Milovan akifanya mahojiano na Saleh Ally, mara baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara mzunguko wa kwanza kati ya Yanga na Simba iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1... |
Na Saleh Ally
MILOVAN Cirkovic ameingia katika rekodi
kati ya makocha waliowahi kuzifundisha moja ya timu kubwa za Tanzania, lakini
kikubwa zaidi ni kuiwezesha moja kushinda kwa mabao mengi katika mechi
inayokutanisha watani.
Ushindi mkubwa zaidi katika mechi za
watani nchini ni ule wa mwaka 1977 wakati Simba ilipoishindilia Yanga kwa mabao
6-0.
Lakini kuanzia miaka ya 1980, 1990 na
2000, Milovan raia wa Serbia ndiye anashikilia rekodi ya kuwa kocha aliyepata
ushindi mnono zaidi katika mechi ya watani.
Milovan aliiongoza Simba kuichapa Yanga
mabao 5-0 katika mechi ya mwisho msimu uliopita, wakati huo Yanga ilikuwa
ikitafuta heshima baada ya kuwa imeangukia katika nafasi ya tatu, nafasi ambayo
ilikuwa haijawahi kuishika tokea mwaka 1988, mara zote ilikuwa bingwa au nafasi
ya pili.
Kesho Simba na Yanga zinarudi uwanjani,
‘hadithi’ za mechi hiyo hazina tofauti kabisa na mechi iliyopita, kama
ilivyokuwa Simba bingwa msimu uliopita, zamu hii ni Yanga na Msimbazi
wanaendelea kutafuta nafasi ya tatu na wanataka waishinde Yanga.
Yanga ambao ni mabingwa, wanataka
kushinda kwa ajili ya kusherekea kombea lao raha mustarehe lakini kuanzia
viongozi, makocha, wachezaji na hata mashabiki wanachotaka ni kulipa kisasi cha
mabao 5-0 waliyofungwa katika mechi ya kufunga msimu uliopita.
Yanga nao wanataka kufunga msimu kwa
heshima na kikubwa ni kurudisha adhabu ya kipigo na ikiwezekana tano zote
zirudi. Katika mechi hiyo mabao ya Simba
yalifungwa na Abdallah Kibadeni dk 10, 42, 89, Jumanne Masimenti
dk 60, 73 na Selemani Saidi wa Yanga aliyejifunga katika dk 20.
Milovan ambaye sasa amerejea anaishi
katika mji aliozaliwa wa Cacak nchini Serbia anasema kama ni soka pekee bila ya
mipango mingine yoyote, Yanga haina uwezo wa kuifunga Simba bao 5-0.
Mahojiano kati ya Salehjembe na Milovan
kutoka Serbia yalikuwa hivi:
Salehjembe: Yanga wanajiamini sana na
wanaamini kuishinda Simba ni lazima?
Milovan: Wanakosea, mpira hauchezwi kwa
hisia, lazima ujipange, uingie uwanjani na kuanza kutafuta matokeo.
Salehjembe: Kama ilivyokuwa Simba, timu
bora msimu uliopita, safari hii ni Yanga. Hauoni wana haki ya kujiamini kwa
watashinda tena kwa idadi kubwa?
Milovan: Kujiamini ni haki yao, hamuwezi
kwenda uwanjani hamjiamini. Lakini kuifunga Simba itabidi wacheze kwa mipango
zaidi na kuwazidi lakini si kuamini hivyo kabla ya kucheza.
Salehjembe: Inawezekana wakashinda mabao
matano na kulipa kisasi?
Milovan: (kicheko), Yanga watakosea
zaidi kuanza kuwaza bao tano wakati hawajafunga hata moja. Hilo ni kosa.
Salehjembe: Kwani wanatakiwa kuwaza
vipi?
Milovan: Kawaida ukifunga bao moja,
unafikiria la pili, ukifunga la tatu unapanga la nne. Hivyo ndivyo mambo
yanakwenda.
Salehjembe: Nakumbuka siku chache kabla
ya mechi ya Yanga mlioshinda tano, ulisema mnaweza kushinda tano?
Milovan: Kweli, nilisema tunaweza.
Sikwenda nasema tunakwenda kuishinda tano, badala yake niliamini inawezekana,
lakini isingekuwa hivyo kusingekuwa na tatizo nilichotaka ni ushindi. Lakini
Yanga wanataka tano tu, hilo ni kosa.
Salehjembe: Unakionaje kikosi cha Simba?
Milovan: Simba ni timu yenye vikosi bora
Tanzania, utaona pamoja na matatizo yote iko katika nafasi ya tatu. Maana yake,
Yanga hawapaswi kuidharau, wanaweza kujikuta wanashangaa.
Salehjembe: Nilifikiri ungekuja
kuangalia mechi hiyo ya Jumamosi?
Milovan: Nilitamani maana wanaocheza ni
vijana wangu, nawapenda na kuwakumbuka sana. Lakini sitaweza ila nitafuatilia
kila kitu kupitia mitandao. Tanzania bado ni rafiki wengi na ninakupenda sana.
Salehjembe: Nashukuru kwa ushirikiano
Profesa Cirko.
Milovan: Nashukuru, wewe matatizo sana...
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment