Kamati ya Mashindano ya Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) inakutana Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kupitia maandalizi
ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) iliyopangwa kuanza Mei 12 mwaka huu.
Tayari mikoa 18 kati ya 27 kimpira
imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya RCL itakayotoa timu tatu zitakazopanda
daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014).
Kamati hiyo chini ya Uenyekiti wa
Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF itapokea
taarifa ya maandalizi ya ligi hiyo kutoka Idara ya Mashindano ya TFF na kufanya
uamuzi juu ya mikoa ambayo haijawasilisha mabingwa wao.
Ligi hiyo itachezwa kwa mtindo wa
nyumbani na ugenini, na ratiba (draw) itapangwa wakati wowote. Ada ya kushiriki
ligi hiyo kwa kila klabu ni sh. 100,000 na usajili utakaotumika na ule ule wa
ligi ngazi ya mkoa. Hakutakuwa na usajili mpya wa wachezaji.
0 COMMENTS:
Post a Comment