Ingawa kasi yao bado haijawa kubwa, lakini baadhi ya wajumbe wa kundi
maarufu la Friends of Simba wameanza kusaidia kazi kadhaa ndani ya klabu hiyo.
Wajumbe hao wameanza kuhaha katika baadhi ya sehemu kuhakikisha kikosi
cha Simba kinabadilika msimu ujao.
Taarifa za uhakika ambazo Salehjembe inazo, wajumbe hao wamekuwa
wakizungumza na wachezaji kadhaa kuhakikisha wanajiunga na Simba ili kujenga
kikosi imara cha msimu ujao.
“Kweli baadhi tumerudi na kuanza kusaidia kazi za usajili na nyinginezo,
klabu iko taabani kifedha na utaona mambo mengi ni magumu.
“Lakini kuna baadhi wanahofia kuingia moja kwa moja kwa kuwa hawamuamini
mwenyekiti, maana anaweza kusema anataka ushirikiano katika wakati mgumu lakini
baadaye akageuka.
“Hivyo wanataka uhakika wa mambo zaidi, ndiyo maana wako pembeni kidogo.
Lakini wakiona kuna ukweli basi timu nzima itarudi,” kilieleza chanzo cha
uhakika kutoka katika kundi hilo.
Friends of Simba ndiyo kundi maarufu zaidi linaloogopewa kwa kusuka timu
pamoja na mipango ya ushindi katika soka Tanzania.
Kuondoka kwa kundi hilo ambalo Mwenyekiti wake ni Zacharia Hans Pope,
kuliifanya Simba iyumbe ingawa angalau kwa msimu mmoja, ilifanya vizuri. Lakini
msimu huu, Simba ikawa dhoof-li hali.
Uongozi wa Simba chini ya Ismail Aden Rage uliokuwa ukitangaza kwamba
kundi hilo linawahujumu, hivi karibuni ulikwenda kupiga magoti na kukiri mambo
ni magumu.
Wako wajumbe wamekubali kurudi na kushirikiana naye, lakini wengine bado
wana hofu kwamba mara nyingi hakuna kauli dhabiti zinazosemwa na uongozi huo wa
Simba.








0 COMMENTS:
Post a Comment