August 16, 2013



 
VINCENT KOMPANY-MAN CITY
Na Saleh Ally
Utamu wa Ligi Kuu England ‘Premiership’ unaanza kesho Jumamosi, kila timu itashuka dimbani ikitaka kuchukua pointi tatu kwa kuwa “biashara ni asubuhi.”

Burudani ni nyingi, ndiyo maana Premiership inakuwa ligi maarufu zaidi ya soka duniani na moja ya vitu ambavyo watu wanategemea kuviona ni namna makocha na manahodha wa timu 20 watakavyokuwa wanaziongoza timu zao.
 
RON VLAAR MACRON-ASTON VILLA
Ubingwa wa England ni kwa timu yoyote, lakini hakuna ubishi ni timu tano tu hupewa nafasi ya kuutwaa ambazo ni Manchester United, Manchester City, Chelsea, Arsenal na Liverpool na kweli imekuwa hivyo miaka nenda, rudi.
 
NEMANJA VIDIC-MAN UNITED

England iliyo ndani ya Uingereza, imekuwa ikisifika kwa kuhakikisha inatoa nafasi kubwa kwa wachezaji na makocha wake kushiriki katika ligi hiyo maarufu.


Lakini kiasi kikubwa inaonekana imezidiwa nguvu na utaalamu na uwezo halisi wa soka, kwani ukihesabu kati ya makocha na manahodha 20 walio katika ligi hiyo, wengi wanatokea nchi jirani.

Kati ya manahodha 20, 11 ambao ni zaidi ya nusu wanatokea katika nchi nyingine zikiwemo Scotland na Wales zilizo ndani ya Uingereza lakini zina bendera inayojitegemea kama nchi hasa.

Kwa upande wa makocha watakaoongoza timu 20, kati yao 15 wanatokea nje ya England na hii ni zaidi ya asilimia 70 ya makocha wote, maana yake taratibu inaonekana England wanashindwa na nguvu halisi.

Mfano kwa karibu misimu kumi, hakuna timu imebeba kombe ikiwa chini ya kocha kutoka England, Alex Ferguson kutoka Scotland ndiye alibeba makombe mengi, halafu kuna Jose Mourinho kutoka Ureno, Mfaransa, Arsene Wenger na Muitalia, Carlo Ancelotti.

England ina makocha maarufu kama Harry Redknapp, Sam Allardyce na Alan Pardew lakini wengi wamekuwa wakipigania kuziokoa timu zisishuke daraja au kuwania kucheza michuano ya Europa na si kutwaa ubingwa.

Inaonekana ubingwa umekuwa ni wa makocha wageni na ikiwezekana hata manahodha ndiyo wamekuwa na nafasi ya kubeba makombe hayo.

Hali ilivyo kama utakwenda katika timu zote tano zinazopewa nafasi ya kutwaa ubingwa, ni Liverpool na Chelsea zenye manahodha Waingereza, zilizobaki wote ni wageni.

Man City na Arsenal manahodha wake wanatokea Ubelgiji wakati Man United nahodha wake ni raia wa Serbia.

Wakati kivumbi kinaanza ‘kusambaa’ kesho, swali la kujiuliza ni kocha yupi atakiongoza kikosi chake kumbeba mwari huyo anayemilikiwa na Man United kwa sasa, lakini kwa manahodha, yupi mikono yake italiinua kombe hilo?

Wafuatao ni makocha na manahodha wa timu zote za Premiership nchi, na vikosi wanavyoviongoza;

TIMU                        KOCHA                                      NAHODHA
1.Arsenal                  Wenger (Ufaransa)            Thomas Vermaelen  (Ubelgiji)
2. Aston Villa           Lambert  (Scotland)           Ron Vlaar Macron (Uholanzi)
3. Cardiff City          Mackay  (Scotland)            Mark Hudson (England)
4. Chelsea                 Mourinho (Ureno)             John Terry (England)
5. Crystal Palace     Holloway (England)           Paddy McCarthy (Ireland)
6. Everton                Martínez (Hispania)           Phil Jagielka (England)
7. Fulham                  Jol  (Uholanzi)                    Brede Hangeland  (Norway)
8. Hull City                Bruce (England)                  Robert Koren  (Slovenia)
9. Liverpool             Rodgers (Ireland)               Steven Gerrard (England)
10. Man City            Pellegrini (Chile)                 Vincent Kompany (Ubelgiji)
11. Man United      Moyes (Scotland)               Nemanja Vidić  (Serbia)
12. Newcastle         Pardew (England)             Fabricio Coloccini (Argentina)
13. Norwich City    Hughton (Ireland)              Russell Martin (Scotland)
14. Southampton   Pochettino (Argentina)  Adam Lallana (England)
15. Stoke City          Hughes  (Wales)                 Ryan Shawcross (England)
16. Sunderland        Di Canio (Italia)                  John O'Shea  (Ireland)
17. Swansea City    Laudrup (Denmark)            Ashley Williams (Wales)
18. Tottenham        Villas-Boas (Ureno)            Michael Dawson  (England)
19. West Brom        Clarke (Scotland)               Chris Brunt (Ireland)
20. West Ham         Allardyce (England)           Kevin Nolan (England).

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic