Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
amemshukuru Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kwa kusajili Katiba ya
TFF toleo la 2013 kutokana na marekebisho yaliyofanywa na Mkutano Mkuu Maalumu
uliofanyika Julai 13 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo, Rais Tenga
ameishukuru Serikali, Msajili, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Dk. Fenella Mukangara na Naibu wake Amos Makala kwa ushirikiano ambao wametoa
kwa TFF katika kufanikisha suala hilo.
Amesema baada ya kupokea usajili huo, kinachofuata ni Katibu Mkuu
wa TFF kumwandikia rasmi Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ili aanzishe mchakato
wa uchaguzi wa viongozi wa TFF.
Kuhusu kauli ya Naibu Waziri Makala kuwa marekebisho hayo
yasingeweza kusajiliwa kwa sababu hayakufuata Katiba ya TFF, Rais Tenga
amesema:
“Makala hakuwepo kwenye mkutano ndiyo maana alisema hivyo. Ana
haki ya kuuliza, nina hakika sasa atakuwa ameeleweshwa na ameelewa kwa sababu
ni msikivu. Kuhusu marekebisho hayo kupigiwa kura, hilo lisingewefanyika kwa
sababu hakukuwa na mjumbe aliyepinga marekebisho,” amesema.
“Hakukuwa na dispute (mabishano) kuhusu marekebisho, isipokuwa
wajumbe walitumia muda mwingi kuboresha kanuni na kutoa ushauri wa aina ya watu
ambao wangeingia kwenye kamati mbalimbali zikiwemo zile mpya za Maadili,”
amesema.
Ameongeza kuwa kwa vile wote walioingia kwenye Mkutano Mkuu huo
Maalumu ni watu wa mpira wa miguu wasingeweza kupinga marekebisho kwa vile
yametokana na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
“Labda itokee aliyeingia kwenye mkutano alikosea njia. Mtu yeyote
wa mpira wa miguu ni lazima afahamu kuwa maagizo ya FIFA ni lazima yatekelezwe,
na Katiba ya TFF inasema hivyo,” amesema Rais Tenga.
Pia Rais Tenga amewataka wapenzi wa mpira wa miguu kushawishi watu
wenye sifa na uwezo wa kuongoza kujitokeza kwa wingi wakati Kamati ya Uchaguzi
itakapotangaza mchakato na tarehe ya uchaguzi huo.
0 COMMENTS:
Post a Comment