Na Saleh Ally
KUTOKANA na mwendo mzuri wa timu ya
taifa ya soka, Taifa Stars, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
imeunda kamati ya Saidia Taifa Stars ishinde.
Kamati hiyo itaongozwa na Mwenyekiti,
Mohammed Dewji ambaye ni Mbunge wa CCM (singida Mjini). Hakuna asiyejua uzoefu
wa Mo katika masuala ya mchezo wa soka.
Kamati hiyo ina watu wengi tu ambao
wanaweza kupambana kwa ajili ya Taifa Stars kama Mkurugenzi wa Shirika la Taifa
la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ramadhani Dau. Mbunge wa Kigoma Mjini (Chadema) Zitto
Kabwe, mdau Teddy Mapunda na Dioniz Malinzi.
Niseme ninaiamini kamati hiyo kwamba
inaweza ikafanya vizuri na kupambana kusaidia joto la ushindi katika mechi
ngumu za Stars kama hiyo dhidi ya Morocco, ugenini na pia Ivory Coast hapa
nyumbani.
Naiamini kamati kwa maana naona ina watu
wapambani, sitaki kuingia kwenye kuhoji kwamba wako ‘wanajeshi’ wengine
wameachwa nje. Najua huu si wakati wake, lakini kuna mambo nataka nikumbushe
kuigusa kamati hiyo ya Mo Dewji.
Kama nilivyoeleza awali kwamba kamati
ninaiamini, lakini kuna mambo kadhaa ya kufanya ambayo yataisaidia kamati hiyo
kufikia malengo yake, la sivyo itakuwa sehemu ya kuporomosha mambo kabisa na
kuivuruga morali ya Taifa Stars.
Lakini tukubali kuwa Stars hadi inafikia
hapo kulikuwa hakuna kamati, kwamba iliweza kufanya vizuri ikiwa chini ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ndilo lilikuwa linapigana jino kwa jino
kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri. Pia msiwasahau wadhamini wao Bia ya
Kilimanjaro.
Katika kamati hiyo hakuna mtu wa TFF,
inawezekana ikawa si lazima. Lakini kuna tatizo nimeliona mapema, kwamba
sijasikia mtu wa kamati katika mahojiano akizungumzia kuhusiana na kazi nzuri
iliyofanywa na shirikisho hilo.
Kamati isingeundwa kama Stars ingekuwa
katika nafasi ya ‘mashaka’, hivyo lazima TFF ipewe shukurani, lakini lazima
ihusishwe kwa ukaribu zaidi kwa kuwa inajua msingi na njia ilizopita Stars hadi
kufikia hapo ilipo.
Watu wa kamati wameonyesha mapema kama
vile ni wanajeshi wapya, wameingia kupambana. Lakini si wale wanaotaka kujua
wanajeshi waliofikisha timu hapo walifanya vipi. Hilo ni kosa, TFF ipewe
heshima yake, pia ipewe nafasi ya ushiriki wa karibu kwa kuwa ndiyo mhimili.
Kocha:
Bado nasisitiza, inapofikia wakati watu
wa kamati wanataka kwenda kuzungumza na wachezaji kwenye kambo ya Taifa Stars,
basi lazima TFF ihusishwe na kujua nini kinaendela.
Lakini muhimu zaidi ni kuheshimu ratiba
ya kocha Kim Poulsen inasemaje. Msithubutu kufanya mambo kisiasa au kuangalia
hamasa zaidi kuliko hali halisi inayohusu maandalizi.
Kama mwalimu atataka timu ipumzike, basi
iwe hivyo na kusiwe na mjadala. Kwa kuwa haitakuwa na maana kama mtaingilia
maandalizi kwa maana ya kuhamasisha, itakuwa kichekesho.
Mikakati:
Juzi, kamati hiyo imetoa Sh milioni 30
kwa Taifa Stars kama zawadi na kujenga morali. Jambo zuri sana, lakini lazima
tukubaliane kutoa fedha pekee hakuwezi kuwa kila kusaidia kufanikiwa na kuibuka
na ushindi dhidi ya Morocco.
Soka ina mipango, soka ina mapambano ya
nje na ndani ya uwanja. Hivyo kamati inapaswa ijipange vilivyo na kuhakikisha
ushindi na kufanya kazi ya ziada kwa kuwa jukumu walilokabidhiwa si lelemama na
haliwezi kufanikiwa kwa kutoa motisha tu, badala yake wanatakiwa kuingia
‘msituni’ na kupambana.
Umakini:
Watu wote wa kamati ni “watu wa mpira”,
hilo hali ubishi. Hofu yangu ni moja na ni vema nikaanza na mfano. Wakati
fulani kuna mdau mmoja aliwahi kwenda katika kambi ya timu ya taifa, alikuwa
anajulikana kama sehemu ya wahusika wa Stars kama ilivyo leo kwa watu wa
kamati.
Alipofika pale akatoa jozi mbili za
viatu na kumkabidhi mchezaji mmoja, hali ambayo baadaye ilizua mzozo wa
chinichini katika kambi hiyo.
Inawezekana kabisa nia yake ilikuwa
nzuri na mchezaji aliyepewa huenda aliomba msaada wa viatu. Lakini kwa kuwa
aliyetoa alijulikana kama mhusika, tayari ikawa tatizo. Hilo ndilo ninataka
kusisitiza kwamba lazima kuwe na umakini sana katika kushiriki na wachezaji.
Umakini hasa katika utoaji vitu na suala
la usawa, vizuri
kuwasaidia wote au kuacha. Kwani akionekana mtu wa kamati
anamsaidia zaidi mchezaji au wachezaji fulani, tayari itazua mgawanyiko kupitia
moyoni na mwisho morali “itauwawa” badala ya kuiimarisha.
Kuua morali na kusaidia timu ni sawa na
kumpigia mbuzi gitaa, ndiyo maana nasisitiza sana suala la umakini katika hilo
ili kamati iweze kuwa na matunda.
Sitaki kusema mengi, nimaamini
nimeaminika kwa maana ya kusisitiza usawa, heshima kwa kocha, heshima na
kuwajali TFF na wadhamini wao, Bia ya Kilimanjaro kama walioanza mbali na timu
hadi kufikia walipo badala ya kamati kujiiona ina uwezo wa kila kitu bila ya
kujua timu imefikaje ilipo.
Good observation man, Kamati inabidi iangalie jambo hili. Linaweza kuonekana dogo sana, lakini likawa na madhara makubwa baadaye.
ReplyDeleteabel