*Aeleza
matatizo mambo yalivyokuwa, siku alipozinduka, namna P Funk alivyompa dili feki
la Sh milioni 200
*Sasa
aandaa albamu, inamhusu Mangwea, apanga kujichora tatu ya marehemu
Na Saleh Ally
Msanii wa
muziki wa kizazi kipya, Mgaza Pembe maarufu kama M To The P, alizushiwa kifo
siku moja baada ya rafiki yake kipenzi Albert Mangweha ‘Mangwea’ au ‘Ngwea’
kufariki dunia jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Ngwea
alikutwa chumbani akiwa na M To The P, wote wakiwa hawajitambui na
walipokimbizwa hospitali, Ngwea aliaga dunia na yeye akalazwa katika chumba cha
wagonjwa mahututi (ICU). Baada ya hapo mengi yalitokea.
M To The P
amepita katika mengi hadi alivyorejea nyumbani salama na sasa yuko katika hatua
za mwisho za maandalizi ya albamu yake mpya. Lakini hapa katika mahojiano exclusive
na Championi Ijumaa, anaelezea mengi yaliyotokea kuanzia siku ya tukio hadi
alivyorejea jijini Dar es Salaam na baadaye kwenda Morogoro kushiriki mazishi
ya rafiki yake kipenzi.
Siku ya
tukio:
Siku hiyo
nakumbuka tulikuwa na washkaji, tuliungana pamoja na kwenda kusherekea. Unajua
kabla ya hapo tulichelewa ndege baada ya kupitiwa na usingizi. Hivyo safari
hiyo hatukutaka kurudia kosa tena, kwa kuwa ndege ilikuwa ni Saa 12:30 asubuhi,
tulikubaliana tusilale.
Tulilazimika
kutolala kuepuka kuchelewa ndege, maana baada ya kuchelewa ndege ya kwanza, ili
tiketi yetu iendelee kuwa hai na kuitumia wakati mwingine tulilazimika kulipa
rand 1200 (Sh milioni 1.7), hatukutaka kuingia tena gharama kwa uzembe.
Hivyo
tukaondoka kwenda kujiachia (kusherekea) na washkaji na lengo likiwa ni kuhakikisha
hatulali, baadaye tulienda klabu na baada ya kuona muda unakaribia, nakumbuka
ilikuwa Saa 10 usiku, tukaamua kurudi nyumbani kuchukua mizigo yetu kwa ajili
ya safari.
Hakika huko
ndiyo matatizo yalianzia, kweli nikikumbuka roho inaniuma sana na kuna mambo
mengi hadi leo yananiumiza sana. Ila nakuhakikishia hivi vitu kuanzia hapo
siwezi kuvizungumzia kwenye vyombo vya habari hasa kwa wakati huu. Subiri muda
ukifika, lazima tujue mchini (Ngwea) ana mzazi wake, pia familia. Hivyo
tuwaonee huruma pia kuwa watajisikiaje.
Nilipozinduka:
Kuhusu
kuzinduka kwangu naweza kuelezea, baada tu ya kupata fahamu nilianza kumuulizia
mchini wangu, nikaambiwa alikuwa ametangulia Dar. Kidogo nikashangaa, vipi
aliniacha wakati tulitakiwa kuondoka wote!
Yule
daktari mzungu alinisisitizakuwa natakiwa kupumzika, sikujua nilikaa hapo siku
ngapi, lakini baadaye nilielezwa kuwa nilikaa siku mbili, nikauliza vitu vyangu
ikiwemo mizigo ilikuwa imepotea pia.
Baada ya
siku mbili nilitolewa wodi ya watu mahututi (ICU), nikapelekwa ya kawaida
ambako pia nilitoka baada ya siku kadhaa nakumbuka Jumatatu kamaa saa moja
usiku ndiyo niliruhusiwa na kibali cha kuruhusu mwili wa Ngwea kikatoka siku
hiyo saa 4:30 usiku.
Nafikiri
walisubiri kuniona niko fresh ndiyo watoe kibali, lakini muda wote huo mimi
sikujua kitu chochote kwa kweli kuhusiana na msiba.
Kuchungwa:
Nilichukuliwa
na kupelekwa kwa mshkaji mmoja, nilikaa huko na nilianza kushangazwa kila
nilipokuwa napigiwa aliiwahi simu yangu na kuichukua halafu yeye ndiyo
alizungumza na huyo mtu. Nilishangaa kwa kuwa haikuwa kawaida, nikadhani huenda
kwa kuwa ni mgonjwa hakutaka nizungumze sana, sikujali sana.
Dili la Sh
200m:
Siku hiyo
hiyo, P Funky alinipigia simu, akanieleza kuwa kuna dili la kurekodi muvi,
limefikia hadi Sh milioni 200 na nilikuwa natakiwa mimi kwa kuwa nilianza
kuifanyia mazoezi halafu baadaye wenyewe wakaahirisha. Nakumbuka hiyo muvi
ilikuwa imepewa jina la Sarkana.
Nilishangazwa
na wingi wa fedha, lakini niliona inawezekana maana muvi ni nzuri. Wakanikatia
tiketi ya Jumanne, lakini baadaye ikabadilishwa, hata sikujua sababu. Kumbe
siku hiyo ndiyo mwili wa Ngwea ulikuwa unasafirishwa tena na ndege ambayo
nikapanda.
Wakanikatia
ndege ya South African ambayo walijua wanapanda wazungu wengi, huenda ingekuwa
vigumu kukutana na mtu ambaye angenipa pole na kufanya nijue tatizo. Nilipofika
Dar es Salaam, gari nne zilikuja kunipokea, nilikuwa kama mheshimiwa au mtu
fulani tajiri, waliniingiza katika moja ya gari na tukaondoka haraka kwa kasi.
Kidogo
ilinishangaza, P Funk aliendelea kusisitiza kwamba sikutakiwa kuonekana
kutokana na ile ishu ya muvi. Siku hiyo Dar kulikuwa na foleni sana, ingawa nilitua
moja na nusu hivi, tulifika Mikocheni Saa tano usiku na huko ndiyo nilifichwa.
Baada ya
kufika walifanya kama tunafanya mkutano fulani hivi kuhusiana na ile muvi na
mimi nikaamini dili lilikuwa limeiva. Lakini ilipofika saa nane usiku ndiyo
wakaniambia ukweli kwamba kulikuwa na tatizo kubwa na mchini wangu (Ngwea)
alifariki dunia. Kwangu ilikuwa ni vigumu kuamini tu kwa maneno.
Mwili
kwenye Ipad:
Kwa mara ya
kwanza kuhakikisha kuwa ni kweli niliona kwenye picha kweli mchizi (Ngwea)
alikuwa amefariki, picha za video kwenye Ipad, zilifanya nithibitishe. Pale
ndiyo walinionyesha watu walivyokuwa wanaanga siku hiyo, sikuamini,
nikachanganyikiwa na kuanza kulia sana.
Walinitaka
kujikaza kwa kuwa kesho yake alfajiri nilitakiwa kuanza safari ya kwenda
Morogoro kwenye mazishi. Nilijitahidi lakini ilikuwa vigumu sana kwangu,
sikuacha kulia hadi siku iliyofuata. Kweli siku hiyo alfajiri tukasafiri kwenda
Morogoro kwa ajili ya kuuaga mwili wa Ngwea pamoja na mazishi.
Kweli
nisingependa kuelezea zaidi kuhusiana na Mangwea, natakiwa kukutana na familia,
hasa Bi Mkubwa wake (mama), ili nimuelezee kila kitu. Sasa siwezi kuendelea
zaidi hadi hapo nitakapomueleza. Hivyo vizuri tukaishia hapa.
Jina M To
The P:
Maana ya
jina hili ni Mgaza wa Pembe, ndiyo maana M, yaani Mgaza to the, nikimaanisha wa
P, Pembe. Najua kunakuwa na ugumu kidogo lakini ndiyo nililiweka hivyo kisanii.
