Na Saleh Ally
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Said Sued ‘Scud’ amesema soka ya Tanzania inaporomoka kutokana na watu wenyewe walio ndani ya soka.
Scud ambaye sasa anaishi kwao mkoani Kigoma, ameiambia Salehjembe kwamba watu wengi wa soka ndiyo wamekuwa chanzo cha kuporomoka kwa mchezaji huo ukilinganisha na zamani.
“Kuna mambo mengi sana yanayoporomosha mchezo wa soka, kwanza watu hawajitumi, wachezaji hawapendi kufundishwa.
Wakati wewe unaanza A kumuelekeza mtu, yeye tayari anakuwa amefika K. hilo ni tatizo, tofauti na wakati wetu tulikuwa tunaelekezwa na kukubali kujifunza.
“Lakini watu wengi wanaoingia katika mchezo wa soka, pia si wanasoka wala hawakuwahi kucheza soka. Sasa hapo pia kunakuwa na tatizo,” alisema.
Scud anakumbukwa kutokana na uwezo mkubwa wa kupachika mabao aliouonyesha wakati akiwa Yanga mwaka 1991 hasa mechi mbili dhidi ya Simba ambazo zote alifunga mabao ya ushindi, moja kila mechi.
Alipewa jina la Scud kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga mashuti makali na kufananishwa na mabomu aina ya Scud yaliyokuwa yakimilikiwa na serikali ya Iraq chini ya Saddam Hussein ambaye sasa ni marehemu.
Kwa sasa anaendesha maisha yake mjini Kigoma ambako alichipukia kisoka kabla ya kujiunga na Yanga mwaka 1990 na kuendelea kufanya mambo makubwa.







0 COMMENTS:
Post a Comment