Na Saleh Ally
MIAKA imesonga mbele, mwaka 2009 nikiwa nchini Ivory
Coast nilikutana na Aziz Alibhai, raia wa nchi hiyo mwenye asili ya Tanzania
aliyeniambia anavyotamani kufanya kazi na klabu za hapa nyumbani.
Nilitembelea katika shule yake ya soka inayojulikana
kwa jina la Ivoire Academie ambayo wachezaji kadhaa waliopita hapo akiwemo
Gervais Lombe Yao maarufu kama Gervinho wanacheza soka la kulipwa barani Ulaya.
Alibhai alizaliwa jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa
miaka ya 1950, baadaye familia yake ikahamia nchini Ivory Coast ambako ndiyo
yaliko maisha yake huku akiendelea na biashara mbalimbali.
Bilionea huyo alikuwa nchini wiki iliyopita
akiongozana na kikosi cha Ivory Coast akiwa kati ya wajumbe wa kamati ya
kuhakikisha timu hiyo inafuzu kwenda kucheza Kombe la Dunia nchini Brazil 2004.
Alibhai anamiliki magari maalum ya kutengeneza
barabara zaidi ya 50 kupitia kampuni yake ya Civil Works &Renting
Equipment. Kampuni hiyo ina malori zaidi ya 80 ambayo imekuwa ikiyatumia kwa
kazi zake pamoja na kukodisha.
Anamiliki ndege mbili binafsi, moja imekuwa
ikiendeshwa na binti yake, pia ana uwanja wake binafsi kwa ajili ya ndege hizo.
Championi Ijumaa lilifanya mahojiano kuhusiana na
Alibhai kama ana ndoto za kutaka siku moja kusaidia soka ya Tanzania, kwani
tayari ametoa msaada mkubwa kwa Ivory Coast ambako amekulia na anaendelea
kuishi.
Salehjembe: Karibu Tanzania. Je, una mpango wowote wa
kusaidia soka hapa nyumbani?
Alibhai: Bado Tanzania ni sehemu ya maisha yangu,
siwezi kuondoa kwamba nilizaliwa na kukulia hapa kabla ya kuhama. Ninatamani
sana kusaidia na nimeanza mikakati.
Salehjembe: Mikakati ipi hiyo?
Alibhai: Nimezungumza na wakala mmoja wa kuuza
wachezaji wa Fifa ambaye ni Mtanzania,
atanisaidia kuwasiliana na Klabu za Yanga, Simba na ikiwezekana Azam ambayo
nimeambiwa kuna wachezaji wa Ivory Coast wanacheza katika timu yao.
Salehjembe: Unataka akusaidie kitu gani?
Alibhai: Nimeanza na suala la kuleta wachezaji. Kama
watakuwa tayari nitawapa wachezaji, kuna kipa wangu yuko katika timu ya taifa
anaitwa Badri Ali (Sangare).
Tuko naye hapa katika kikosi cha timu ya taifa, ni
mmoja wa makipa bora, angalia yuko timu ya taifa ya Ivory Coast bado akiwa
anacheza timu ya daraja la kwanza. Niliambiwa Yanga wanahitaji kipa, tunaweza
kuzungumza.
Salehjembe: Utahitaji walipe kiasi gani kwa kipa huyo?
Alibhai: Vyote vinawezekana, kwangu fedha si kitu
kikubwa lakini nataka mafanikio ya wachezaji wangu wakati nikiwa nasaidia soka
ya Tanzania kama itawezekana. Tunaweza kukaa na Yanga, huyo wakala atazungumza
nao na kujua wana uwezo wa kufanya nini kwa mchezaji huyo na kuona nifanyeje.
Salehjembe: Vipi kuhusu Simba?
Alibhai: Simba pia au hata hao Azam FC, wanaweza pia
kuzungumza nami kupitia huyo wakala. Hapa kinachotakiwa ni suala la maelewano. Nimemueleza
wakala azungumze nao na ikiwezekana basi wafunge safari na kuja Ivory Coast
ambako wataiona timu yangu ya watoto na ile ambayo inashiriki ligi daraja la
kwanza.
Salehjembe: Iko katika nafasi gani?
Alibhai: Msimu uliopita ilikuwa bingwa daraja la pili,
msimu huu imeshika nafasi ya nne, inaundwa na vijana tu. Nilifanya hivyo ili
kuwapa uzoefu zaidi na kwa kushika nafasi hiyo nimewapa ofa ya kwenda Ghana
ambako watacheza mechi mbili za kirafiki halafu acha wale maisha kidogo, tayari
wako Ghana.
