Na Saleh Ally
Tayari
mshambuliaji Nonda Christophe Nonda ameamua kustaafu soka, sasa anaendelea na
maisha mengine, mfano suala la uhamasishaji wa amani katika sehemu mbalimbali
duniani.
Yanga ambayo
ndiyo chachu ya Nonda kuanza kupata mafanikio, imekuwa ikiumia na majeraha
makubwa ambayo dawa yake ingekuwa mshambuliaji huyo kama kila kitu kingekwenda
kwa mpangilio.
Viongozi wa
soka nchini ni watu wanaojali maslahi yao binafsi hata kuliko soka ya Tanzania
ndiyo maana imedumaa, wako wanaowatetea lakini ni vigumu sana kukwepa ukweli,
kwa kuwa mifano ni mingi na hili la Nonda ni sehemu tu.
Ukiangalia
katika rekodi za Nonda kimataifa, zinakuonyesha mshambuliaji huyo alianzia Vaal
Professional ya Afrika Kusini, wazungu hawajui lolote kwa kuwa Yanga walifanya
madudu makubwa wakati wa kumuuza.
Sheria za
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) zinataka mchezaji anapouzwa, basi lazima
kuwe na faida kwa klabu inayomuuza katika misingi ya asilimia.
Nonda alikuwa
na uwezo wa kuiingizia Yanga zaidi ya milioni 500 katika kipindi ambacho
alikuwa anauzwa kutoka klabu moja kwenda nyingine, lakini ikawa vigumu kwa kuwa
uongozi wa Jangwani kipindi hicho chini ya George Mpondela haukuwa umejali
hilo.
Viongozi
waliokuwa madarakani waliangalia maslahi yao kipindi hicho na taarifa
zinaelezwa Nonda aliuzwa kwa dola 10,000 tu na viongozi wakachanganyikiwa.
Kikubwa mkataba ulisema vipi kama Nonda angeuzwa klabu nyingine.
Inaonyesha
viongozi waliangalia fedha hizo siku wanakabidhiwa, hawakuona umuhimu wa
kuingia mkataba wa uhakika ambao ungeisaidia Yanga kuendelea kuigiza fedha kwa
miaka mingine 15 au zaidi baada ya hapo.
Angalia hapa
namna uhamisho wa Nonda ulivyokuwa na huenda Yanga ingepata kiasi gani kwa kuwa
mara nyingi klabu kama Yanga ingekuwa inapata asilimia 10 kila anapojiunga na
klabu nyingine.
Mwaka 1995
ndiyo alijiunga na Vaal Professional baada ya kumuona akiichezea Yanga, tena
aliingia kwa kuwa namba yake ilikuwa inathibitiwa na Mohammed Hussein Daima
maarufu kama Chinga One.
Vaal ilimpata
kwa dola 10,000 tu, yenyewe ikamuuza kwa dola 150,000 kwa klabu ya FC Zürich ya
Switzerland, hiyo ilikuwa ni mwaka 1996, hapa Yanga ingepata dola 15,000,
lakini ikaambulia patupu.
Nonda
aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Switzerland, soko lake likapanda na mwaka
1998 akauzwa Rennes kwa kitita cha dola milioni 9, Yanga ilitakiwa kupata dola
900,000. Na miaka miwili baadaye Nonda akajiunga na AS Monaco kwa uhamisho
uliovunja rekodi wa dola milioni 25 million, Yanga ilitakiwa kupata dola
250,000.
Bado Nonda
aliendelea kuhama kwenda AS Roma, Blackburn kwa mkopo na mwisho Galatasaray ya
Uturuki, nafasi anayocheza leo Didier Drogba.
Hii
inaonyesha kuwa Yanga ilipoteza zaidi ya Sh milioni 500 katika kipindi hicho
kutokana na uzembe wa uongozi wake kipindi hicho kwa kuwa uliona dola 10,000
ilikuwa ni kama fedha zilizohifadhiwa na
benki zote duniani.
Yanga imebaki
inajisifia kitu kimoja tu, kwamba Nonda aliwahi kupita hapo, kitu ambacho
hakina faida yoyote zaidi ya kuonekana hakuna lolote.
Hapa kuna masomo
mawili kwa Yanga na timu nyingine ambazo zinaweza kupata nafasi ya kuwauza
wachezaji wake Ulaya au kwingineko ambako soka limepiga hatua.
Kwanza
kung’amua mapema kwamba umuhimu na upana wa biashara kwa kuwa katika nchi
zilizopiga hatua wanalijua hilo na wanakuwa wajanja sana kuwamaliza viongozi
waliozubaa kama walivyokuwa wa Yanga kipindi hicho kwa kuwa walichanganywa na
dola 10,000.
Katika hilo,
bado viongozi wajifunze kuingia mikataba iwe ni ya mauzo au kazi ambayo inaweza
kuwa na msaada mkubwa kwa klabu na si wao binafsi. Kama wanakuwa hawaelewi,
vizuri wapateushauri kutoka kwa wataalamu na si kujiona wanajua sana, kumbe
hamna kitu.
Somo la pili
ni kuhusiana na Nonda mwenyewe, kabla ya kuja Yanga aliichezea Atletico ya
Burundi, hakuwa tegemeo na muda mwingi aliutumia kufanya kipindi cha DJ Show
katika redio moja mjini Bujumbura.
Baada ya
kutua Yanga hakuwa staa pia, zaidi alicheza katika timu ya pili kabla ya
wachezaji wengi nyota kama akina Edibily Lunyamila kuondoka, yeye na wenzake
kama Anuar Awadhi, Maalim Saleh ‘Romario’ kutoka kikosi B wakapandishwa na kuwa
timu kubwa.
Siku chache
baadaye akauzwa Afrika Kusini na inaonekana hivi, kama viongozi Yanga
hawakufanya ‘usamjo’ na kuchukua fedha zile kwa faida yao, basi walidharau na
kuona kama Nonda kawapa faida kubwa na hakuwa na lolote.
Kama ni hivyo
walitakiwa kujiuliza kwa nini timu kutoka katika ligi iliyoendelea kuliko Yanga
inamhitaji? Halafu wangepata jibu na kunusa faida mbele yao na mwisho
wangeingia mikataba yenye faida.
Vaal
wasingekubali kufanya kosa kama la Yanga, lazima watakuwa wamefaidika vilivyo
kutokana na mchezaji huyo, huku Yanga wakibaki na sifa tu, eti “alipita hapa”.
Halafu?
SOURCE;
CHAMPIONI
bado naamini, ska letu linaongozwa na watu dhaifu , dhaifu , dhaifu.
ReplyDeleteMakosa aliyoyafanya Mpondela katika usajili wa Nonda hadi kuikosesha Yanga mamilioni hadi leo huwenda yanaweza kujirudia.
na kwa wachezaji wetu, Nonda lazima awe somo kuwa Kipaji ni kichochocheo tu, lakini nidhamu na maadili ya soka ni kila kitu.
wako wapi kina Mohamed Hussein Machinga na Edibily Lunyamila ? walimzidi kipaji tena kwa mbali, lakini Nonda aliwazidi ujanja na akili ya soka.