August 16, 2013



Na Saleh Ally
Hivi karibuni Yanga waliamua kuanzisha mjadala kuhusiana na malipo ya matangazo ya mechi za Ligi Kuu Bara, na tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeishasaini mkataba wa awali na Azam TV na kama hadi mwisho hakutakuwa na malalamiko hadi mwezi mmoja, mkataba kamili utasainiwa.

Yanga walikuwa wakipinga kwamba Sh milioni 100 zinazotolewa na wadhamini Azam TV kwa msimu kwa kila timu hazikuwa sahihi, sehemu ya hoja za Yanga ni kwamba wao ni timu kubwa na fedha hizo ni chache.
 
BAKHRESA, MMILIKI WA AZAM TV NA AZAM FC..
Baada ya siku chache timu 13 za Ligi Kuu Bara, zikatoa taarifa kwa vyombo vya habari kuonyesha zinapingana na Yanga na msimamo wao ulikuwa ni kuendelea na mkataba wa Azam TV.

Ukiangalia kwa undani utagundua kila upande unapambana kupata maslahi yake, utaona wakongwe wengine Simba wako upande wa klabu nyingine 12 kwa kuwa tayari wao wana mkataba na Azam TV ambao ni pembeni na watapata Sh milioni 331 kupitia Simba TV.

Timu 13 zote zimeridhika na maslahi yao, timu nyingine ukiacha Simba, kama zitalipwa Sh milioni 100 kwa msimu, kwao ni bingo. Simba tayari ina malipo mikataba miwili, hivyo imeridhika pia.


Hapa ndipo ninasema Yanga wana hoja, hawajaridhika na wana haki ya kusema. Sidhani kwamba ni sahihi kuridhika tu kwa kuwa wengine wamekubali, kwa viongozi makini lazima wafikirie maslahi ya wanachokiongoza.

Inawezekana katikati kuna tatizo la kufikiria na kuamini kuhusu suala hilo, hoja nyepesi zimeingia katikati na sasa zinahusisha utajiri wa Said Salim Bakhresa na Yusuf Manji ambao ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa hapa nchini.

Manji ni mwenyekiti wa Yanga na Bakhresa ndiye mmiliki wa Azam TV  na Azam FC ambayo ni moja ya timu imara sasa na wapinzani wakubwa wa Yanga katika Ligi Kuu Bara.

Kuna hoja kadhaa za Yanga kama kweli watapata haki kutangazwa kwenye Azam TV wakati timu hiyo ni wapinzani wao katika ligi? Wadau wengi wameibeza hiyo hoja, lakini kweli Yanga wanapaswa kuhoji kwa kuwa vyombo vya habari kadhaa vimekuwa vikifanya propaganda kutetea maslahi na hili liko dunia nzima, hakuna kosa kuhoji katika hili.

Kuhusiana na suala la mchakato wa tenda ulivyokuwa, kweli TFF ndiyo wenye haki na haki za matangazo ya runinga, lakini Yanga wanakuwa ni washiriki kama zilivyo klabu nyingine hivyo wanaweza kuhoji pia kuhusiana na hilo.

Kuhusu malipo, hapa ni sehemu muhimu sana. Kweli shilingi milioni 100 zinaweza kuwa nyingi kwa Rhino au Ruvu JKT au hata Kagera Sugar. Lakini isiwe hivyo kwa Yanga, ni fedha nyingi na si haba, lakini bado klabu hiyo ni kubwa.

Yanga ina uwezo wa kuingiza mara mbili au tatu ya fedha hizo katika mechi moja. Au imekuwa ikiingiza nusu ya fedha hizo kwa mechi moja ambazo imelipwa kwa msimu mzima. Mtibwa Sugar au Mbeya City haziwezi kuingiza fedha hizo.

Angalia asilimia 85 ya timu za Ligi Kuu Bara zinasubiri kucheza na Yanga au Simba ili kupata mapato makubwa ya viingilio vya milangoni. Kama sivyo, kama zinakutana zenyewe kwa zenyewe basi zinaingiza hadi Sh 56,000 au laki moja tu!

