Ningeweza kusema sina kabisa cha kuzungumza, lakini naamini
nitaendelea kwa manufaa ya michezo ya Tanzania na hasa mchezo wa soka,
nasisitiza, mwisho majibu yatapatikana tu.
Nimeanza na kusisitiza kwa kuwa kila kitu kimeanza kuonekana,
kwanza nawapongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope
ambaye aliamua kubwaga manyanga baada ya kuona kweli mambo hayaendi vizuri
ndani ya Simba.
Geofre Nyange ‘Kaburu’ pia aliachia nafasi yake ya makamu
mwenyekiti wa Simba, kitu ambacho ni cha kumpongeza pia, kwa kuwa hata kama
mwanzo alikuwa mgumu, mwisho ameona ukweli, ndiyo maana nikasisitiza wasiouona,
sitachoka kuwaambia hata kama inawaudhi.
Simba imeyumba, haifanyi vizuri na matatizo yake hata si
mambo yaliyojificha chini ya mwembe, kila kitu kikaonekana kwamba uongozi ni
sehemu kubwa ya kusababisha Simba kufeli kuanzia katika michuano ya ndani hadi
ile ya ligi.
Hii si mara ya kwanza Ismail Aden Rage kuwa kiongozi wa
Simba, anajua alishawahi kuondoka baadaye akarejea. Katika masuala ya uongozi
pia hilo ni jambo linaweza kutokea na yanatokea kila kukicha.
Lakini ni vizuri zaidi kuwa na viongozi wanaojitambua, wenye
mapenzi ya dhati na wanachokiongoza. Mfano, kujiuzulu ni kujitambua lakini
utakuwa umeonyesha unakipenda kile unachokiongoza kwa kuwa kuwepo kwako ni
sehemu ya kufeli kwake, sasa kwa nini kiendelee kufeli na wewe umeng’ang’ania tu
pale.
Kuendelea kung’ang’ania ni dalili tosha ya kuonyesha wewe
hauna mapenzi na unachotaka ni manufaa yako binafsi, sasa huu ni wakati mwafaka
wa kumkumbusha Rage bila ya woga, kwamba yeye ni Simba damu,sawa. Lakini
ameshindwa kazi, afuate uzalendo wa Hans Pope na Kaburu.
Angalia matatizo yaliyotokea jana kwa Simba kuzuiliwa katika
hoteli ya Sapphire kutokana na deni la Sh milioni 27, lakini pia wachezaji wake
Waganda, Abel Dhaira, Mussa Mudde na Meneja, Moses Basena kutimuliwa katika
hoteli ya Spice ya Kariakoo.
Aibu gani hiyo, imefikia Simba inashindwa hata kupasha viungo
uwnjani wakati inacheza na Coastal Union, haikuwa sahihi. Ila mwenye hoteli pia
hakuwa na ujanja zaidi ya kuanzisha shinikizo hilo ili alipwe.
Rage anastahili kuondoka Simba wakati huu, wakati ambao timu
hiyo imeshindwa kila kitu. Mambo yanakwenda mlama na inaonekana hakuna pa
kushika, badala yake maisha ya klabu hiyo kwa sasa ni sawa na mfamaji,
inatapatapa tu.
Simba inaonekana hata uongozi umeshindwa kuongoza mambo
vizuri, imefikia hadi wazee wameamua kuunda kamati mpya ya ushindi ambayo
inaongozwa na Malkia wa Nyuki. Wasipoangalia inaweza ikafeli pia kwa kuwa bado
kuna matatizo mengi juu.
Kuundwa kwa kamati hiyo, inaonyesha mambo si mazuri. Kama
kila kitu kingekuwa kinakwenda sawa, basi wakati huu haukuwa wa kuunda kamati.
Ukiachana na hivyo, awali nilieleza kwamba uongozi ni sehemu
ya matatizo, hali halisi inaonyesha hivyo kwa kuwa angalia Rage alivyokuwa
tatizo kwa kuahidi mambo milioni lakini akashindwa kutekeleza hata moja.
Unajua namna ahadi inavyopandisha morali, lakini
isipotekelezwa hugeuka na kuwa sumu. Rage amepandika sumu za ahadi bila ya
mwenyewe kujua, lakini uongozi wake umekosea mambo mengi sana ya kiutendaji
ukiwa madarakani.
Kila mmoja ameona walivyofeli, mfano kusema kocha hafai,
halafu wakaleta mwingine na mambo yakazidi kuwa mabaya zaidi. Sisemi kocha ni
mbaya, lakini kocha hawezi akafanya mambo mazuri bila ya kuwa katika mazingira
mazuri.
Simba inatawaliwa na madeni lukuki, kila siku inakutana na
fedheha kama ile ya basi lake kuzuiliwa Arusha hadi Malkia wa Nyuki alipoamua
kuokoa jahazi na kulipa Sh milioni 11` kati ya Sh milioni 15 walizokuwa
wanadai.
Achana na hiyo, uongozi unasisitiza wachezaji wako katika
morali nzuri, lakini wengi wanadai fedha zao za usajili. Vipi watacheza mpira
kwa kujituma, kibaya zaidi hata mshahara wao wanadai pia, hii hali utasema ni
kosa la nani?
Achana na hivyo, wachezaji wamekuwa hawaelewani, ndani yake
kuna makundi ambayo yamesababisha mpasuko mkubwa. Lakini uongozi kwa kuwa
haushughuliki na masuala ya klabu kwa karibu zaidi na hasa Rage ambaye ndiye
bosi mkubwa, umeshindwa kulitatua tatizo hilo hadi leo.
Mimi ninaamini Rage ni muungwana sana, itafika siku atakubali
ninachomueleza kwa kuwa nia ni kusaidia kwenye tatizo, ataondoka kwa moyo safi
ili kuisaidia Simba. Akiendelea kung’ang’ania, basi iko siku ataondoka kwa
aibu.
0 COMMENTS:
Post a Comment