Muziki:
Nilikuwa
karibu sana na Mangwea, lakini mimi pia ni msanii wa siku nyingi. Sasa
ninachofanya nimeamua kurudi kwa nguvu kubwa na niko ‘siriaz’ sana. Tayari
singo ya kwanza imekamilika inaitwa Masambe Wena, yaani twende zetu kwa lugha
ya Kizulu ambayo asili yake Afrika Kusini.
Ndani yake
nimewashirikisha Chegge na Country Boy. Maana yake kuna kwaito na hip hop.
Singo hiyo itaanza kusikika kwa mara ya kwanza Jumatano (juzi). Humu pia
nimetua baadhi ya sauti za Ngwea.
Songi
linalofuata:
Singo
inayofuata itakuwa ni Mungu Ndiyo Anapanga, humu ndani nimemshirikisha Diamond
na Jay Mo, tena hautachelewa kuingia katika redio mbalimbali baada ya Masambe
Wena. Ninafanya hivyo kwa kuwa nataka mambo yaende haraka pia katika mpangilio
mzuri.
Ndani ya
singo hii, kuna baadhi ya mambo yaliyotukuta na Mangwea nayaelezea na wenye
hamu ya kusikia huenda angalau wakakata kiu chao.
Albamu:
Tayari
nyimbo nne zimeishakamilika katika albamu yangu zikiwemo hizo za Masambe Wena
na Mungu Ndiyo Anapanga. Lakini lengo ni kufanya albamu yenye nguvu ambayo
itakidhi kiu ya mashabiki kutokana na ushindani sokoni.
Albamu
itatoka haraka iwezekanavyo na kwa kushirikiana na P Funk na watalaamu wengine,
tumekuwa tukifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mambo yanakwenda.
Taasisi:
Hii Mangwea
foundation itakuwa inafanya mambo kadhaa ya kuendeleza muziki. Lakini zaidi
inalenda suala la kuangalia alichokuwa amekianzisha Mangwea wakati akiwa hai.
Mfano kuna
nyimbo zake nyingi sana zilizo katika studio mbalimbali, tutazikusanya na
kutengeneza albamu kali ambayo mapato yataingia katika foundation. Lakini bado
watu watapewa nafasi ya kutumia baadhi ya sauti zake katika nyimbo zao. Kwa
kweli kuna mambo mengi sana ambayo yatafanyika kwa ajili ya kusaidia jamii.
Denja Vu:
Hawa ni
vijana waliokuwa chini ya Mangwea, wana vipaji na nisingependa vipaji vyao
vife. Hivyo nitashirikiana na wadau wengine akiwemo P Funky kuhakikisha
tunawaendeleza. Mmoja tayari nimempa nafasi katika singo ya Masambe Wane na
amefanya vizuri.
Lengo hapa
ni kusaidia vipaji vingine lakini pia kuonyesha tunakubali kile kilichoanzishwa
na Ngwea kuwa aliona ni kitu cha msingi na tunakiunga mkono:
Tatoo ya
Mangwea:
Najiandaa
kuchora tatuu kubwa mgongoni ambayo itakuwa na picha ya Mangwea, nitafanya hivi
kuonyesha upendo wangu kwake na hii si mara ya kwanza.
Nilianza kuchora
tatuu ya machozi baada ya kufiwa na mama yangu mzazi, hii ilikuwa ni kuonyesha
mapenzi yangu kwake. Lakini nina tatuu nyingine ya gitaa, hii ni kuonyesha
mapenzi yangu katika muziki ambao uko katika damu yangu.
Maana yake
tatuu ya Ngwea itakuwa ni ya tatu kwangu na mambo yote utaona ni mapenzi ya
dhati na ninaamini hii itatuu ya Mangwea itakuwa ni gharama kubwa.








Asizingue, anajua kilichotokea ndo mana anataka kwanza aongee na Mama Ngwea halafu kila mara anasema kuna mengi yametokea, halafu wale Madaktari si Waganga wa kienyeji kumponya bila kujua tatizo...kwani walipiga ramli??
ReplyDelete