Lakini bado utaona kuwa kama mechi zinaonyeshwa kwenye runinga basi kuna uwezekano wa kupungua kwa mapato kwa kuwa wako ambao wataamua kubaki na kuangalia kwenye runinga.
Kama hiyo haitoshi, Azam FC lazima itatengeneza fedha nyingi kupitia matangazo na hakuna ubishi kwamba katika mechi zitakazohusisha Yanga au Simba, ndiyo itaingiza fedha nyingi kwa kuwa wadhamini watakuwa tayari kulipia matangazo kwa kuwa wanajua mechi hizo zitaangaliwa na watu wengi zaidi.

Hapa ndipo kunakuwa na hoja ya msingi ya Yanga kuhoji, ingawa imeshindikana hata baada ya wote kukutana kwa waziri, lakini walikuwa na hoja ambayo ilipaswa kuwa na majibu na hasa kama uongozi wa Simba pia ungeweza kufikiria mbali na kuamini kuwa mikataba miwili ya Sh milioni 100 na ule wa Sh milioni 331 ilikuwa tofauti, hivyo bado wangeweza kupigania kuongezwa kwenye ligi.

Azam FC kupata nafasi ya kuonyesha ligi ni jambo zuri zaidi kwa kuwa ni runinga ya hapa nyumbani, hili ni jambo zuri zaidi. Lakini bado kuna la kuhoji kuhusu maslahi kwani ni jambo zuri zaidi na haki hiyo iko wazi, hakuna sababu ya upande mmoja kuuzuia mwingine.

Kuhoji kwa Yanga, kumesababisha kufanyika kwa mikutano kadhaa, wamekwenda hadi kufanya mkutano katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Naibu Waziri, Amos Makala, aliongoza kikao kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Mwisho inaonekana kikao hicho kimezaa kingine kati ya Yanga na Azam FC, lakini sasa mwanasheria wa Yanga atapata nafasi ya kukaa na mwanasheria wa kamati ya ligi na kuchambua mambo ya msingi.

Azam FC sasa watakwenda kwenye kikao na Yanga wakijua nini kinatakiwa na huenda mwisho majibu ya kikao hicho yakawa ni maslahi bora zaidi kuliko klabu nyingine. Lakini mwanasheria wa Yanga tu, si wa klabu nyingine 13, atapata nafasi ya kuchambua mambo kadhaa muhimu.

Inawezekana kabisa kuna vitu kadhaa Yanga waliteleza wakati wa kupeleka madai yao, lakini walikuwa na hoja za msingi na haki ya kupambana kwa ajili ya maslahi yao. Ndiyo maana wakati wanaanza walisema kuhusu Yanga na si klabu nyingine.

Bado nasisitiza, huenda Yanga wakaonekana kama ‘majuha’ leo, lakini siku nyingine wakawa mashujaa. Au wanachokidai Yanga leo, huenda Simba au klabu nyingine wakaanza kukidai baada ya msimu mmoja au miwili baadaye.

Lakini siku nyingine linaweza kuwa funzo kwa klabu nyingine kuhusiana na kujali maslahi ya klabu zao kwa kujitambua uwezo wao wa kuingiza kipato na si kukurupuka tu.

Ukiachana na kila, bado nina ushauri kuwa baada ya makubaliano kufikiwa kati ya Yanga na Azam TV, maana yake chombo hicho cha habari kitakuwa kimekubaliana na klabu zote 14 za ligi kuu.

Baada ya hapo, kila upande unapaswa kuheshimu utekelezaji wa jambo hilo tena kwa kina. Yaani klabu zihakikishe zinafanya mambo bila ya kukiuka mikataba na Azam TV nayo ihakikishe inafanya mambo yake kwa kutimiza yaliyo katika mkataba pia.

Kisheria, haki za matangazo ya runinga ziko kwa TFF, lakini bado naona kuna jambo la msingi, kwamba ili klabu zisikiuke mkataba, basi kuna sababu ya kupewa nafasi ziupitie na kujua kipi hasa wanatakiwa kufanya. Au kama TFF inaona mkataba huo ni siri, basi klabu ziandikiwe vipengele muhimu vinavyowahusu na kukabidhiwa.

Msisitizo ni kwamba, hakuna sababu ya kuliweka suala hilo la kishabiki sana. Maana kuna wale ambao wamekuwa wakisema Yanga yaibwaga Azam TV au Azam TV yaishinda Yanga, hiyo si hoja ya msingi badala yake tuangalie hizi timu zinafaidika vipi na si ushabiki wa kijinga.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic