July 1, 2013


SEHEMU YA PILI NA YA MWISHO....
Na Saleh Ally
Ukisia jina la Mohammed Bin Slum, moja kwa moja utaelekeza mawazo yako katika mambo mawili, soka na biashara ya matairi ya magari.
Bin Slum ni mfanyabiashara maarufu zaidi katika biashara ya matairi na betri za magari. Lakini ndiye mdhamini mkuu wa klabu ya Coastal Union ya Tanga.

Pamoja na kuwa mdhamini, Bin Slum ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal Union maarufu kama Wagosi wa Kaya.

Mwendo wa timu hiyo kwa misimu miwili pamoja na usajili wa msimu ujao, unaifanya Coastal Union kurudisha heshima na umaarufu wake wa miaka ya 1980 na kuingia kwenye mbio za moja ya timu zinazoweza kuwa bingwa
.
Katika mahojiano maalum na Championi Jumatatu, Bin Slum ambaye alizaliwa na kukulia mkoani Tanga kabla ya kuhamia jijini Dar es Salaam mwaka 1994 baada ya kumaliza kidato cha sita, anazungumzia masuala kadhaa kuhusiana naye lakini pia Coastal Union.


Bin Slum ambaye amewahi kuwa mchezaji wa timu ya NBC Tanga na timu ya mkoa huo ya Tanga Stars ambayo ilikuwa inaundwa na wachezaji wengi kutoka Coastal Union na African Sports ‘Wana Kimanumanu’, anaamini Coastal itafanya vizuri zaidi msimu huu.  

Salehjembe: Mmewachukua Boban na Nyosso,  Simba wamewaondoa kwa sababu ya nidhamu…
 Bin Slum:  Nawajua vizuri sana Boban na Nyosso, ni watu ambao tunaishi karibu na tunashirikiana katika mambo mengi ya mpira. Sitaki tufanye kitu kwa kuamini wengine, huenda kuna viongozi au kiongozi wa Simba alikuwa na matatizo nao binafsi, kayaingiza hadi kazini.


Salehjembe: Hivyo mmeamua kujaribu kama moto unaunguza?
Bin Slum: (kicheko), hatuna maana hiyo. Huenda Simba hawakuwapa second chance (nafasi nyingine) ili waone kama watajirekebisha. Utaona tumewapa mkataba wa mwaka mmoja kila mmoja. Hapo tuna nafasi ya kuangalia na kuhakikisha ingawa mimi ninaamini watacheza.

Salehjembe: Coastal Union inaonekana ni kati ya Big Four za Ligi Kuu Bara? Vipi hauna hofu ya kuingia kwenye football fitna na hujuma?
Bin Slum: Najua una maanisha kuonewa labda kwa kuwa tunatokea mikoani, mimi siamini kama TFF au kuna mtu anaweza kufanya hivyo.
Huenda Simba na Yanga zinaweza kuvuta kutokana na maslahi, lakini tunajiamini na tutakachofanya ni maandalizi ya kutosha.

Salehjembe: Labda wapi mnapanga kufanya maandalizi, mtaweka kambi Tanga au nje ya Tanzania?
Bin Slum: Ninaamini tutakwenda nje ya Tanzania. Ni suala tunalolifanyia kazi, kama kila kitu kikikamilika, basi tutao taarifa.

Salehjembe: Simba ndugu yao Coastal Union, wewe pia ni shabiki wa Simba?
Bin Slum: Nimelipenda hili swali, unajua kasumba iliyopo ni kila Mtanzania lazima awe Yanga au Simba, si kweli. Mimi si shabiki wa timu yoyote kati ya hizo mbili, tokea nimezaliwa ni Coastal Union.

Salehjembe: Inaonekana ni vigumu kwa Watanzania wengi, wewe umeweza vipi?
Bin Slum: Baba yangu alinishika mkono tokea nikiwa mdogo kwetu Tanga kwenda uwanjani kuiona Coastal Union. Zamani mikoani, watu walikuwa mashabiki wa timu zao na Yanga au Simba, ndiyo maana zilipata tabu zilipoenda mikoani maana watu walishangilia timu zao. Nafikiri hata sasa ifikie iwe hivyo.

Salehjembe: Mara ngapi umeona mechi za Simba na Yanga zilizokuvutia?
Bin Slum: Hata mara moja, sijawahi kwenda uwanjani kuziona Yanga na Simba zikipambana, imewahi kutokea hivyo mara mbili na niliona mechi kwenye runinga. Sioni sababu ya kwenda uwanjani kwa kuwa hizo si timu zangu, bora niende nikaione Coastal inacheza mechi ya kirafiki.

Salehjembe: Maana yake zikicheza Yanga au Simba hata na timu nyingine hauendi uwanjani?
Bin Slum: Hapana, nimewahi kuziona zikicheza lakini mara nyingi kama zinacheza na timu nyingine, mfano Yanga na JKT Ruvu au zinapokuja kucheza na Coastal Union.

Salehjembe: Nini kinakuvutia zaidi kwa Yanga na Simba na unaamini mkijifunza au kukipata basi mtapiga hatua?
Bin Slum: Sidhani kama wana kitu kizuri kama idadi kubwa ya mashabiki, natamani ingekuwa ni ya Coastan Union. Kwetu ingekuwa biashara kubwa, angalia wao hata biashara ya jezi tu hawafanyi kwa kuwa hawana jezi inayotambulika ni ya Yanga au Simba. Coastal Union tuna jezi inatambulika kokote, wao hawana na wamewaachia wajanja wachache wanajiingizia mamilioni. Ndiyo maana unaweza kusema Simba na Yanga wana rangi tu.

Salehjembe: Kwa miaka yote uliyoishi nini Dar es Salaam, vipi Yanga au Simba hawajawahi kukuomba kusaidia?
Bin Slum: Kweli wamenifuata mara nyingi sana kujaribu kunishawishi niingie na kusaidia klabu hizo. Lakini nimekataa, mimi ni Coastal Union na ninahitaji kuisaidia ili irejee katika hadhi yake. Najua wao ni timu kubwa, lakini tutapambana.
SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic