Lawama za
kwamba wachezaji wamekuwa ni watovu wa nidhamu zimekuwa zikisambaa kila kukicha
na kuna mambo mengi sana ya kuthibitisha kwamba kuna wachezaji Fulani wamekuwa
wakihusika na vitendo hivyo.
Hakuna
ubishi, wachezaji lukuki tumesikia wamekamatwa wakifanya vitendo vya utovu wa
nidhamu na klabu zao zao zikaamua kuchukua hatua zinazostahili kwa ajili ya
kuwadhibiti.
Ingawa
mashabiki wamekuwa wakilalama, bado viongozi wana haki ya kuchukua hatua kwa
kuwa kama watatoa nafasi ya vitendo vya nidhamu kuendelea kwa ajili ya
kuwafurahisha mashabiki basi watakwama na siku ya mwisho lawama zitaangukia
kwao.
Hivyo ni
suala la msingi sana kwa viongozi kusimamia suala la nidhamu bila ya hofu ya
kitu chochote kwa kuwa tunajua wazi kwamba bila ya nidhamu, basi hakuna
mafanikio hata kama timu itakuwa na vipaji vya hali ya juu, bila ya nidhamu,
hakuna mafanikio.
Pamoja na
yote hayo, bado nataka kusisitiza pia kuhusiana na viongozi wanaokuwa katika timu
ambao wanakuwa na tabia ya kujenga chuki kama inatokea wakakosa na wachezaji.
Mara kadhaa
tumekuwa tukisikia na wachezaji nao wakilalama kwamba kuondoka kwao katika timu
fulani kunahusiana na chuki kati yao na viongozi kadhaa wa timu wanayoondoka.
Lakini kama
wadau suala hilo tumekuwa tukilichukulia la kawaida tu, hakuna ambaye anataka
kuhoji na kujua kama kweli viongozi wanaweza kuwa tatizo kwa kuingiza masuala
ya kibinadamu, yaani yasiyohusu umuhimu katika timu na kuyageuza maamuzi ndani
ya timu.
Mimi
ninaamini kwamba katika timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara, kuna viongozi wenye
tabia hizo ambao wamekuwa wakijenga chuki kati yao na wachezaji na mwisho
wakafanya vitu Fulani bila ya kujadili wanachoamua kitaiathiri klabu.
Badala yake
wanaangalia watafurahisha vipi nafasi zao kwa kuona mchezaji au wachezaji fulani
wanaondolewa katika timu ikiwa ni sehemu ya wao kuwaonyesha wachezaji hao wana
nguvu kiasi gani au jeuri yao ikoje!
Kwenye
kundi la watu wengi lazima kutakuwa na hali ya kutofautiana, hii inatokea
shuleni, maofisini halikadhalika katika timu. Kikubwa ambacho kinaweza
kuwaendesha watu ni vumilifu, kila mmoja kuvumilia sehemu mwenzake
alipopungukiwa.
Pia bado ni
busara kukubali kusamehe kwa kuwa binadamu hatujakamilika na ikiwezekana lazima
kuna kukoseana, viongozi na wachezaji wakubali kusameheana kwa maana ya
kukubali ubindamu lakini pia kuangalia faida ya wanachokitumikia kinatakiwa
kifanikiwe vipi.
Ndiyo maana
nasisitiza, wale wenye tabia ya kujenga chuki na hasa viongozi kwa kuwa tu
wanajua wana ‘mpini’ si sahihi, lazima watafakari mara mbili. Kwamba kama
viongozi, wanachotakiwa kufanya zaidi ni kwa faida ya timu na kwa faida ya
nafsi zao.
Timu lazima
ziendeshwe na watu, ili mambo yaendelee watu lazima wapishane mawazo kwa maana
ya kutofautiana na mwisho watakaa na kujadili hadi kupata jibu moja ambalo
litafanyiwa kazi ili kusukuma maendeleo ya timu.
Kama suala
la wachezaji watovu wa nidhamu litaendelea kushughulikiwa kwa faida ya timu,
halafu hili la viongozi wenye chuki na gubu likaachwa, basi itakuwa na kutwanga
maji katika kinu.
Lazima
mkubali, kwamba kama binadamu lazima mtakosea. Hivyo vizuri kila mmoja kukubali
makosa ya mwenzake, msahihishane na muombane radhi lakini mwisho, kila mmoja
lazima akubali kwamba kama timu lazima maslahi ya timu yawe mbele kuliko yale
binafsi, hii ndiyo maana ya professional.







0 COMMENTS:
Post a Comment