Na Saleh Ally
Mchezo wa
soka nchini unaathiriwa na mambo mengi sana, lakini bahati mbaya wengi wamekuwa
wakiyafanya mambo hayo kama hadithi za kupita bila ya kuyashughulikia.
Soka ni
mchezo wenye mashabiki wengi zaidi nchini na duniani kote, ni biashara kubwa na
inayoweza kutoa ajira kwa wingi kwa vijana na Watanzania wengine, tena wakapata
mishahara bora kabisa na kuepusha mambo mengi kama vijana kuwa vibaka au
watumiaji madawa ya kulevya.
Ndani ya
soka kuna wigo mpana sana, utapata ajira, fedha pamoja na afya. Ndiyo maana
nataka kuzungumzia matatizo yanayoonekana kama kitu cha kawaida na kuachwa
yapite hivihivi.
Kila timu
inayoshiriki Ligi Kuu Bara, sasa ipo kwenye mchakato wa kujenga kikosi imara na
moja ya mikakati mikubwa ni usajili.
Usajili una
wigo mpana sana, lakini tatizo kubwa ambalo limekuwa likiyumbisha mambo mengi
sana ni ubinafsi wa watu ambao zaidi wanaangalia nafsi zao kuliko hali halisi
na kwa kifupi mambo mengi hayaendi kitaalamu.
Matumbo:
Wapo watu
ndani ya klabu nyingi nchini ambao wamekuwa wakishiriki katika zoezi la usajili
kama wahusika na wao zaidi wanaangalia watapata kiasi gani ili wafaidishe
matumbo yao kuliko klabu itafaidika na kipi.
Mwaka 2004
nikiwa nchini Rwanda kuripoti michuano ya Kombe la Kagame, kulitokea mgogoro
mkubwa katika Klabu ya Rayon Sports ambayo haikuwa ikishiriki kwa kuwa wenyeji
waliwakilishwa na APR na Kiyovu.
Tatizo
kubwa lilikuwa ni kocha mmoja raia wa DR Congo kulaumiwa kuwa alikuwa akichukua
fedha kwenye usajili wa wachezaji na wengine walilia alikuwa akikata hadi
mishahara yao.
Mambo
hayakuisha kimyakimya, mwishowe kocha huyo alitupiwa virago na wengine
waliokuwa wakishirikiana naye wakaonywa kwa kuwa mtandao ulikuwa mkubwa.
Hata hapa
nyumbani mtandao ni mkubwa na hasa katika klabu za Yanga na Simba. Wapo watu
ambao siku zote ninaeleza hutaka kuonyesha wana mapenzi makubwa na klabu hizo,
kumbe wanajua wanafaidika vipi, maana yake hawazipendi bure!
Watu hawa
husajili wachezaji kwa lengo la kupata ‘ten percent’, hapa kwa kuwa wanaangalia
zaidi maslahi yao, basi kama mchezaji bora atagoma kuwapa ‘kitu kidogo’, halafu
yule asiye bora anakubali, watamchukua.
Utaona hapa
klabu ndiyo imeharibikiwa kwa kuwa itakosa mchezaji bora na kupata bora
mchezaji ili watu washibishe matumbo yao. Haya mambo yanafanyika na wahusika
wanajua.
Watoto wa mjomba:
Nimetumia
jina la ‘mtoto wa mjomba’, lakini inawezekana akawa wa shangazi, nyumba ndogo
na vinginevyo. Ufafanuzi ni kwamba kuna ambao wanahusika na usajili huangalia
nafsi zao na si faida kwa timu.
Kwa kuwa
mtu fulani amepewa nafasi katika kamati ya usajili au ana sauti kwa kuwa yupo
karibu na mwenyekiti au katibu wa Yanga au Simba, basi anapiga debe na kutoa
nafasi ya mtoto wa ndugu yake kufanyiwa majaribio.
Halafu
anakwenda kwa kocha anayejua ndiye anatakiwa kupitisha ubora wa mchezaji na
kumueleza anahitaji msaada wake. Siku ya mwisho mtoto wa mjomba anapita na
kupata nafasi ya kuichezea Simba, Yanga au timu nyingine, hatimaye anakuwa mtu
wa benchi.
Hili jambo
limekuwa likionekana ni kama stori ya kawaida na mambo yanaendelea kutokea kila
kukicha, hasa katika kipindi kama hiki cha usajili.
Kweli klabu
ndiyo inayoumia na wanaofaidika ni hao watu wachache bila ya kujua madhara ya
baadaye kwa klabu ambayo inakuwa imetoa fedha nyingi halafu inakuwa na kikosi
dhaifu.
Kwa nini
kikosi ni dhaifu? Kwa kuwa watu fulani wamepata fedha, wamekula au
wamewafaidisha ndugu zao!
Vitu hivi
viwili ni sehemu ya sumu inayofanya soka ya Tanzania endelee kudumaa na
wachache hao wakigeuza kipindi cha usajili ni mtaji kwao.
Makocha
mfano Abdallah Kibadeni kwa Simba, Ernie Brandts kwa Yanga ambao ndiyo
wataalamu, wapewe nafasi ya kufanya kazi yao kwa faida ya klabu na vikosi vyao.
Kuna kila sababu ya kusema wao ndiyo wahusika wakuu, ingawa wanaweza kushauriwa,
sawa, lakini si kuelekezwa.
Kwa wale
ambao wanaangalia nafsi na matumbo yao, lazima wakumbuke kwamba mashirika mengi
ya umma yalikufa kwa kuwa watu wengi walifanya kama wanavyofanya wao sasa.
Hivyo vizuri wakawa waungwana na kufanya kazi kwa uaminifu na kufuata weledi.







0 COMMENTS:
Post a Comment