.
Lakini hofu kubwa ambayo nimekuwa nayo ni mchezo wa
kizamani sana ambao unachezwa, inawezekana wengine mkawa mmesahau au si wenyeji
wa kitambo wa soka Bongo, nitawakumbusha kidogo.
Timu zilikuwa zikiuza wachezaji, mara nyingi wanachama
walikuwa wanatangaziwa fedha zao zitalipwa kwa mafungu. Mtindo huo haukuanza
leo, ingawa mifano ya hivi karibuni inajulikana, mfano Haruna Moshi alipouzwa
Sweden na Henry Joseph alipouzwa Norway.
Lakini hakuna shabiki au mwanachama anayejua kama
fedha hizo zilikuja zote au la, hakuna taarifa ambayo ilitolewa baada ya hapo,
kwa kifupi viongozi wanajua mashabiki na wanachama ni wasahaulifu ndiyo maana
wanatumia mbinu hiyo.
Kusema fedha za Okwi zitakuja kwa mafungu huku
viongozi wa Simba wakionekana kujikanyaga katika hilo, kidogo kunanishtua na
ninapata hisia ule mtindo wa kitambo utaendelea na mwisho hapa itatokea ishu
nyingine na fedha hizo zitakuwa zimepita.
Katika ya vitu vinavyoshangaza zaidi katika biashara
hiyo ya Okwi, eti Simba wamemuuza, Watunisia hao wako tayari kutoa dola 300,000
na Okwi wamempa dola 100,000 (Sh milioni 160), lakini katika malipo ya klabu
hawajaanza kulipa hata senti.
Ninavyojua kama ni malipo ya mafungu (installment),
basi baada ya kukubaliana, Etoile du Sahel walitakiwa kulipa fungu la kwanza.
Mfano ingekuwa dola 100,000 na baada ya hapo wangeendelea kulipa hatua kwa
hatua, labda dola 100,000 au 50,000 hadi watakapomaliza.
Lakini kusema Simba hawakupokea kitu kabisa baada ya
biashara hiyo ni kuudanganya umma. Hakika haiwezi kuwa lahisi, hauwezi kuiita
biashara ya kwenda kuuza bidhaa unaondoka bila kupata malipo ya awali.
Kama itakuwa Simba walifanya hivyo itakuwa ni makosa
makubwa, lakini bado ninahisi kutakuwa na namna, huo ni wasiwasi wangu nilionao
kuhusiana na hilo na kama kutakuwa na kiongozi wa Simba ambaye anapinga hilo,
vizuri akajitokeza wakalizunghumzia hilo.
Fedha za Simba ni za umma, hata kama hautakuwa umma
wote basi ni Wanasimba na wana haki ya kujua. Waelezwe ili kuondoa hali hii ya
wasiwasi kwa kuwa fedha walizopata ni nyingi sana na zinaweza kuisukuma Simba
mbele kimaendeleo badala ya kuendelea kuwa ombaomba kama ilivyo sasa.
Simba ina madeni lukuki, wachezaji hawajalipwa hata
fedha zao za usajili, makocha na wachezaji bado wanadai, lakini hata kocha
aliyeondoka walishindwa kumlipa hadi wakapata msaada. Sasa vipi leo kuna fedha
nyingi kama hiyo hakuna ufafanuzi na wanachama wako kimya.
Najua wako wanaochukizwa na kuhoji kwangu, lakini
nitaendelea kufanya hivi kwa kuwa lazima tujue kuhusiana na hilo kwa vile mauzo
ya Okwi yalikuwa hadharani na kila kitu kilionekana, basi ni vizuri sana uwazi
ukaendelea kuchukua nafasi.
0 COMMENTS:
Post a Comment