March 4, 2013



 Saleh Ally ambaye ni mhariri kiongozi wa gazeti la Championi lililoandaa michuano hiyo akihojiwa...
 
Na Mwandishi Wetu, Geita
MICHUANO ya Amani na Upendo iliyoandaliwa na Gazeti la Championi ilianza juzi kwa Timu ya Katoro kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ludete baada ya dakika 120.

Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kuvutia, timu hizo zilimaliza dakika 90 zikiwa sare ya mabao 1-1 na ndipo zilipoongezewa dakika 30 na Katoro kuchomoza na ushindi huo.
Mratibu wa michuano hiyo, Michael Izengo (Zagallo), alisema jana kuwa mashabiki walikuwa  wengi sana na kiwango cha soka uwanjani kilionekana kuwavutia.


“Katoro walitoka hapa uwanjani kwa maandamano huku wakishangilia kijiji kizima kuonyesha kuwa wenyewe ndiyo wameibuka na ushindi kwenye mchezo wa ufunguzi.
“Ukweli hali ya Kijiji cha Buseresere ni tofauti sana na jinsi ilivyokuwa hapo nyuma, sasa kuna amani ya kutosha,” alisema Zagallo.

Katika mchezo wa jana kati ya Buseresere na Samaki, hadi dakika 120 timu hizo zilikuwa sare ya mabao 2-2, lakini mvua kubwa iliyonyesha iliwafanya waandaaji wa michuano hiyo kuuahirisha hadi leo saa tisa alasiri.


Mashabiki walikuwa ni wengi na hata mvua hiyo ilipoanza kunyesha hawakuonyesha kujali bali waliendelea kushangilia huku wakipiga vingoma vyao.

Mshindi wa mchezo wa leo atakutana na Katoro kwenye mchezo wa fainali utakaopigwa wikiendi ijayo lakini Ludete nayo inasubiri timu itakayokutana nayo kwenye nafasi ya tatu.

“Mchezo wa kesho utaanza mapema zaidi ili muda wa kupiga penalti upatikane kama itakuwa hivyo. Leo bado muda ulikuwepo, lakini mvua kubwa iliyonyesha ndiyo imeharibu na mwamuzi akamaliza mchezo,” alisema Zagallo.
Katika michuano hiyo itakayodumu kwa wiki moja, timu zote zimepewa jezi na mipira huku mshindi wa kwanza akitarajiwa kujinyakulia kombe na shilingi laki tano, wa pili atapata laki tatu, wa tatu laki mbili na wa nne laki moja.

Michuano hiyo ni ya kuenzi amani kijijini hapo baada ya mchungaji Mathayo Kachila kuuawa kwenye vurugu za kidini katika tukio lililotokea Februari 12, mwaka huu, saa 2:27 asubuhi kwenye soko la Buseresere, kufuatia kundi la wananchi kuvamia bucha iliyokuwa na maandishi ya ‘Bwana Yesu Asifiwe, Yesu ni Bwana’, kuwataka waliokuwa wakiuza kuifunga, hali iliyozusha vurugu.
Mbali na mchungaji huyo kuuawa, watu wapatao 15 walijeruhiwa wengine ikiwa ni vibaya wakati wa vurugu hizo.


Michuano hiyo imeandaliwa na gazeti maarufu la michezo na burudani nchini la Championi kwa lengo la kusaidia kurudisha amani na upendo katika eneo la Buseresere kupitia michezo.








0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic