May 3, 2013



Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limetangaza rasmi kufuta uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kutaka mchakato uanze upya.

Pamoja na hivyo, Fifa wametaka kuundwa kwa kamati ya hadhi na maadili ambayo itakuwa na kazi ya kufanya mchanganuo kuhusiana na haki za wagombea na si wao TFF.


Kamati hiyo ndiyo itakuwa na nguvu ya kusema mtu fulani ana haki ya kugombea au la, kwa mujibu wa Fifa wanaona hilo ndilo sahihi na TFF wameagizwa kuhakikisha kila kitu kinakuwa tayari kabla ya Oktoba.

Sharti lingine, kamati hiyo inatakiwa kuwa chini ya mwanasheria kwa kuwa mambo mengi yatakuwa yanahusiana na sheria.

Sitaki kuingia katika hisia wala makundi ambayo yalionekana wazi kuutafuta uchaguzi wa TFF ambao ulikuwa umejaa zengwe kuliko hali halisi hadi ulipofikia.

Lakini kwa hali ninavyoiona, bado ni sawa na kuuzunguka mbuyu halafu siku ya mwisho tunarudi palepale tukiamini kwamba kila kitu kilikwenda vizuri, lakini tumepoteza muda.

Kamati hiyo ya hadhi na maadili, bado itakuwa na uwezo wa kusema Jamal Malinzi au Michael Wambura hana sifa, halafu tutarudi kulekule baada ya kuwa imepotea zaidi ya miezi mitano mchakato huo ukiendelea.

Picha ya mbele inanionyesha ni kama Fifa waliamua wapoze joto hilo kwa muda fulani, ninasema hivi naona siasa kama imetumika zaidi bila ya kujali muda unaopotea.

Mfano, kinaweza kikatumika kigezo cha kuendelea kuwaacha akina Tenga madarakaniw akati wamemaliza muda wao kwa kuwa wanashughulikia mchakato huo walioagizwa na Fifa.

Siku ya mwisho, atatokea mtu na kusema walioshughulikia mchakato walikuwa madarakani batili kwa kuwa hawakupata idhini ya kukaa pale kutoka kwa mkutano mkuu.

Fifa imeamua hivyo baada ya kubaini kasoro chungu nzima ikiwemo kuwaagiza kufanyia marekebisho katiba yao na  waunde kamati ya maadili ambayo hiyo ndio itakuwa na jukumu la kusema huyu hana uadilifu na sio kamati ya uchaguzi ambayo ilikuwa ndio hakimu wa kila kitu.

Hivyo TFF sasa haina budi kurudi tena kwa wajumbe wao wa mkutano mkuu kwa  kuitisha mkutano mkuu ambao naamini hawakuwa wakiutaka maana safari ile walishindwa kuitisha kwa vile hawakuwa na hela na wakatumia njia ya waraka na hatimaye kupitisha katiba japo ilipingwa sana.

Tumefikaje kote huku? Hili ndio swali la kujiuliza na mara kadhaa niliwahi kuandika kuwa Kamati ya rufaa za uchaguzi chini ya uenyekiti wake Idd Mtiginjola ndio ilitufikisha hapa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic