Na Saleh Ally
UNAPOMUULIZA Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts kama
Yanga ina uhakika wa kutwaa ubingwa katika mechi yake ya Jumatano ijayo dhidi
ya Coastal Union, jibu lake ni “lazima”.
Brandts raia wa Uholanzi anaamini kikosi chake ndiyo
imara zaidi kuliko kingine chochote kinachoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu,
hivyo kuwazuia kutwaa ubingwa katika mechi mbili walizobakiza itakuwa miujiza.
“Nina uhakika, tutashinda na kutwaa ubingwa. Hakuna
anayetaka sare hata kama tuna nafasi. Hata baada ya kuwa mabingwa tunataka
kuendelea kushinda mechi zilizobaki ikiwemo ya Simba.
“Najua, Simba na Yanga ni sawa na Madrid na Barcelona.
Kila upande hutaka kushinda, hivyo tutafurahi kuchukua ubingwa na kuwafunga
wapinzani wetu wakubwa,” anasema.
Vita ya kuhakikisha Yanga inafikia ilipo si rahisi,
Championi Ijumaa lilishuhudia makaratasi lukuki katika moja ya meza nyumbani
kwa Brandts ambayo yamejaa mahesabu na michoro ‘ya ajabu’ sawa na ile ya wahasi.
Mazingira ya eneo analoishi Mholanzi huyo yanavutia
kwa mpangilio lakini usafi wake unaonyesha ni ule unaofanywa kwa kufuata
utaratibu.
“Kweli haya makaratasi ni mpangilio wa mazoezi kwa
mwezi mzima, lakini ni namna ninavyoweza kufanya kazi zangu za kila siku.
“Kwanza ninapanga ratiba ya mwezi mzima na nini cha
kufanya, baada ya hapo kila baada ya mazoezi ya siku moja huandika kilichotokea
na tathmini nifanye nini siku inayofuata. Baada ya hapo narudi kwenye ratiba ya
mwezi na kubadilisha mambo kadhaa.
“Haya ni mambo ya kujifunza kila siku, ninasoma kila
siku bila ya kujali uzoefu wangu. Wakati mwingine nafanya hivyo hadi saa nane
usiku, halafu ninaamka saa 11 alfajiri kujiandaa kwa ajili ya kwenda
mazoezini,” anasema Brandts.
Alipoulizwa kwamba, pamoja na kusoma na kubadili mambo
kwa mahesabu na maandishi lakini huangalia mikanda ya video ya timu pinzani?
“Hata siku moja, kazi yangu iko kwenye haya
makaratasi. Naamini nina kikosi bora zaidi katika Ligi Kuu Bara. Hivyo wao
ndiyo wanaopaswa kutuangalia sisi na si sisi kuwaangalia wao, sijafanya hivyo
hata kidogo labda katika michuano mingine.”
Kama anabanwa na mazoezi, usafi na mambo mengine ya
timu, anaweza vipi kudhibiti mambo yote na yote yakaenda kwa mpangilio mzuri?
“Ninaweza ingawa si kazi rahisi, kazi ya ukocha ni
ngumu na unalazimika kuipenda ingawa suala la kujitolea inabidi ulipe nafasi. Lazima
ukubali kufanya kazi zaidi ya kiwango chako wakati mwingine.
“Kuhusu usafi wa hapa nyumbani, kuna mtu anahusika na
kufanya hivyo. Lakini mimi napenda kujifanyia usafi mwenyewe, nafua nguo zangu na
kuosha vyombo. Ingawa (mfanyausafi) amekuwa akisisitiza niache, lakini sioni
shida kufanya hivyo.
“Kwa binadamu unapokuwa una utamaduni wa kujali kitu
chako, mfano mazingira unayoishi. Basi inakuwa ni rahisi kujali kazi yako na
unaofanya nao kazi. Ninaamini kocha au mchezaji kama ilivyo kwa binadamu
wengine anapaswa kuishi sehemu nzuri na mazingira mazuri ambayo yanapaswa yawe chini
ya usimamizi wake.”
“Nilielezwa wanaume kuosha vyombo, hasa katika umri
wangu inaonekana si sahihi kwa utamaduni wa Kiafrika, lakini ninaamini wako
watakaoungana nami kwamba kujituma kwenye vitu vya nyumbani vinakusaidia
kujituma katika kazi pia,” anasema Brandts.
Iwapo Yanga itatwaa ubingwa katika mechi hiyo dhidi ya
Coastal Union ambayo inahitaji sare, maana yake kocha huyo atakuwa ameweka
rekodi ya kuchukua mataji matatu ya ligi katika nchi mbili za Afrika.
Misimu miwili iliyopita alibeba ubingwa wa Rwanda
akiwa kocha mkuu wa APR, hivyo kombe la Yanga litakuwa la tatu.
Pamoja na kutwaa ubingwa wa Rwanda, kwa misimu hiyo
miwili, Brandts alifanikiwa kutwaa makombe manane, yaani michuano yote APR
iliyoshiriki.
Hadi sasa Yanga ina pointi 56 kileleni na zinaweza
kufikiwa na Azam FC pekee iliyo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 47 na
mechi tatu mkononi.
Pointi moja inahitajika kwa Yanga, maana yake kama
itatoka sare na Coastal Union inayoendelea kuwania nafasi ya tatu, basi
itatawazwa kuwa mabingwa wapya wa msimu huu.







0 COMMENTS:
Post a Comment