May 17, 2013



 
Mashabiki Simba...

Na Saleh Ally
MECHI ya kesho kati ya Simba dhidi ya Yanga imebadilika ghafla, gumzo lake limepanda kwa kasi katika kipindi cha siku tatu sasa.

Awali ilionekana kama itakuwa kama mechi lahisi, lakini ushindi wa mwisho wa zaidi ya mechi nne wa Simba, kidogo umefanya mambo yabadilike na inaonekana Yanga wameamka na kuona haitakuwa kazi lahisi, hiyo ndiyo imeongeza joto hilo.
 
Mashabiki Yanga..
Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts amekuwa akitoa onyo mara kadhaa kwa wachezaji wake, kwamba Simba si timu dhaifu, hivyo lazima wajue kazi ni ngumu. 

Kuna mambo mengi lakini uwanjani hakika ufundi utatoa majibu mengi sana, makocha wa timu zote mbili na wachezaji watakuwa na kazi ya kufikisha kinachotakiwa kwa ajili ya kufanikisha wanacholenga.


Kwa takwimu inaonekana karibu kila kitu Yanga iko juu, unaweza kuangalia mfano ule wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Bayern Munich inaonekana iko juu kitakwimu kuliko Borussia Dortmund. Lakini hilo haliwezi  kuwa jibu la mechi kwamba mshindi ni fulani.

Kawaida soka, lazima watu waingie uwanjani na baada ya hapo majibu yatapatikana baada ya hesabu za kutosha kupigwa, tena hadharani bila ya kificho.

Wafungaji:
Yanga inaonyesha ina safu kali ya ushambuliaji, katika mechi 25 imefunga mabao 45 huku ikiwa na washambuliaji wake wawili walio juu katika orodha ya wafungaji bora.

Kipre Tchetche wa Azam FC ndiye kinara akiwa na mabao 17, anafuatiwa na Didier Kavumbagu wa Yanga mwenye mabao tisa kama Paul Nonga wa Oljoro na nafasi inayofuatia ni Jerry Tegete wa Yanga mwenye mabao nane.
Simba haina mshambuliaji mwenye makali zaidi, hata katika listi ya wafungaji bora hakuna, kiungo wake mkongwe, Amri Kiemba ‘Baba Shabani’ ana mabao saba na ndiye kinara Msimbazi.

Ulinzi:
Bado Yanga inaonyesha imefanya ulinzi mkali zaidi kuliko Simba katika mechi 25 walizocheza. Jangwani wameruhusu mabao 14 tu na kuwa timu yenye ngome ngumu zaidi inayoongoza na Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Simba imeruhusu mabao 23 ambayo ni karibu mara mbili ya Yanga.

 Viungo:
Kila upande uko sawa, Yanga wana Haruna Niyonzima na Athumani Idd ‘Chuji’, lakini Mrisho Ngassa ndiye anayeongoza kwa kutoa pasi nyingi za mabao. Inaelezwa amepiga 10 ambazo hazijafikiwa na yoyote.
Lakini Kiemba anaonekana ndiye kiungo hatari zaidi katika Ligi Kuu Bara, kwani pamoja na kufunga mabao mengi kuliko kiungo mwingine yoyote, ndiye ameonakana mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kuchezesha timu.

Muhimu hapa kwa Simba inaonekana ni timu yenye viungo bora kwa misimu mitatu mfululizo na mara nyingi wafungaji bora wake huwa ni viungo kama ilivyokuwa kwa Emmanuel Okwi na marehemu Patrick Mutesa Mafisango.


Hatari:
Inaweza kuwa hatari kwa Yanga kama watajisahau na kuwadharau makinda wa Simba, ni wachezaji wasiokuwa na majina lakini wenye uwezo mkubwa sana. Kupambana na usiyejua uwezo wake pia inahitaji umakini maradufu kuliko unayejua anacheza vipi.

Makocha:
Brandts itakuwa mechi yake ya pili, wakati anaanza kazi kwa mara ya kwanza alikutana na Simba na kupata sare ya bao 1-1, Kiemba akiwa ametangulia kufunga na Said Bahanuzi akasawazisha kwa mkwaju wa penalti.

Mholanzi huyo anaweza kuwa ameona kazi ya mechi hiyo ya watani na joto lake liko vipi. Mfaransa Patrick Liewig hapaswi kufanya mzaha hata mdogo, mechi hiyo ni kubwa na hilo halikwepeki.
Lazima ajue kuna utofauti na ushindi muhimu, hivyo lazima umakini uongezeke maradufu lakini hesabu za kutambua Yanga imeimarika ndiyo maana imechukua ubingwa mapema, hivyo wanakutana na kikosi bora kwenye ligi, lakini hakuna kizuizi kwamba wakiwa makini na kukamilisha kiufasaha mipango kama wanayo madhubuti, basi watashinda.

Makosa&nafasi:
Dali zinaonyesha kama kawaida, kabla ya kuanza kwa mecho hiyo, matokeo ni bao 0-0. Matokeo hayo yanaweza kubadilishwa kwa vitu viwili tu, upande mmoja kufanya makosa na mwingine kuyatua kwa faida.
Lakini inawezekana kabisa, kila upande ukafanya makosa halafu kila upande ukashindwa kuyatumia, basi mwisho matokeo yatakua yaleyale waliyoanza nayo ya 0-0.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic