Hatimaye uongozi wa Yanga umejinusuru na
adhabu kutoka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufuatia kuwalipa
waliokuwa wachezaji wao, Stephano Mwasyika na Shadrack Nsajigwa ‘Fusso.’
Taarifa ambazo zimelifikia Championi
Jumatano kutoka kwa mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo, imesema tayari
uongozi wao umeshamalizana na nyota hao kwa kuwalipa fedha zote walizokuwa
wakiidai klabu hiyo, ambazo ni jumla ya Sh million 15.5 za usajili.
Bosi huyo (jina tunalo), amesema tayari
wachezaji wote wameshachukua hundi zao za malipo ya madeni hayo. Fusso ambaye
alikuwa nahodha wa timu hiyo, alikuwa akiidai Yanga kiasi cha Sh milioni 9 wakati
Mwasyika, anayekitumikia kikosi cha Ruvu Shooting kwa sasa, alikuwa akidai Sh
milioni 6.5.
“Hatukuona haja ya kulumbana nao sana,
tayari tumeshawalipa fedha zote wiki hii, nafikiri kila mmoja mpaka sasa
atakuwa tayari ameshachukua hundi yake,” alisema bosi huyo.
Kufuatia kauli hiyo ya bosi huyo,
Championi Jumatano lilimtafuta Fusso katika kujua ukweli, ambapo alisema: “Ni kweli
wameshanilipa fedha zangu, siyo kwa nusunusu, binafsi wamenilipa zote, hakuna
tatizo sasa.”
Nyota hao ambao waliachwa na Yanga
mwishoni mwa msimu uliopita, walipeleka malalamiko yao TFF wakidai fedha hizo, baadaye
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliyokaa Septemba 12, mwaka
huu, ikaamuru klabu hiyo ilipe madeni hayo ndani ya siku 14.








0 COMMENTS:
Post a Comment