April 12, 2013




Na Saleh Ally
CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), juzi kilitangaza kumfungia Kocha Mkuu wa Malindi, Mohamed Shuber kwa mwaka mzima.

Shuber amefungiwa baada ya kumkwida mshika kibendera namba moja, Mohamed Seif, wakati timu yake ilipoivaa Chipukizi na kukumbana na kipigo cha mabao 2-1, wiki iliyopita.

Pamoja na adhabu hiyo Malindi imetozwa faini ya Sh 100,000, lakini Shuber alipohojiwa kuhusiana na adhabu hiyo akasema, hakuhusika na kumpiga wala kumsukuma mwamuzi huyo badala yake aliwazuia wachezaji waliokuwa na jazba wakitaka kumvamia.


Kubwa katika ukurasa huu, inaonyesha kiasi gani anavyopingana na ukweli kwa makusudi.

Hiyo si adhabu ya kwanza angalau kuwa kubwa kwa ZFA kutoa kwa mchezaji au kocha kuhusiana na suala la kupigwa kwa waamuzi ambalo limekuwa likikua kwa kasi kubwa kila siku zinavyosonga mbele.

Unaweza kusema Zanzibar ni kama wanasubiri kifo cha mwamuzi, halafu baada ya hapo waanze kulishughulikia kwa kina suala hilo.

Adhabu ya Shuber kufungiwa kwa mwaka mmoja ndiyo kubwa zaidi ukilinganisha na awali adhabu zilizokuwa zikitolewa, suala la kuwapiga waamuzi lilionekana ni kama la kawaida tu.

Ilifikia wakati, mashabiki walitangaza kuandaa Sh milioni 2 kwa ajili ya kununua sanda za waamuzi ambao walijibu mapigo kugomea kuchezesha mechi ya timu yao kwa kuhofia maisha yao.

ZFA wanaonyesha kuna uzembe, lakini swali lingine, vipi kuhusiana na ulinzi katika viwanja hivyo. Jeshi la Polisi visiwani humo pia ni wazembe?

Kumbukumbu chache za waamuzi kupigwa ziko hivi:

Aprili 8, 2013
Katika mechi kati ya Malindi na Chipukizi kwenye Uwanja wa Gombani, mwamuzi msaidizi namba moja, Mohamed Seif alijikuta akiwa katika wakati mgumu baada ya kocha wa Malindi, Mohamed Shuberi kwenda kumvamia na kumkaba shingo.

Machi 28, 2013
Mwamuzi wa Ali Mohamed ‘Anko Saleh’, alilazimika kuyakumbuka mafunzo ya Polisi Moshi na kujihami kwa kupangua ngumi alizokuwa akipigwa huku akirusha mateke na ngumi kwa baadhi ya wapenzi wanao sadikiwa kuwa ni timu ya Selemu Renger, waliomvamia.

Baadaye viongozi walijitokeza na kuanza kuamua mgogoro huo, Anko Saleh alijikuta akiwa katika wakati mgumu, baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Daraja la Kwanza Pemba, kati ya FSC na Selemu Ranger. Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Gombani. FSC ilishinda bao 1-0.

Machi 20, 2013
ZFA Taifa Pemba iliitoza timu ya Daraja la Kwanza ya African Kivumbi faini ya Sh 200,000 baada ya kusababisha vurugu katika pambano lake dhidi ya timu ya Small Tiger katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kangani Skuli.

Februari 13, 2013
Waamuzi nane wa visiwani hapa walitangaza kugoma kuichezesha Hard Rock kutokana na mashabiki wake kusema wametenga kitita cha shilingi milioni mbili kwa ajili ya kununulia sanda za waamuzi.

Katika barua iliyoandikwa na waamuzi hao wanaochezesha ligi mbalimbali kisiwani Pemba na kutumwa kwa Katibu Msaidizi wa ZFA Taifa Pemba, waamuzi hao walisema hawapo tayari kuchezesha mechi za timu hiyo kutokana na kauli hiyo ya vitisho.

Maana yake
Ukiangalia matukio hayo, utagundua Ligi Kuu ya Zanzibar (Unguja na Pemba) zimejaa madudu lukuki na huenda uongozi wa ZFA haukuwa ukilichukulia suala hilo kwa uzito wa juu.

Inawezekana waamuzi hawalindwi, lakini sheria za ZFA hazina meno ya kutosha kuwatisha waovu lakini uongozi wa chama cha waamuzi unaweza usiwe makini kwa kuzalisha waamuzi bora.

Lakini viongozi na mashabiki wa timu za Zanzibar kwa jumla wanaweza pia wasiwe waungwana kwa kuwa wanachukua sheria mkononi, kitu ambacho ni hatari na itafikia siku wasababishe mauaji, kisha waangukie katika vyombo vya sheria ambako wataishia gerezani kwa kushindwa kuzuia jazba.

Kuna njia sahihi za kuchukua hatua na si kupiga au kutishia kwa silaha. Badilikeni, soka ni mchezo wa furaha na ajira. Sehemu kadhaa soka imesaidia kurudisha amani, lakini Unguja na Pemba, mnautumia mchezo huo kutengeneza maafa bila ya sababu zozote za msingi.

Mwisho nampa pongezi, Abdi Suleiman mwandishi wa Championi visiwani humo kutokana na kufichua kila kinachoendelea ambayo ni picha halisi.

SOURCE: CHAMPIONI NEWSPAPER

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic