Kufungwa kwa Taifa Stars mabao 4-2 dhidi ya Ivory Coast
ndiyo gumzo kubwa kwa takribani wiki moja sasa. Wako Watanzania wapenda soka
wameshindwa kuzuia hasira zao baada ya kipigo hicho.
Walioshindwa kuzuia hasira zao
wanaonyesha ni mapenzi tu na taifa lao, kwa kuwa walitaka kuona Taifa Stars
inawapa adhabu Tembo hao wa Ivory Coast kama ilivyokuwa kwa Morocco.
Lakini mambo yakaenda tofauti, kwangu
naona hakuna ubishi kwamba Taifa Stars walijitahidi kadiri ya uwezo wao lakini
mambo yahakawa magumu. Hivyo hakuna sababu ya kumshambulia mchezaji mmoja, wote
au zaidi.
Kama kuna mchezaji anaonekana alikosea,
basi inawezekana aliwahi kuwa msaada mkubwa katika mechi kadhaa zilizopita. Hivyo
lazima tukubali, binadamu hufanya mambo yake tofauti kulingana na siku, tuwape
nafasi nyingine, kwani hatuwezi kuwajenga kwa kuwalaumu tu.
Iwapo itaonekana kuna mtu kapewa nafasi
za kutosha, lakini akashindwa kuzitumia kwenda kwenye mabadiliko, basi ujue
hapo kuna tatizo na adhabu inaweza kutolewa.
Kingine ambacho ndiyo Hoja Yangu leo, ni
kwetu kutafakari kuhusiana na suala la uwezo wa wachezaji wa Ivory Coast hasa
wale waliokuwa katika kikosi cha timu ya taifa kilichopambana na Stars.
Tuna mfano mzuri ambao unaweza
kutufungua macho, Kipre Tchetche wa Azam FC ndiye kipoko wa makipa, mabeki na
washambuliaji wote walioshiriki Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
Tchetche ambaye ni raia wa Ivory Coast amekuwa
mfungaji bora msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, ndiyo maana nimesema ni kiboko
wa washambuliaji wote. Lakini kumbuka amewafunga makipa kibao na amewapita
mabeki lukuki kwenda kufunga ndiyo maana nimesema ni kiboko yao pia.
Mshambuliaji huyo kutoka Ivory Coast
hana hata nafasi ya kukaa benchi katika kikosi cha timu ya taifa ambayo ilikuwa
hapa Tanzania kuivaa Taifa Stars.
Ninachoonyesha hapa ni hivi, Tchetche
ndiye bora na hatari zaidi anayewasumbua mabeki na makipa wa hapa, lakini hana
nafasi katika kikosi cha Ivory Coast, hata kukaa benchi. Maana yake, wachezaji
waliopambana na wa kwetu walikuwa na kiwango cha juu zaidi.
Hii maana yake, kikosi hicho si Yaya
Toure, Salmon Kalou na Gervinho pekee, badala yake wachezaji walio ndani yake
ni bora zaidi ya Stars kutokana na mazingira kama vile makuzi sahihi kisoka.
Ndiyo maana hata anayeonekana bora
katika ligi yetu, hana nafasi hata ya kulikalia benchi lao. Maana yake vijana
wa Stars walifanya kazi kubwa nay a ziada kupambana na Ivory Coast.
Hakuna ubishi kuna makosa yalifanyika
ambayo yalisababisha adhabu hiyo ya mabao kwa Stars. Ni jambo zuri kujifunza
kwa kuwa Stars ilikuwa inapambana na timu namba moja kwa ubora Afrika ambayo
ingeipa hofu hata Misri, Nigeria, Cameroon au timu nyingine kama ingekutana
nayo.
Utaona mechi ilivyokuwa katika uchezaji,
kwamba walikuwa wakipambana karibu sawa kwa kila kitu. Lakini Ivory Coast
walikuwa wazuri kuyatumia makosa ya Stars na kuwamaliza.
Angalia faulo walizopiga, zilikuwa mbili
wakafunga moja kupitia Yaya. Wakati Stars walipata nne na hawakufunga hata
moja, hata kama walizipiga vizuri. Hivyo kuna mambo mengi ya msingi ya
kujifunza.
Stars inatakiwa kupambana na kucheza
michuano ya Chan itakayofanyika nchini Afrika Kusini. Hivyo hakuna haja ya
kuendelea kuwashambulia wachezaji au kujadili nani alikosea kwa muda mrefu.
Ili kuvuka Chan, lazima Stars iing’oe
Uganda ambayo kwa viwango vya Fifa inatuzidi, lakini kisoka uwanjani
inawezekana na tunaweza kwenda Chan ingawa kinachotakiwa sasa ni kitumia makosa
ya Ivory Coast kujiboresha na kufanya vizuri.
Bado tuna nafasi ya kujirekebisha na
kufanya vizuri zaidi kutokana na mwenendo wa kikosi chetu kiuchezaji. Kikubwa
Kocha Kim Poulsen na benchi lake la ufundi wayafanyie kazi makosa hayo na
ikiwezekana kama kuna mchezaji wa kuongezwa ifanyike hivyo mara moja.
Lakini kwa mashabiki na wadau, pia
tuangalie kipi ni msaada zaidi kwa timu yetu katika kipindi hiki. Kama
tunahitaji kulaumu na tunaona ndicho kitu kinachoridhisha nyoyo zetu, basi
tusubiri kwanza. Lakini sasa tusaidie kukosoa kwa ajili ya kurekebisha bila ya
kuvunja moyo ili timu yetu ifanye mazuri zaidi.
0 COMMENTS:
Post a Comment