Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji amesema amefurahishwa na Yanga kutimiza
moja ya malengo yake makubwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, lakini haoni kama
kuna sababu ya kufanya sherehe kubwa.
Akizungumza moja kwa moja na Salehjembe kutoka nje ya Tanzania, Manji
alisema ubingwa ni sehemu ndogo tu ya malengo wanayotaka kufikia.
“Tunaweza kusherekea lakini si kufanya sherehe kubwa ambayo itatugharimu
fedha nyingi sana. Tunahitaji fedha kwa ajili ya kujenga uwanja, ni fedha
nyingi mno.
“Hivyo haitakuwa jambo la busara kutumia fedha nyingi kufanya sherehe. Lakini
bado nawapongeza viongozi wenzangu, benchi la ufundi, wachezaji na Wanayanga
wote kwa ujumla.
“Umoja na ushirikiano wetu umetufanya tufike hapa lakini bado tuna
safari ndefu na tunapaswa kuudumisha ili tuendelee kufikia malengo
tuliyojiwekea,” alisema Manji.
Yanga imetawazwa kuwa bingwa jana saa 12:30 jioni baada ya mechi kati ya
Coastal Union na Azam kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Baadhi ya mashabiki wa Yanga walikuwa wakitaka kufanyika kwa sherehe
kubwa baada ya wao kufanikiwa kutwaa ubingwa huo.
Maana yake, kama itawezekana, itafanyika sherehe ndogo tu au haitakuwepo
kabisa kutokana na maelezo ya mwenyekiti wao ambaye anaangalia kusonga mbele
zaidi.







0 COMMENTS:
Post a Comment