Na Saleh Ally
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetangaza kumtaka mshambuliaji wa
Coastal Union, Nsa Job kuwasilisha ushahidi mara moja kuhusiana na mtu
aliyemtaja kwamba alimhonga ili asifunge.
Aprili 3, mwaka huu, Nsa alikaririwa na kituo kimoja cha redio akisema
aliwahi kuhongwa na kiongozi mmoja wa klabu kigogo cha soka nchini ili
asiifunge timu yake watakapocheza dhidi yake, akampa fungu la fedha, naye
akapokea halafu bado siku ya mchezo akapachika bao.
Awali ilikuwa ikiaminika kwamba Nsa alipokea fedha hizo wakati akiwa
anaichezea Coastal Union, lakini kwa takwimu kama ni msimu huu, Nsa hajaifunga
timu yoyote ambayo ni kigogo.
Kigogo, maana yake kongwe au kubwa kifedha na umaarufu. Katika Ligi Kuu Bara,
zinazoingia kwenye kundi hilo ni timu nne tu, Yanga, Simba, Azam FC na Mtibwa
Sugar.
Nsa alicheza mzunguko wa kwanza tu, akaumia mechi ya mwisho dhidi ya Ruvu
JKT na ameukosa mzunguko wote wa pili. Katika mechi za mzunguko wa kwanza dhidi
ya Simba, ilikuwa sare ya bila kufungana, walipocheza na Azam, timu yao ikalala
kwa mabao 4-1, bao lao la kufutia machozi likafungwa na kiungo Jerry Santo.
Dhidi ya Yanga, vijana hao wa Tanga walifungwa mabao 2-0, yaliyofungwa na
Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza. Walipowavaa Mtibwa, Coastal walishinda mabao
3-0 yakiwa yamefungwa na Juma Jabu, Gerald Lukindo na Daniel Lyanga.
Kwa takwimu hizo, maana yake msimu huu, Nsa hakuwa ameifunga timu yoyote
kigogo, maana yake tunalazimika kurudi na kuangalia msimu uliopita aliokuwa
akiichezea Villa Squad.
Msimu uliopita, takwimu zinaonyesha Nsa alimaliza akiwa na mabao 12 akiwa
nafasi ya pili ya upachikaji mabao akiwa na Villa Squad ambayo iliteremka
daraja.
Hesabu zinaonyesha
katika mabao yake 12 ya msimu uliopita, timu kigogo aliyoifunga katika
mizunguko yote miwili akiwa na Villa Squad ni Simba katika mechi iliyopigwa Februari
4, 2012, bao lake pekee ndiyo liliiangusha Simba siku hiyo kwa ushindi wa 1-0.
Lakini Machi 17, 2012, Mtibwa Sugar iliichapa Villa kwa mabao 2-1 na hilo
la kufutia ‘machozi’ likapachikwa kimiani na Nsa.
Maana yake Nsa hajaifunga Azam FC wala Yanga msimu huu na uliopita,
lakini uliopita ameifunga Mtibwa na Simba na ndiko anakoelekeza lawama zake
kama ni kati ya misimu hii miwili.
Kama itakuwa hivyo, maana yake timu mbili ndiyo zinaingia katika tuhuma
hizo za Nsa ambazo tayari TFF imemtaka azifafanue kwao kwa kuwaeleza ni
kiongozi yupi aliyefanya hivyo la sivyo adhabu itamkuta mchezaji huyo.
Rushwa limekuwa tatizo kubwa sana katika soka nchini, ingawa ni kitu
kigumu kugundulika kutokana na kufanyika kwa siri sana. Lakini Nsa ameamua
kuweka hadharani, huenda ni wakati mzuri kwa TFF kutoa mfano iwe kwa kiongozi fulani
au mtu mwingine.
Mechi za vigogo (Yanga, Simba, Azam, Mtibwa Sugar) msimu wa 2011-12
alizocheza Nsa akiwa na Villa:
MZUNGUKO WA KWANZA:
Septemba 7, 2011
Simba 1-0 Villa
Gervais Kago 7
Septemba 13, 2011
Villa 0–2 Azam
Tchetche 1
Bocco 35
Septemba 17, 2011
Villa
0-2 Mtibwa
Thomas Morris 13
Said Rashid 47
Septemba 21, 2011
Yanga 3-2 Villa
Niyonzima 19 Kijuso 11
Asamoah 27
Kigi Luseke 72
Kiiza 63
MZUNGUKO WA PILI:
Februari 4, 2012
Villa
1-0 Simba
Nsa Job 40
Februari 15, 2012
Azam 4-1 Villa
Salum Abubakar Nsa Job 22
Abdi Kassim 28
Hamis Mcha 43
Kipre Tchetche 45
Februari 19, 2012
Mtibwa 2-1 Villa
Vincent Barnabas 19 Nsa Job
32
Said Bahanuzi
Machi 17, 2012
Villa 0-1 Yanga
Kiiza
90
0 COMMENTS:
Post a Comment