Bin Slum ofisini kwake Kariakoo jijini Dar es Salaam |
*ASISITIZA
YEYE NI COASTAL TOKEA MDOGO MWANZO MWISHO, AZIKANA SIMBA, YANGA
Na Saleh Ally
KUTOKANA na mambo yanavyokwenda Coastal
Union inaonekana kuwa moja ya timu zitakazokuwa tishio kubwa msimu ujao.
Coastal Union ni moja ya timu kubwa
katika soka ya Tanzania, lakini ilionyesha kupoteza mwelekeo hadi iliporejea
tena ligi kuu misimu miwili iliyopita.
Mohammed Bin Slum ni kati ya watu
waliokuwa wakitoa msaada katika Coastal Union tokea ikiwa katika hali mbaya
hadi sasa imeonyesha kuwa si timu ya kubahatisha mambo.
Msimu uliopita imemaliza ikiwa katika
tano bora, mafanikio yake yanaonyesha timu hiyo inaweza kurejea katika heshima
yake ya enzi zile ikiwa moja ya timu tishio kabisa.
Hata usajili wake wa msimu huu, tayari
unaonyesha Coastal Union ni kati ya “Big Four” za Ligi Kuu Tanzania Bara. Timu nyingine
ni Yanga, Simba na Azam FC ambayo tayari imejihakikishia tatu bora tena ikiwa
nafasi ya pili kwa misimu miwili mfululizo.
Lakini yote hayo na mafanikio ya Coastal
Union, vigumu ukayazungumzia bila ya kuitaja ‘injini’, Bin Slum ambaye sasa
pamoja na kuwa mdhamini, anashikilia nafasi ya mkurugenzi wa ufundi katika
klabu hiyo.
Juhudi za Bin Slum ingawa alizianza muda
mrefu tena kimyakimya lengo likiwa ni kuisaidia Coastal Union, sasa zinaanza
kuonekana hadharani na mwenyewe anasisitiza “atakufa na Coastal Union” maarufu
kama Wagosi wa Kaya.
Bin Slum aliyezaliwa Tanga na kupata
elimu yake mkoani humo hadi kidato cha sita kabla ya kuhamia jijini Dar es
Salaam ambako alianza maisha yake ya biashara, anaamini Coastal Union ina
nafasi ya kurejea katika kilele na kuanza kusumbua kama ilivyotwaa ubingwa wa
Tanzania Bara mwaka 1988.
Bin Slum ambaye ni mmoja wa wachezaji wa
zamani wa timu ya mkoa wa Tanga, maarufu kama Tanga Stars anasema yeye amekuwa
shabiki wa Coastal Union tokea azaliwe.
Kingine ambacho anaeleza na huenda
kikawashangaza wengi ni kwamba hajawahi kuingia hata mara moja uwanjani katika
mechi kubwa kuliko zote za soka ya Tanzania ambayo kawaida huwakutanisha watani
wa jadi, Yanga na Simba.
Salehjembe: Inashangaza kidogo kwa
mfadhili wa timu kubwa kama Coastal, mdau wa soka kusema hujawahi kuingia
katika mechi kubwa ya watani?
Bin Slum: Kwani kuna ulazima gani
kuingia kwa kuwa mimi si Simba wala Yanga.
Salehjembe: Haushabikii timu moja kati
ya hizo?
Bin Slum: Haijawahi kutokea, nimekuwa
Coastal Union tokea utoto hadi leo.
Salehjembe: Kipi kinafanya usiende
katika mechi inayowakutanisha watani Yanga na Simba?
Bin Slum: Kwanza bugudha ya kuingia na
kutoka uwanjani kwa kuwa watu ni wengi, lakini hakuna timu ninayoishangilia. Nimewahi
kuangalia mechi ya Simba dhidi ya Yanga kwenye tv ilipokuwa inaonyeshwa na
Supersport. Ukiachana na hivyo sijawahi kwenda uwanjani.
Salehjembe: Maana yake hujawahi kuziona
Yanga na Simba zikicheza live?
Bin Slum: Nimewahi, lakini labda iwe
Simba na JKT au Yanga na timu nyingine lakini si siku zinapokutana zenyewe.
Salehjembe: Unafikiri inawezekaan mtu
kuwa shabiki wa soka hapa nchini bila kupenda Yanga au Simba?
Bin Slum: Kabisa, mimi ni mmoja wapo. Mimi
si Yanga au Simba kama nilivyokueleza. Watu hawaelewi na wanaona haiwezekani.
Salehjembe: Kivipi? Fafanua tafadhari.
Bin Slum: Mimi Coastal wa kuzaliwa
kabisa, tokea mdogo baba yangu alikuwa akinishika mkono na tunakwenda wote
uwanjani. Hivyo sijawahi kushabikia timu nyingine hapa nyumbani, zaidi kama
England ni Liverpool lakini si Simba wala Yanga.
Salehjembe: Wengi wanaamini haiwezekani,
kwako imekuwa vipi lahisi?
Bin Slum: Wengine wamezichagua Simba au
Yanga, lakini mimi nimeanza kuipenda Coastal Union nikiwa mtoto. Ndiyo maana
hata ilipokuwa daraja la kwanza nilikuwa tayari kwenda hadi viwanja kama
Mabatini kwenda kuona inacheza. Mfano mechi ya Simba na Yanga ya kufunga msimu,
mimi nilikuwa Morogoro kwa kuwa Coastal ilikuwa inacheza.
Katika mechi hiyo Coastal isingechukua
ubingwa wala nafasi ya pili, lakini kwangu ni bora kusafiri hadi Morogoro
kuiona Coastal Union inacheza kuliko kuona Simba na Yanga Dar es Salaam.
Salehjembe: Vipi kuhusu usajili wa
Coastal Union?
Bin Slum:Kwa kushirikiana, ninamini
tumefanya usajili vizuri sana. Coastal union itafanya vizuri zaidi ya msimu
uliopita.
ITAENDELEA SEHEMU YA PILI NA YA MWISHO…
0 COMMENTS:
Post a Comment