September 17, 2016

Na Saleh Ally, Barcelona
Saleh Jembe na Gazeti la Championi wameendelea kuweka rekodi ya kupaa na kufanya mahojiano na wachezaji mbalimbali wa kimataifa. Jana tulianza kuelezea kuhusiana na beki Eric Abidal ambaye ni mtaratibu na aliyepitia mambo mengi sana katika maisha yake ya soka.


Jana, tuliishia akielezea namna alivyopitia mitihani mingi hasa baada ya kugundulika na ugonjwa wa ini huku akitaka kutosahau matukio kadhaa likiwemo lile la beki mwenzake, Dani Alves kukubali kutoa kipande cha ini lake kumpa ilia pone.


Abidal ni mchangamfu sana, ni mtu anayependa utani na mara kadhaa, alikuwa akiulizia kuhusiana na kuja Tanzania kwa kuwa amepata sifa nyingi kutoka kwa wachezaji katika kikosi cha Maveterani wa Barcelona.


“Nitakuja siku moja, nitajipanga. Pia ningependa kusaidia watoto wa Tanzania kutokana na namna ambavyo itawezekana na bajeti itakavyoruhusu,” anasema Abidal akionyesha uchangamfu.


Baada ya hapo, anayakatiza mahojiano, anainuka na kuuliza. Nikuletee nini, maji au kahawa. Jibu linakuwa kahawa, mara moja anafanya hivyo na baada ya kurejea anasema, hakuwa na maziwa.


“Pole, unaweza kunywa hii ya bila maziwa, nafikiri utainjoi tu,” anasema na jibu linaonekana hakuna shida kabisa.


Abidal analikumbuka tukio la Alves kama la ajabu na kushangaza, kwamba ni mapenzi makubwa kupita kiasi ambayo mwanadamu anaweza kumfanyia mwingine.


“Alisema atoe sehemu ya ini lake kwa ajili ya kunipa, ni jambo zuri. Lakini nilikataa katakata. Nilijua akifanya hivyo asingeweza kuwa imara kama mwanzo, pia unajua yeye kazi yake ni soka, ingemuathiri.


“Lakini nikuhakikishie, Alves si rafiki kwangu, ni ndugu, tena ndugu wa damu. Hadi sasa tuko karibu sana katika maisha yetu,” anasema.


“Tukio jingine ni lile la mashabiki kwenye uwanja wote wa Santiago Bernabeu kusimama na kunipigia makofi. Ilikuwa ni mechi ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa, yeye akiwa amerudi Lyon.
“Kama haitoshi, wachezaji wa timu zote mbili walivaa fulana zilizoandikwa “Animo Abidal” (Pona Haraka Abidal). Lilikuwa ni jambo kubwa na aghalabu kutokea, lilinifanya nilie kwa uchungu,” anasema.

Wakati aliposikia kwamba ana ugonjwa huo, Abidal alijua ndiyo mwisho wake wa kucheza soka. Alikata tamaa na kujua kwamba hakuwa na njia nyingine tena, aliamini kuwa ndiyo mwisho wake wa furaha.


“Soka kwangu haikuwa kazi pekee inayoingiza fedha, ndiyo furaha yangu na kila kitu. Niliona kama nimeisha kabisa,” anasema.


Aprili 10, 2012 alifanyiwa upasuaji, lakini baada ya muda ilionekana haukuwa na mafanikio sana kwa kuwa haukumsaidia kurejea katika hali nzuri kama ambavyo ilitarajiwa.


Hata hivyo, baada ya matibabu zaidi, mwezi mmoja baadaye daktari alitangaza kwamba anaweza kuendelea kucheza soka. Akarejea mazoezini.


“Ilikuwa ni sawa na kuzaliwa upya, niliona kama miujiza, nilikuwa muoga lakini taratibu nilianza kuzoea na kucheza kama kawaida,” anasema.


Baada ya kurejea uwanjani, kwa mara nyingine tena aliichezea Barcelona. Jambo ambalo watu wengi hawakutarajia kumuona akirejea uwanjani hadi kufikia kucheza dakika 90.


Je, yeye alikuwa muoga kucheza katika mechi za ushindani tena? Je, baada ya kuanza kucheza kuna matatizo yoyote alikutana nayo? Usikose sehemu ya tatu na ya mwisho ya mahojiano haya maalum na Eric Abidal.


USIKOSE sehemu hiyo ya mwisho itakuwa Jumatatu, ataelezea alivyomaliza mpira wake. Pia anachokifanya kwa kipindi hiki na taarifa kuhusiana na yeye kutaka kuwa kocha.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV