Rais wa Shirikisho Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kikosi cha Taifa Stars sasa kina uwezo
wa kushindana katika mashindano yoyote, kwani tayari kimeiva.
Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo
kambini kwao hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Rais Tenga aliwaambia kuwa
kiwango walichoonesha kwenye mechi zilizopita za mchujo za Kombe la Dunia dhidi
ya Morocco na Ivory Coast kimethibitisha hilo.
“Kiwango mlichoonyesha katika mechi
hizo kila Mtanzania anayewafuatilia amekiona, hivyo hatuna shaka kuwa
mtatuwakilisha vizuri kwenye mechi ya kesho dhidi ya Uganda,” amesema Rais
Tenga na kuwataka kupigana kwa ajili ya Tanzania.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager kesho (Julai 13 mwaka huu) saa 9 kamili alasiri
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itacheza na Uganda (The Cranes) katika mechi ya
kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za CHAN
zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Rais Tenga amesema TFF, mdhamini
Kilimanjaro Premium Lager, Kamati ya Ushindi na Watanzania kwa ujumla
wanawaunga mkono kwani wamekuwa wakiboresha kiwango chao kila wanavyozidi
kucheza mechi tangu wake chini ya Kocha Kim Poulsen, Mei mwaka jana.
Wakati huo huo, Rais Tenga ameahidi
kumpatia tiketi ya kwenda Uganda kwenye mechi ya marudiano mshabiki Wiseman
Mwakyusa Luvanda anayetembea kwa miguu kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam
kushuhudia mechi ya kesho.
“Kama ni kweli anakuja kwa kutembea,
huyu ameonyesha kiwango kikubwa cha uzalendo kwa timu ya Taifa, nitampatia
tiketi ya kwenda Kampala kuishangilia Taifa Stars kwenye mechi ya marudiano,”
amesema Rais Tenga.
POULSEN,
MICHO:
Makocha wa timu hizo Kim Poulsen wa
Taifa Stars na Sredojvic Micho wa The Cranes wamesema mechi ya kesho itakuwa
ngumu kwa vile kila mmoja amejiandaa kuhakikisha anafanya vizuri.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari
leo, makocha wote waliezea ubora wa wapinzani wao, lakini wakasisitiza kuwa
wanaingia uwanjani kuhakikisha wanashinda ili kujiweka katika mazingira mazuri
kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa Kampala wiki mbili zijazo.
Kim alisema Uganda ndiyo inayoongoza
kwa ubora wa viwango vya FIFA katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati,
hivyo ni changamoto kwao ingawa wachezaji wake tayari wamejipanga vizuri kwa
ajili ya mechi hiyo.
Naye Micho aliyefuatana na nahodha
wake Hassan Wasswa alisema Taifa Stars imekuwa ikifanya vizuri tangu iwe chini
ya Kim, na itakuwa na wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza kinachocheza mechi za
mchujo za Kombe la Dunia wakati kwa upande wake atakuwa na wachezaji wawili tu.








0 COMMENTS:
Post a Comment