Uongozi wa klabu ya Simba umeanza kusaka kimyakimya
kipa mwingine kwa ajili ya kuimarisha kikosi.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hizo
zinaeleza, tayari Simba imeanza kufanya mazungumzo na makipa kadhaa wanaocheza
katika timu za Ligi Kuu Bara.
Tayari Simba ina makipa wawili wa kimataifa ambao
ni Juma Kaseja ambaye ni nahodha wa Taifa Stars na Abel Dhaira ambaye ni kipa
wa timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’.
Uamuzi huo wa Simba unaonekana kuwashtua wengi kwa
kuwa kama itasajili kipa mwingine, maana yake kati ya Kaseja au Dhaira mmoja
atalazimika kuondoka.
“Uamuzi huu umeishajadiliwa na kamati ya ufundi na
suala hilo likapelekwa katika kamati ya usajili, hivyo limeanza kufanyiwa kazi.
“Kidogo hata sisi linatugawanya kidogo kwa kuwa
hatujui nani ataendelea kubaki kati ya Kaseja na Dhaira. Maana kama ni makipa
hao wangebaki wanatosha sana,” kilieleza chanzo.
Pamoja na kutua kwa Dhaira, lakini Kaseja
aliendelea kudaka mechi nyingi zaidi baada ya kuonekana ana kiwango bora zaidi.
Hivi karibuni Simba wamekuwa wakimpa nafasi Dhaira
ambaye mashabiki walikuwa wana hamu ya kumuona akicheza.
Huenda wamemchoka Kaseja ambaye alitua Simba mwaka
2002 na kuanza kuichezea mechi za mashindano mwaka 2003. Lakini bado ameendelea
kuwa kipa bora zaidi Tanzania Bara kwa kipindi kirefu.
0 COMMENTS:
Post a Comment