NGASSA SIKU YA KWANZA MAZOEZINI YANGA.. |
*Azungumzia tena kuhusu
Msuva, asisitiza namba Yanga hazina mwenyewe
Na Saleh Ally
KOCHA Mkuu wa Yanga,
Ernie Brandts anaanza msimu mpya ambao utakuwa na mambo mengi sana lakini
kikubwa zaidi ni kuthibitisha kama kweli alichokifanya msimu uliopita hakikuwa
ni cha kubahatisha.
Brandts ameanza
maandalizi ya msimu mpya baada ya Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Huu
ndiyo msimu mgumu zaidi kwa kocha huyo Mholanzi ambaye anataka kikosi chake
kuwa na maandalizi mazuri zaidi.
Pamoja na usajili,
Brandts ambaye anasema wazi kuwa bado anamhitaji mshambuliaji Moses Oloya
Mganda anayekipiga nchini Vietnam lakini ujio wa Mrisho Ngassa nao umekuwa ni
gumzo kubwa sana.
Anasema anajua kwamba
Ngassa ni gumzo kutokana na umaarufu wake na uwezo alionao na amekuwa akifanya
vizuri katika soka ya Tanzania kwa kipindi kirefu sasa.
Lakini anasisitiza kwamba
katika kikosi chake kila mchezaji yuko sawa na mwingine, hakuna mwenye uhakika
na namba zaidi ya kumuonyesha kocha anastahili kucheza. Maana yake, Ngassa
atatakiwa kufanya mambo matatu makubwa ili kuendelea kupata nafasi katika
kikosi chake.
Ngassa alianza mazoezi
juzi, kwa mara ya kwanza kocha huyo akamuona Ngassa akifanya mazoezi chini yake
na siku iliyofuata akampa ruhusa ajiunge na kikosi cha timu ya taifa, Taifa
Stars kinachojiandaa na michuano ya Kombe la Chan. Stars itacheza na Uganda
ikianzia nyumbani.
SALEHJEMBE: Nini hasa
Ngassa anatakiwa kufanya ili kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza?
Brandts: Kunaweza kuwa na
mambo mengi sana, lakini matatu yatakuwa muhimu sana kwangu. Kwanza kabisa ni
kuhusu kujituma, lazima afanye hivyo kwa kuwa ana kipaji. Lakini bila ya
kujituma, hakuwezi kuwa na tofauti na mwenye kipaji na asiyenacho.
SALEHJEMBE: Pili na tatu
ni kipi?
Brandts: Kucheza kwa faida
ya timu, mara kadhaa nimeangalia mechi alizocheza akiwa Simba. Lazima ajue
mchezaji anafanya kila analoweza kuisaidia timu yake. Hivyo Ngassa lazima aweke
hayo kichwani wakati akiitumikia Yanga.
SALEHJEMBE: Malizia jambo
la tatu.
Brandts: Kuna mabadiliko
anayotakiwa kuyafanya kiuchezaji, nafikiri nitazungumza naye mwenye na
kumueleza. Wakati akicheza Simba au timu ya taifa nimekuwa nikiyaona. Najua ana
kipaji cha juu sana, hivyo hayo mambo lazima ayafanyie kazi.
SALEHJEMBE: Labda
utakutana naye lini?
Brandts: Sasa ana
majukumu ya timu ya taifa na tayari nimetoa ruhusa kwa wachezaji walio na
kikosi cha Taifa Stars, lakini atakaporejea mazoezini, basi nitazungumza naye
na huu ni utaratibu wa kawaida wa kuzungumza na wachezaji wote ikiwezekana kila
mmoja kwa wakati wake.
SALEHJEMBE: katika siku
yake ya kwanza ya mazoezi na Yanga, kuna kitu umeona?
Brandts: kitu kipi?
SALEHJEMBE: Ambacho anacho
Ngassa na huenda kimekuvutia?
Brandts: Amenifurahisha
kwanza kuwahi, pili alifanya mazoezi kwa kujituma na huenda akaendana na
ninachokitaka. Ingawa kuna kitu kidogo alikosea na nikamuonya.
SALEHJEMBE: Siku ya kwanza
tu, kitu gani?
SALEHJEMBE: Unafikiri kuwa
na mchezaji nyota kama Ngassa kunaweza kukusumbua?
Brandts: (Tabasamu) Mimi
nilikuwa mmoja wa nyota wa Uholanzi ambao walicheza Kombe la Dunia. Huenda ni
nyota zaidi, lakini nidhamu yangu iko juu na ndiyo maana kazi yangu
inafanikiwa. Nimesisitiza sana la kujituma, hili linajumuisha nidhamu ambayo ni
sehemu ya mafanikio.
SALEHJEMBE: Ngassa ni winga,
awali ulikuwa ukimtumia Simon Msuva, ndiyo kusema sasa ataozea benchi?
Brandts: Kila mchezaji
ana nafasi yake Yanga, hapa muhimu ni suala la kujituma kutoka kila upande.
Kama nilivyosema, Yanga hakuna mchezaji mwenye uhakika wa namba asilimia mia.
Kila mmoja lazima ajitume kuoyesha anataka na anaweza kuisaidia timu.
SALEHJEMBE: Bado haujajibu
kuhusu Ngassa na Msuva?
Brandts: Ndiyo nimejibu,
labda nifafanue zaidi. Kutokana na juhudi zao mazoezini, Msuva na Ngassa wote
wanaweza kucheza kutokana na viwango vyao vilivyo au anaweza kucheza Msuva
halafu Ngassa akakaa nje, inategemea anajituma vipi mazoezini.
SALEHJEMBE: Kwani utatumia
mfumo upi?
Brandts: Mifumo ni mingi,
iko ambayo atacheza mmoja na mwingine kubaki benchi, lakini kuna mfumo ambao
wanaweza kucheza wote. Hapa itategemea viwango vyao na wenyewe wako katika
viwango vizuri kiasi gani, hasa kutokana na ninachokiona mazoezini.
0 COMMENTS:
Post a Comment