Straika Simba, Amissi
Tambwe, amesema sasa anafurahia maisha ndani ya kikosi hicho, lakini akatoa
siri nzito kuwa ilisalia nukta moja atue katika Klabu ya Yanga ambayo ni
wapinzani wakubwa wa Wekundu hao.
Tambwe raia wa Burundi, amesema
kati ya klabu mbili za Simba na Yanga, Yanga ndiyo walikuwa wa kwanza kuanza
kuzungumza naye.
Alisema walifika kwake
wakiwa na lengo kubwa la kutaka kumsainisha mkataba lakini alipowaambia
wasubiri mpaka amalize mechi kati ya nchi yake dhidi ya Sudan, hawakurudi tena.
Tambwe amesema mara baada ya
kumalizika kwa mchezo huo, mabosi hao wa Yanga hawakuonyesha tena kuwasiliana
naye kabla ya Simba kuingilia kati kupitia aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa
Wekundu hao, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, aliyefanikisha usajili wake na timu hiyo.
“Mpaka sasa nadhani
ningekuwa Yanga kwa kuwa wao ndiyo waliotangulia kunifuata na kuzungumza na
mimi wakitaka kunisajili, nikawaambia wasubiri lakini baadaye hawakuja tena,
niliwasubiri lakini wakawa kimya, hapo ndipo Simba walipopata nafasi,” alisema
Tambwe ambaye sasa ndiye kinara katika msimamo wa ufungaji akiwa na mabao sita.
“Yanga walifikia pazuri na
hata katika mazungumzo yangu ya mwisho na bosi wao, alikubali hata kwenda
Vital’O kuvunja mkataba wangu, lakini ukimya wao ukawapa nafasi Simba, waliokuja
kupitia Kaburu na kila kitu kilikwenda kwa haraka tofauti na Yanga,” alisema.
Tambwe amesajiliwa na Simba
msimu huu akitokea Vital’O ya Burundi. Kabla ya kujiunga na Wekundu hao,
alifanikiwa kuipa klabu hiyo ubingwa wa Kombe la Kagame huku yeye akiwa
mfungaji bora katika michuano hiyo iliyofanyika Sudan, mwaka huu.







0 COMMENTS:
Post a Comment