Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Liewig yuko jijini Dar es Salaam akisubiri kulipwa
fedha zake baada ya uongozi wa timu hiyo kumfuta kazi.
Simba
imemfuta kazi Liewig raia wa Ufaransa baada ya kuamua kuvunja naye mkataba na
kumpa mzawa Abdallah Kibadeni na atasaidiwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’
aliyekuwa msaidizi wa Liewig.
Liewig
alikuwa analipwa dola 6,000 (zaidi ya Sh 9.7) kwa mwezi, mkataba wake
unaonyesha anatakiwa kulipwa mshahara wa miezi miwili.
Lakini kama
hiyo haitoshi inaonyesha Liewig alikuwa anaidai Simba mshahara wa miezi mingine
miwili na nusu, maana yake dola 15,000 (zaidi ya Sh milioni 24.5).
Ukijumlisha,
Liewig anaidai Simba Sh milioni 44.1 kiasi ambacho ni kikubwa kwa klabu hiyo
ukizingatiwa iko katika kipindi kigumu cha usajili na maandalizi ya msimu mpya.
Kwa kuwa
fedha ni ngumu, lazima kutakuwa na ugumu kwa vile Simba ina mahitaji mengi
muhimu, hilo halina ubishi. Lakini hakuna ujanja lazima walipe wanachodaiwa na
kocha huyo mtu mzima.
Tokea
amekuja, Championi lilikuwa la kwanza kufanya mahojiano naye na alisema
hahitaji malumbano na alichotaka ni kuhusiana na fedha zake, alipwe ili aondoke
kwa amani.
Hivyo ni
vizuri hilo likafanyika, alipwe fedha zake kama inavyotakiwa ili aondoke, kama
itashindikana kulipwa zote, basi alipwe kiasi fulani na mwisho kuwe na
makubaliano ambayo yatatekelezeka.
Simba
wanatakiwa kufanya hivyo hata kama wako katika hali ngumu kwa kuwa huo ndiyo
uamuzi sahihi kutokana na walichokiamua.
Tukirudi
miezi sita tu, tunakutana na saga la aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Milovan
Cirkovic raia wa Serbia ambaye alikuwa anadai takribani dola 33,000 baada ya
mkataba wake kuvunjwa.
Staili ya
kufukuzwa kwake haipishani na hii ya Liewig, naye alilazimika kurudi na kusaka
fedha zake na uongozi wa Simba ukashindwa kulipa ‘kwa makusudi’ hadi mlezi wao
Malkia wa Nyuki alipoamua kufuta aibu hiyo kubwa.
Sidhani
kama Malkia wa Nyuki anatakiwa kurudi tena na kufuta deni la Simba, uongozi
ulifikia uamuzi wa kumuondoa kocha huyo, basi lazima ulikuwa unajua cha
kufanya.
Walimuondoa
Milovan, mimi sikuona kama ni sawa hasa ukilinganisha na uwezo wa Liewig, Simba
wakasema wanamjua zaidi, leo wamemuondoa tena kwa mtindo uleule nao wakiwa
wamekubali kweli kama ulivyokuwa ufafanuzi wangu.
Vizuri
wakajiondoa katika kuonekana ni timu iliyojaa watu wasiojali heshima na jina la
timu hiyo na kuonekana ndiyo wanaoongoza kwa kudhulumu makocha.
Hakuna
ambacho Simba wanaweza kusema kama kisingizio, kwani uamuzi wa kumuondoa kocha
ulikuwa wa kwao. Unaweza kusema wanaitia hasara klabu kwa hesabu zinazolazimu
kutumia mamilioni ya fedha bila sababu za msingi.
Kuna
taarifa zinaeleza kwamba uongozi wa Simba umepanga kukutana na Liewig Jumapili
na kulijadili suala hilo ikiwezekana mwafaka upatikane.
Lakini kwa
heshima ya Simba na hali halisi, hawana ujanja ni lazima walipe, yaliyotokea
kwa Milovan yasirudie kwa Liewig maana itakuwa ni zaidi ya kuharibu.
Simba ni
klabu kubwa, hilo halina ubishi na inastahili heshima. Utekelezaji wa mambo kwa
uhakika ni sehemu ya heshima, kuwa na viongozi wasiobahatisha mambo ni sehemu
ya kuonyesha ukubwa wa Simba na ubora wa ufanisi wao, basi suala la Liewig
limalizwe kitaalamu zaidi.








0 COMMENTS:
Post a Comment