Salehjembe: Baada ya Gervinho, kuna wachezaji wengine
walitoka katika ‘akademi’ yako na kucheza Ulaya?
Alibhai: Wako wengi sana, nafikiri zaidi ya 15 na
mwaka huu wengine kama wanne au sita watakwenda UIaya. Nina mshambuliaji mmoja
anatakiwa na klabu sita za Ulaya ikiwemo ile niliyokuwa namiliki?
Salehjembe: Ulikuwa unamiliki, sasa umeachana nayo?
Alibhai: Niliiuza, wakati fulani kulikuwa na vita
Ivory Coast. Ikawa vigumu kwangu kuendelea kufuatilia maendeleo yake.
Salehjembe: Ilikugharimu kiasi gani kuiendesha?
Alibhai: Unajua ni klabu ya daraja la tatu, si klabu
kubwa sana. Pamoja na wadhamini kila mwaka nilitoa dola milioni moja (zaidi ya
Sh bilioni 1.6). Haikuwa hasara kwangu na mara nyingi sipendi kuhesabu sana
kuhusiana na fedha ingawa baadaye nitalazimika kufanya hivyo.
Salehjembe: Gervinho hutampa nafasi ya kurudi katika
shule yako?
Alibhai: Mara kadhaa, ni mtu mzuri anayekumbuka
alikotoka kiuchezaji. Wako pia wachezaji wengine ambao hurudi kusaidiana na
vijana waliopo pale.
Salehjembe: Labda elezea kidogo ukubwa wa shule yako
ya soka.
Alibhai: Kawaida tuna wachezaji 40 tu, tunawagawanya
katika makundi mawili. Wanasoka na kujiendeleza kisoka. Katika eneo ulilokuja
mwaka 2009, utaona kuna viwanja vinne vizuri kabisa, pia kuna viwili vina taa
zinazoruhusu kucheza usiku.
Tuna viwanja vya mpira wa wavu kama vile ufukweni.
Kuna vyumba vya kulala wachezaji pamoja sebule kubwa. Gym maalum, sehemu ya
kupumzikia, sehemu ya chakula na madarasa mawili kwa ajili ya kujifunza mambo
kadhaa, lakini kuna basi maalum kwa ajili ya kuwapeleka shuleni.
Salehjembe: Kwa hiyo soka ndiyo biashara yako?
Alibhai: Hapana, ingekuwa ndiyo biashara yangu
nisingekuwa hapa. Nafanya biashara mbalimbali, tena ni nyingi sana ndiyo maana
unaona naweza kumiliki ndege mbili na sehemu kubwa kama ile. Soka kwangu ni
kama kitu kinachofurahisha moyo wangu, napenda kusaidia vijana wakue, napenda
kuona wanacheza ndiyo maana naendelea kufanya hivi.
Salehjembe: Una eneo kubwa sana, kuna mipango zaidi ya
hapo?
Alibhai: Ndiyo, nataka kujenga hoteli maana timu
nyingi zimekuwa zikitaka kuweka kambi eneo hilo. Wameliona limetumia na kila
kitu kwa ajili ya mazoezi kipo, lakini hakuna nafasi ya kuishi pale, hivyo
nitajenga hoteli ya kisasa ili ikiwezekana timu ziwe zinaweka kambi pale.
Nakumbuka hata Kenya, walitaka kuleta timu yao ya
taifa ije iweke kambi kabla ya kucheza na Nigeria, lakini tatizo ni sehemu ya
kulala kwa wachezaji wenye hadhi ya timu ya taifa.
Salehjembe: Ukimaliza ujenzi ninaamini siku moja Taifa
Stars itapata nafasi ya kuweka kambi?
Alibhai: Kweli, kama watapangiwa kucheza na nchi za
Magharibi. Hata wakati wanakwenda kucheza na Gambia, tunaweza kuwasiliana na
nikaona kama naweza kusaidia katika gharama za muda za kuweka kambi wakakaa
kidogo pale Abidjan.
Salehjembe: Unatarajia kurudi tena Tanzania?
Alibhai: Ndiyo, nafikiri nitarejea na mke wangu niende
Zanzibar kwa mapumziko, pia niweze kuwajua watu zaidi hapa.
Salehjembe: Ulitembea kidogo Dar es Salaam?
Alibhai: Ndiyo nilifika hadi Upanga nilipokuwa ninaishi,
lakini nilienda hadi pale Karume uwanjani (Ofisi za TFF), maana enzi zile ndiyo
ulikuwa uwanja mkubwa wa Dar es Salaam ambao tulikuwa tukienda kuangalia mechi
za soka.
0 COMMENTS:
Post a Comment