June 12, 2013

Kaka wa Amri Kiemba ambaye pia ni wakala wake, Ulimwengu Hamimu (aliyekaa) baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kwa niaba ya Kiemba jana katika  hoteli ya Tansoma Kariakoo jijini Dar.
Ulimwengu akiwa na milioni 35 baada ya kusaini mkataba kwa niaba ya mdogo wake.
...Akihesabu mkwanja.
...Sehemu ya mkataba huo.

Amri Kiemba akiwa na aliyekuwa kocha wa Simba, Patrick Liewig.

Khatimu Naheka na Wilbert Molandi

KAMA ni umafia basi huu uliofanywa na Simba ni kiboko.
Simba jana iliifanyia Yanga umafia wa kiwango cha hali ya juu na kufanikiwa kumnasa kiungo wao aliyekuwa amemaliza mkataba, Amri Kiemba na kumpa mkataba mpya.
 
Kiemba ambaye msimu uliopita alifanikiwa kuonyesha kiwango cha hali ya juu, jana alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia timu hiyo ya Msimbazi.
Yanga Jumapili walimweka mtu kati kaka wa Kiemba ambaye ndiye meneja wake, Hamim Ulimwengu na kukubaliana kumpa kiungo huyo kitita cha shilingi milioni 35 na mshahara wa shilingi milioni 3.2, kilichokuwa kikisubiriwa ni staa huyo kufika kutoka Morocco na kusaini, lakini jana Simba waliwapiga bao.

Viongozi wa Simba na Yanga walikesha kwenye kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars, iliyopo kwenye Hoteli ya Tansoma, Kariakoo jijini Dar es Salaam, huku kila mmoja akitaka kumwahi kiungo huyo mkongwe.
Hata hivyo, pamoja na timu zote mbili kuhaha huku timu moja ikipanga chumba hotelini hapo, bado zilishindwa kuonana na kiungo huyo kwa kuwa uongozi wa Stars ulimwekea ulinzi mkali.
Asubuhi viongozi hao waligongana tena nje ya kambi ya timu ya taifa, huku kila mmoja akijifanya kuwa amekwenda pale kwa shughuli nyingine, lakini wakichungana kwa umakini mkubwa.
Yanga walizidiwa nguvu na kuwaacha Simba ambao waliendelea kufuatilia nyendo za kiungo huyo, huku wakiwasiliana na Ulimwengu kwa umakini mkubwa.
Timu zote mbili ziliwatumia wachezaji wao waliopo kwenye kambi hiyo kufanya uchunguzi juu ya nini kinaendelea na simu zilitumika sahihi kupeleka habari.
Hofu iliwatanda viongozi wa Simba majira ya saa nane mchana, baada ya kupata taarifa kuwa Ulimwengu ameonekana jirani na ofisi ya kiongozi mmoja wa Yanga, Posta jijini Dar es Salaam.
Hali hiyo iliwafanya wawe macho kuchunga geti la timu ya taifa ili mtu yeyote asiingie kufanya umafia au Kiemba asitoke nje.
Hata hivyo, dakika 45 baadaye walipata furaha baada ya kumuona Ulimwengu akiwasili nje ya hoteli hiyo akiwa kwenye usafiri wa pikipiki, lakini hakuruhusiwa kuingia ndani.
“Kiemba hayupo kambini, ametoka kidogo lakini hajakwenda mbali na hapa lakini wewe huruhusiwi kuingia ndani,” alisema mfanyakazi mmoja wa hoteli hiyo.
Hata hivyo, kauli hiyo ilizidi kuwatisha Simba, lakini Ulimwengu aliwatoa hofu kuwa hakuna chochote ambacho kimefanyika.
Dakika kumi baadaye, Kiemba alionekana kwa mbali na ndipo viongozi wa Simba, Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’, wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji, Said Pamba na Danny Manembe walipomsogelea Ulimwengu na kuzungumza naye.
Baada ya mazungumzo walimpa mkataba huo ambao ulipelekwa kwa Kiemba akiwa amesimama na kuusaini, baadaye akaingia ndani ya kambi.
Hata hivyo, Ulimwengu aliwataka viongozi wa Simba kumpa fedha zote bila kubaki hata shilingi ambapo viongozi hao walimuomba meneja huyo waende katika ofisi moja iliyopo katika hoteli hiyo ili kuweza kufanya makabidhiano, kwani huko ndiko Wekundu hao walikuwa wameziweka fedha hizo.
Hii ina maana kuwa Kiemba ataitumikia Simba kwa kipindi cha miaka mingine miwili na kuwapiga bao Yanga waliokuwa wakihitaji saini yao, sasa fedha walizobaki nazo wanaweza kumsajili, Moses Oloya ambaye wanamwinda kwa nguvu kubwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic