Na Saleh Ally
SIMBA imefundishwa na makocha wawili katika msimu wa
2012-13, wote kutoka barani Ulaya, mmoja akiwa anatokea Serbia na mwingine
Ufaransa.
Milovan Cirkovic raia wa Serbia ambaye aliipa ubingwa
msimu uliopita, alitimuliwa mwishoni mwa mzunguko wa kwanza kwa madai
alishindwa kufanya vizuri katika mechi zake 13 na kusababisha timu hiyo imalize
mzunguko huo ikiwa katika nafasi ya tatu.
Akaletwa Mfaransa Patrick Liewig, ambaye aliwahi
kufanya kazi ukanda wa Afrika Magharibi, lengo likiwa kuiokoa Simba kutoka
katika mwenendo ambao viongozi wa Simba waliuita ni mbaya.
Tokea Liewig ametua nchini, Simba imeshacheza mechi
tisa za Ligi Kuu Bara na hadi sasa iko katika nafasi ya nne, chini ya vinara
Yanga, wakifuatiwa na Azam FC na Kagera Sugar.
Kwa hesabu, inaonyesha Simba hawajalimaliza tatizo
ambalo walilianzisha mzunguko wa kwanza na mwisho kuamua kuchukua uamuzi wa
kumuondoa Milovan huku wakisema kocha ni tatizo.
Kuna mambo makubwa mawili yanajionyesha, kwamba huenda
Milovan hakuwa tatizo na badala yake ni uongozi, kama si hivyo, basi kocha wa
sasa Patrick Liewig ndiye atakuwa tatizo kwa kuwa ameshindwa kuleta mabadiliko.
Milovan:
Mserbia huyo, katika mechi zake 13, Simba ilishinda 6,
ikatoa sare 5 na kupoteza mbili. Kikosi chake kikafunga mabao 20, kikafungwa 11
na kumaliza katika nafasi ya tatu kikiwa na pointi 23. Tofauti kati yake na
Yanga (ilikuwa sita) na Azam FC (pointi moja).
Liewig:
Katika mechi tisa, tayari kikosi chake kimeshinda 3,
kimetoka sare 4 na kupoteza mbili. Wafungaji wake wamefunga mabao 11,
wamefungwa 9, hivyo katika mechi zote tisa hizo Simba imeingiza pointi 13 tu.
Tofauti ya pointi ya Simba na vinara Yanga na Azam FC
ni kubwa sana ukilinganisha na wakati wa Milovan. Sasa Simba inazidiwa pointi
17 na Yanga, Azam wanaizidi pointi 11.
Mjadala:
Pamoja na mabadiliko ya uongozi kwa Simba,
kinachoonekana hapa hakuna chochote kilicholeta mabadiliko na badala yake
mwenendo wa kikosi cha Liewig kitakwimu ndiyo unaonekana kuyumba zaidi.
Simba imebakiza mechi nne tu kumaliza ligi, ukiacha
Yanga, zote ni dhidi ya timu za wanajeshi kuanzia Ruvu Shooting, Polisi Moro na
Mgambo Shooting, hakuna ubishi zitakuwa ngumu sana kwao.
Ili kufikia angalau rekodi aliyofukuzwa nayo Milovan
kwa madai ni mbovu, Liewig analazimika kushinda mechi zote nne zilizobaki,
kwani ndiyo atakuwa amemzidi Milovan kwa kushinda saba wakati yeye alishinda
sita. Je, itawezekana?
Idadi ya mabao ya kufunga, kwa maana ya kuwa na fowadi
kali. Katika mechi 13, Milovan alifunga mabao 20, Liewig ana 11 katika mechi
tisa. Ikiwa na maana, katika nne alizobakiza anatakiwa kufunga angalau mabao 10
ili kumvuka Mserbia na kuonyesha ilikuwa sahihi kumtimua.
Safu ya ulinzi ya Milovan, ilifungwa mabao 11 katika
mechi 13, lakini ya Liewig ndani ya mechi tisa imeruhusu nyavu kitikiswa mara
tisa. Bado mabao matatu tu kumfikia Mserbia ambayo uongozi wa Simba chini ya
Ismail Aden Rage ulisema ni mbaya.
Swali, katika mechi nne, safu yake ya ulinzi inaweza
kuzuia mabao manne yasiguse nyavu?
Sare za Milovan zilikuwa tano, tayari Simba ina sare
nne. Maana yake kufikia tano inawezekana kabisa. Kitakwimu, bado inaonekana
hakuna tofauti au sababu ya msingi kwa Simba kufanya mabadiliko.
Inawezekana kabisa Milovan hakuwa na matatizo na ugumu
au matatizo yalianzia kwa uongozi kwa kuwa hata Liewig anaelekea kufeli na
huenda akaanguka zaidi ya Milovan kama hakutakuwa na mikakati madhubuti katika
mechi nne zilizobaki.
MSIMAMO WA MILOVAN:
P
W D L
F A GD
Pts
1. Yanga 13 9 2 2 25
10 15 29
2. Azam 13 7
3 3 17
11 6 24
3. Simba 13 6 5 2
20 11 9 23
4. Mtibwa 13 6
4 3 17
12 5
22
5. Coastal 13
6 4 3
16 13 3
22
MSIMAMO WA
LIEWIG:
P W D L
F A GD PTS
1. Yanga 23 16 5 2 41 13 28 53
2. Azam 23 14 5 4 41 19 22 47
3. Kagera 23 11 7 5 24 17 7 40
4. Simba 22 9 9 4 32 21 11 36
5. Mtibwa 24 9 9 6 27 23 4 36
SOURCE: CHAMPIONI NEWSPAPER







0 COMMENTS:
Post a Comment