*Alonga kuhusu Nyoni, refa pia kuhusu Yaya Toure,
Gervinho
*Akubali makala ya Championi Jumatano kuhusu ukabaji
Na Saleh Ally
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen, amekubali kuwa
kuna makosa kadhaa walifanya katika mechi yao dhidi ya Ivory Coast na
kusababisha kupoteza mechi hiyo.
Stars ilifungwa mabao 4-2 na wageni wao Ivory Coast
katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Jumapili
iliyopita na kutoka katika mbio za kuwania kucheza Kombe la Dunia 2014 nchini
Brazil.
Katika mahojiano maalum yaliyofanyika Masaki jijini
Dar, Kim, raia wa Denmark, alisema walikosea mambo kadhaa katika ukabaji ambayo
yaliwaadhibu kwa kuwa walikuwa wakicheza dhidi ya wachezaji wenye kiwango bora
zaidi duniani kisoka.
Pamoja na hivyo, Poulsen alikubaliana na makala ya
uchambuzi kwa kutumia picha iliyoandikwa na Gazeti la Championi Jumatano
kuhusiana na kutokuwa makini na kutowakaba ipasavyo washambuliaji wa Ivory
Coast wakati Stars inashambuliwa.
Salehjembe: Safu ya ulinzi ilikuwa na matatizo
makubwa, utaona picha zinaonyesha kiasi gani mabeki wetu walivyokuwa wakisimama
mbali na washambuliaji wao wakati kwenye lango lao mabeki wao walikaba
kwelikweli hata kama fowadi wetu hana mpira, hilo vipi?
Kim: Kweli, makosa yalikuwepo na tumeyaona wote. Kabla
tulijadili lakini mwisho inawezekana hatukufanya kila tulichotaka kufanya, lakini
hakuna wa kulaumiwa kwa kuwa tumeharibu wote kama timu.
Salehjembe: Makosa unaweza kuyafafanua zaidi?
Kim: Ndiyo, utaona hatukuwa karibu na wachezaji kama
ulivyosema lakini tuliwapa nafasi kubwa zaidi wakati wanatushambulia.
Tulikumbushana lakini bado hatukuweza kumaliza tatizo.
Kikubwa cha kujua tulicheza na wachezaji wa kiwango
cha juu zaidi duniani, ukikosea, ujue umeumia.
Salehjembe: Kivipi?
Kim: Mfano angalia, sisi tulipata faulo zaidi ya nne
karibu na lango lao, tumepiga na kukosa zote. Wao wakapata mbili, moja
iliyopigwa na Yaya Toure wakafunga.
Hii inaonyesha kiasi gani wako makini zaidi. Ndiyo
maana nasema hata kama tumepoteza lakini hapa kuna suala kubwa la kujifunza.
Salehjembe: Vipi kuhusiana na Erasto Nyoni, ilionekana
kama ameshindwa kumdhibiti Gervinho?
Kim: Inawezekana, kuna matatizo yalikuwepo, lakini
bado hatuwezi kumuangushia Nyoni mzigo wote, utaona kuna mambo (Nadir Haroub) Cannavaro
na (Kelvin) Yondani walikosea, lakini kuna wakati viungo pia walikosea na
kusababisha makosa kwa mabeki.
Washambuliaji pia walishindwa kutumia nafasi au
kutulia. Ndiyo maana nasema hili ni kosa la timu na tunachotakiwa sasa ni
kujifunza na kuendeleza nguvu mbele. Kumbuka tumecheza na timu namba moja kwa
ubora wa soka barani Afrika.
Salehjembe: Huenda Nyoni alikuwa na hofu pia? Maana naona
kama bao la nne alionyesha kumhofia kabisa Gervinho wakati ana mpira!
Kim: Naungana nawe, huenda ilikuwa hivyo, baada ya
kusababisha penalti huenda aliingia woga, mbaya zaidi mashabiki walimzomea,
hakikuwa kitu kizuri. Nitakachofanya nitakaa naye na kuzungumza vizuri.
Nitakupa mfano, katika kikosi changu kwa mara ya
kwanza Ulimwengu alianza katika mechi ya Morocco tukiwa ugenini na
hakunifurahisha. Baada ya mechi nilikaa naye, tukazungumza na kumueleza makosa
yake na dhidi ya Ivory Coast nikampa nafasi tena ya kuanza, si unaona amefanya
vizuri. Hii ndiyo inatakiwa badala ya kumsakama mchezaji na kummaliza kabisa.
Salehjembe: Unaizungumziaje penalti?
Kim: Ninaweza kupishana na kila mtu, lakini haikuwa
penalti. Kweli Nyoni alimgusa Gervinho lakini si kwa kiwango cha kumuangusha,
naye alijiangusha na wote tuliona. Ila naamini udogo wetu, mataifa makubwa
yanapendelewa ndiyo maana tukafanyiwa vile. Mbona sikukataa penalti dhidi ya
Morocco ingawa nako haikuwa sawa Aggrey (Morris) kupewa kadi nyekundu!
Salehjembe: Unafikiri itafika siku tutakuwa tishio kwa
timu kama Ivory Coast?
Kim: Inawezekana kabisa, lakini tunahitaji muda kwa
kuwa tunajifunza. Wao wamejifunza mengi, ndiyo maana unapocheza dhidi ya wachezaji
kama Yaya, Gervinho na Salmon Kalou lazima uwe makini zaidi kuepuka makosa,
maana ukifanya kosa tu, umeumia.
Salehjembe: Nini unataka kufanya katika kikosi chako
ili kiwe bora zaidi?
Kim: Kupunguza makosa, hauwezi kuwa bora bila
kupunguza makosa kwa asilimia kubwa. Kama ulifanya kumi, vizuri ukapunguza,
yakifika mawili au matatu, basi utakuwa bora.
Salehjembe: Nini kinafuata baada ya hapo?
Kim: Ni kufuzu kucheza michuano ya Chan, lazima tupite
ili kwenda kupata mambo mapya kama kujiamini na uzoefu zaidi. Hivyo ni lazima
tuishinde Uganda katika mechi zote mbili.
Salehjembe: Bado kuna ugumu, mechi ya kwanza dhidi ya
Uganda utaanzia Dar?
Kim: Kweli, nilipenda tuanzie kwao, lakini ukiwa bora,
unaweza kupata matokeo mazuri Dar na baadaye kwao. Hivyo lazima tujiandae
vizuri katika mechi ya kwanza.
Salehjembe: Unafanya nini kuwarudisha wachezaji wako
katika hali ya kawaida kabla ya mechi ya Uganda, kwani huenda wameathirika
kisaikolojia na mechi dhidi ya Ivory Coast?
Kim: Kweli inawezekana, maana walilia sana, hawakupenda
yale matokeo. Niliwaambia kushangilia na kusikitika mwisho ni saa 24 baada ya
hapo unaanza kitu kipya.
Nitakaa nao kama timu lakini nitazungumza na mchezaji
mmojammoja ili kuwasisitiza kwamba tuna jukumu zito mbele yetu na Watanzania
wanatutegemea, hivyo lazima tuishinde Uganda na kuvuka.
Salehjembe: Hautakuwa na Samatta, Ulimwengu na huenda
John Bocco pia. Hauna mpango wa kuita mshambuliaji mwingine?
Kim: Nitasubiri kuhusu Bocco, lakini bado nimeanza
kufanya kitu mapema kama kujiandaa. Nitambadili Chanongo kutoka kiungo hadi
mshambuliaji, ninaamini bado anajifunza lakini baadaye atakuwa bora na
inawezekana.
SOURCE; CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment