Na Saleh Ally
GUMZO
katika soka la Ivory Coast kwa kipindi hiki ni kocha mpya wa timu ya taifa ya
nchi hiyo, Sabri Lamouchi, ambaye amechukua uamuzi mgumu ambao umewashangaza
wengi.
Lamouchi
raia wa Ufaransa akiwa na asili ya Tunisia ameamua kumuacha nahodha wa timu
hiyo, Didier Drogba, tena katika kipindi kigumu wakati timu yake ikiwa katika
mbio za kupata nafasi ya kubeba ubingwa.
Pamoja na
hivyo, Lamouchi amemuacha beki mkongwe wa kati, Kolo Toure, na kuamua kutumia
vijana zaidi katika mapambano ya kuwania kucheza Kombe la Dunia mwakani nchini
Brazil.
Championi
Jumatatu, lilifanya mahojiano maalum na Lamouchi saa chache kabla ya mechi ya
jana dhidi ya Taifa Stars na akazungumzia mambo kadhaa.
Lamouchi ni
kiungo mahiri wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, lakini alikipiga katika
klabu kubwa kama Ales, Auxerre, Monaco za Ufaransa, Parma na Inter Milan za
Italia.
Pamoja na
kusisitiza kwamba wamekuwa na maandalizi makubwa kabla ya mechi dhidi ya
Tanzania kuliko kawaida, lakini amelenga zaidi kujenga nidhamu upya kwa kuwa
timu nyingi za Afrika Magharibi zilikumbana na suala la ukosefu wa nidhamu.
Pamoja na
hivyo, Lamouchi akasisitiza Drogba bado anaendelea kuwa nahodha wa timu hiyo na
ana nafasi kubwa ya kurejea katika kikosi hicho huku akiona nafasi kama hiyo
kwa Kolo ingawa anaiona ni ndogo sana.
Salehjembe:
Vipi maandalizi dhidi ya Tanzania yawe makubwa kiasi hicho wakati ni timu
ndogo?
Lamouchi:
Tanzania si timu ndogo tena, angalia mechi dhidi yao kule Abidjan, haikuwa kazi
rahisi kuwafunga. Lakini mechi hii ni kama fainali kwetu.
Salehjembe:
Fainali huenda ikawa dhidi ya Morocco na si Tanzania.
Lamouchi:
Tukishinda dhidi ya Tanzania, maana yake tumebakiza asilimia kumi tu ambayo
tutaweka nguvu zote.
Salehjembe:
Umemuacha Drogba, Kolo. Huoni ni presha kubwa ukipoteza nafasi ya kucheza Kombe
la Dunia?
Lamouchi:
Inawezekana kupoteza ingawa hatutaki itokee. Lakini ikitokea pia si presha, hii
ni Ivory Coast na kila mchezaji mwenye uwezo ana haki ya kuisaidia nchi yake
hasa kama nimeona anafaa kufanya hivyo.
Salehjembe:
Drogba na Kolo wana nafasi ya kurejea kikosini, au uzee tayari ni tatizo?
Lamouchi:
Drogba ana nafasi kubwa, ninaamini atarejea. Kiasi alipoteza kidogo kasi
alipokuwa China, inawezekana kutokana na ligi yenyewe.
Lakini sasa yuko Uturuki
, ligi ngumu na yenye ushindani, pia amecheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hivyo ni
suala la wakati tu.
Kuhusu
uzee, Drogba hajafikia huko ingawa umri umekwenda. Bado anaweza kuwa na msaada
mkubwa kutegemeana na mechi. Ndiyo maana timu kubwa kama Galatasaray inaweza
kumuamini.
Salehjembe:
Vipi kuhusu Kolo?
Lamouchi: Sidhani
kama naweza kusema ana nafasi kubwa, kuna vijana wengi wanaocheza kwenye nafasi
yake kwa ubora zaidi. Lakini inaweza kutokea nikamuita. Ingawa ni vizuri kusema
hana nafasi.
Salehjembe:
Unafikiri Yaya, Gervinho na Kalou ndiyo tegemeo pekee la Ivory Coast?
Lamouchi:
Hilo ni kosa kubwa, pia nimekuwa nikiwakumbusha wachezaji wote kwa kuwa nina
uzoefu wakati nikiwa mchezaji. Kila mchezaji anayekuwa katika kikosi, pia
kwenye benchi ni tegemeo la timu. Kocha haangalii majina, anaangalia nani ana
msaada katika wakati husika.
Salehjembe:
Baada ya Ivory Coast, unafikiri utaendelea kufundisha timu nyingine za Afrika
au utarejea kufanya kazi katika klabu za Ulaya?
Lamouchi:
Nilikuwa mchezaji, sasa ni kocha. Chochote kitakachokuwa bora, kama ni klabu
kubwa ya Ulaya au timu ya taifa ya Afrika. Litakuwa ni suala la maslahi, lakini
si pekee kwa kuwa nina ndoto nataka kuzitimiza.
Salehjembe:
Ndoto zipi?
Lamouchi:
Zitabaki kuwa siri yangu, siku moja zikitimia nitasema.
Salehjembe:
Nashukuru.
Lamouchi:
Sawa.
Baadaye
jana jioni Ivory Coast iliifunga Stars kwa mabao 4-2 na kuitoa kwenye reli
kabisa ya kuendelea kuwania kutaka kucheza Kombe la Dunia mwakani.
Mechi ilikuwa
nzuri na yenye mvuto, lakini tatizo kubwa likawa ni umakini katika uchezaji wa
kikosi cha Stars hasa wakati kikosi kinashambuliwa.
Stars haikuwa
na safu ngumu ya ulinzi kwa maana ya kikosi kizima kuimarisha safu yake.
Lakini kwa
makosa ya mchezaji mmoja mmoja, beki Erasto Nyoni pia alishinda kumthibiti Gervinho
ambaye alimgeuza njia.










0 COMMENTS:
Post a Comment