*Aeleza Yanga
walivyomfuata, azungumzia nguvu ligi kuu
Na Saleh Ally
Mshambuliaji nyota wa
Vital’O ya Burundi, Hamis Tambwe ametua nchini juzi Jumatano tayari kumalizana
na Simba ili aichezee katika msimu mpya wa 2013/14.
Tambwe raia wa Burundi na
mshambuliaji tegemeo wa timu ya taifa ya nchini hiyo, Intamba Murugamba ametua
nchini kuzungumza na Simba ikiwa ni siku chache baada ya kuisaidia Vital’O
kubeba Kombe la Kagame katika michuano iliyofanyika nchini Sudan.
Katika michuano hiyo,
Vital’O ilifanikiwa kufika fainali na kucheza dhidi ya APR ya Rwanda katika
mechi iliyokuwa na upinzani mkubwa kwa maana ya nchi hizo zina utani wa jadi
kisoka.
Pamoja na upinzani huo,
Tambwe ambaye ni nahodha wa Vital’O aliiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi wa
mabao 2-0, yeye akiwa amepachika moja na Deo Ndayishimiye akapachika la pili.
Katika michuano hiyo, Tambwe
ameshinda vitu vitatu muhimu na huenda ikawa ni moja ya rekodi chache za
michuano hiyo ya Kombe la Kagame tokea ianzishwe.
Kwanza ameisaidia Vital’O
kubeba Kombe la Kagame, pili ameibuka mfungaji bora na ametangazwa kuwa
mchezaji bora wa michuano hiyo.
Mshambuliaji huyo
amefanikiwa kushinda makombe matatu katika michuano hiyo, kitu ambacho kinampa
jeuri ya kusisitiza kwamba hajaja Simba kujaribiwa.
Mara baada ya kutua
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa sita usiku,
Championi lilifanya naye mahojiano na moja kwa moja akaeleza kuhusiana na ujio
wake.
Salehjembe: Utafanya
majaribio na Simba muda gani?
Tambwe: Naweza kusema
sijaja hapa kufanya majaribio, Simba wameona kazi yangu. Hivyo, nataka
kuzungumza nao na kujua tutafikia vipi.
Salehjembe: Kusaini ni
nia na kuipenda sehemu, nia ya kusajili kwako ni vipi au zaidi unaangalia maslahi.
Tambwe: Maslahi ndiyo
maisha, lakini ninavutiwa na Simba ndiyo maana nikakubali kuja. Nina ofa nyingi
tu.
Salehjembe: Labda kutoka
katika timu zipi?
Tambwe: Kwa sasa siwezi
kusema, ngoja nimalizane na Simba kwanza ili nijue.
Salehjembe: Kuna taarifa
Yanga pia walikufuata?
Tambwe: Kweli,
nilizungumza nao na wakataka niwatumie CV (wasifu) wangu na nikafanya hivyo.
Salehjembe: Vipi sasa
umekuja Simba, wakati umetuma CV?
Tambwe: Simba walianza kabla
ya Yanga na nimekuambia ninavutiwa nao.
Salehjembe: Uliwahi
kukutana nao ukiwa na Vital’O?
Tambwe: Nakumbuka ilikuwa
hapa Dar es Salaam katika michuano ya Kagame na mechi iliisha kwa sare ya bila
kufungana.
Salehjembe: Je,
unaifuatilia ligi ya soka ya Tanzania?
Tambwe: Ninafanya hivyo,
ligi ya hapa wachezaji wanatumia nguvu sana tofauti na Burundi, kule kuna
ufundi mwingi sana.
Salehjembe: Hauna mwili
mkubwa, utaweza kupambana na umeshasema ligi ya hapa ni nguvu zaidi?
Tambwe: Nimeamua kuja
hapa, najua nitaweza hata kama itakuwa ni baada ya kipindi fulani.
Salehjembe: Ukiachana na
mabao yako sita yaliyokupa ufungaji bora, taarifa zinasema umekuwa mfungaji
bora Burundi kwa misimu miwili mfululizo?
Tambwe: Ni msimu huu
ndiyo nimekuwa mfungaji bora, nilifunga mabao 18, lakini nilikuwa na mengine
mawili katika michuano ya Rais Nkurunzinza. Jumla nimefunga mabao 20 msimu
uliopita.
Salehjembe: Kabla ya hapo
pia ulikuwa mfungaji bora?
Tambwe: Hapana nilishika
nafasi ya pili, nilifunga mabao 16 wakati mfungaji bora akawa na 18 pia.
Salehjembe: Lini
unakutana na viongozi wa Simba?
Tambwe: Kweli sijajua,
mimi nawasikiliza wao ambao ni wenyeji.
Salehjembe: Karibu Dar es
Salaam.
Tambwe: Nashukuru sana.







0 COMMENTS:
Post a Comment