Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar
Tenga ameishukuru Kamati ya Ligi kwa usimamizi mzuri tangu ilipokabidhi Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) katika mzunguko wa pili msimu uliopita.
Amesema TFF iliamua kuanzisha Kamati ya Ligi kwa lengo la kutaka
klabu zijisimamie zenyewe ili kuongeza ufanisi, jambo ambalo limeleta
mabadiliko kwa vile hivi sasa hakuna matatizo katika kuwalipa marefa na
makamisha wanaosimamia VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
“Fedha za udhamini sasa zinakwenda moja kwa moja kwenye Kamati ya
Ligi. Ni matarajio yangu kuwa ufanisi utaongezeka, kwani tumeanzisha jambo hili
kwa lengo la kuleta tija, maendeleo na utulivu,” amesema Rais Tenga wakati
akizungumza na Wahariri wa Michezo kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
Rais Tenga amesema mahali penye utulivu na utawala bora watu
wanakuwa na imani hasa katika masuala ya fedha, hivyo ni lazima kwa kampuni
kuwekeza kwa vile kunakuwa hakuna vurugu.
Amesema ukiondoa Afrika Kusini na Angola katika ukanda huu wa
Afrika Mashariki, Kati na Kusini, Ligi Kuu ya Tanzania ndiyo yenye udhamini
mkubwa kupitia mdhamini wa ligi na udhamini wa matangazo ya televisheni.
Pia amesema kuanzia msimu ujao 2014/2015 klabu za Ligi Kuu
hazitaruhusiwa kusajili wachezaji hadi zitakapowasilisha TFF ripoti zao za
mapato na matumizi zilizokaguliwa (Audited accounts), hivyo klabu husika
zijiandae kwa ripoti hizo za Januari hadi Desemba 2013.
Kuhusu tiketi za elektroniki, Rais Tenga amesema bado linafanyiwa
kazi na CRDB ambayo ndiyo iliyoshinda tenda hiyo na liko katika hatua nzuri,
kwani nia ya TFF na benki hiyo kuona kuwa linaanza haraka iwezekanavyo.
“Tiketi za elektroniki zimechelewa kuanza kwa sababu ambazo
haziwezi kuzuilika, lakini CRDB imeshatengeneza miundombinu katika karibu
viwanja vyote. Kulitokea uchelewaji katika kuleta printer (mashine za
kuchapia), zilizokuja hazikuwa zenyewe. Kwa upande wa Uwanja wa Taifa, system
(mfumo) iliyopo inatofautiana na ile ya CRDB. Hivyo sasa tunaangalia uwezekano
wa zote mbili zitumike kwa pamoja, kwa sababu Uwanja wa Taifa una system yake
tayari. Printer zimeshafika, tunataka ili suala lisitucheleweshe,” amesema.
0 COMMENTS:
Post a Comment