Na Saleh Ally
Inajulikana mchezo wa soka ulivyo na
mashabiki wengi, lakini hakuna ubishi kwamba wengi wao ni wanaume na kuna
wanawake wengi hawataki hata kuusikia.
Ambao hawataki kuusikia mchezo wa soka,
ujue umewaathiri na wengi wamekuwa wakiulaani kutokana na kuingilia uhusiano
wao au familia zao.
Wanaume wanakuwa kama wendawazimu
linapofikia suala la mchezo huo unaopendwa kuliko yote duniani. Hali hiyo
inasababisha kupungua kwa upendo na mambo mengi ya msingi ambayo wanayahitaji.
Wakati fulani, Championi lilifanya
uchunguzi wa takribani miezi miwili kuhusiana na wanawake na mchezo wa soka
ikaonyesha zaidi ya 67% ya wanawake wenye umri kuanzia miaka 25, hawafurahiswi
na mchezo wa soka.
Ambao hawafurahishwi wengi wanaonekana
kuwa wameolewa au tayari wako katika uhusiano na wanaamini mchezo wa soka ni
tatizo kwao.
Mfano kwa wale wanaume zao
wanaolazimika kwenda kuangalia kwenye baa au nje ya nyumbani, wanaona ndiyo
chanzo cha kupatikana kwa ‘nyumba ndogo’.
Lakini hata wale wanaume zao
wanaoangalia nyumbani kwa kuwa kipato kinawaruhusu kuweka Dstv, wanaona hawana
raha kwa kuwa wanaume zao wanakuwa na mapenzi makubwa na soka kuliko wao hasa
ndani ya dakika 90.
Kwa wasichana wenye umri kuanzia miaka
17 hadi 25, wao asilimia 74 wanaonekana hawana matatizo na mpira kwa kuwa
wapenzi wao wanaweza kwenda kuangalia nao mpira iwe uwanjani au kwenye baa.
Ila katika umri huo, hadi asilimia 39 wanaonekana
kutojali kuhusiana na soka na ikiwezekana wengine hawajui lolote kabisa
kuhusiana na mchezo huo.
Hii ni sehemu ya uchunguzi mdogo tu wa
hapa nyumbani, lakini hivi karibuni umefanyika uchunguzi nchini England ambao
unaonyesha kuwa na mengi zaidi hadi madhara ya kiafya.
Suala la soka kutokuwa rafiki wa ndoa
limepewa nafasi hadi kwenye uchunguzi huo wa England, lakini wameongeza baadhi
ya mashabiki wa timu wanaoathirika
kiafya.
Waingereza hao wamesema kwa asilimia 63 wamesema wanachukizwa na mchezo wa soka kwa kuwa unawapokonya wapenzi au waume zao na kipindi kigumu zaidi ni kile cha Ligi Kuu England.
Pamoja na hivyo, mashabiki wa Manchester
United kwa asilia 52 wanaongoza kwa kula vyakula vya ‘takeaway’ ambavyo
vinasifika kwa kuongeza haraka uzito na hatari kwa afya.
Mashabiki wa Chelsea, wameshika uongozi
wa kunywa pombe nyingi zaidi kwa asilimia 48. Wastani wa shabiki mmoja ni bia
nne kwa kila mechi ingawa wamekuwa wakijitahidi kutoingia katika vitendo vingi
vya vurugu.
Kwa upande wa West Ham, mashabiki wake
wamechukua namba moja kwa uvutaji sigara katika kipindi cha mechi zao,
wanaongoza kwa asilimia 35 lakini pia wanasifika zaidi kwa kucheza kamari
kuliko wa timu nyingine ya England.
Kwa upande wa Manchester City,
mashabiki wao wameingia katika tatizo la kuongezeka uzito katika kipindi cha
Ligi Kuu England. Wameelezwa kuongezeka zaidi ya asilimia 34 katika kipindi cha
baridi kwa kuwa hulazimika kula mara kwa mara wanapokuwa uwanjani.
Mashabiki wa Tottenham Hotspur, wao
wamekiri kuwa kwa asilimia 23 wamekuwa wakipunguza kushiriki ngono kutokana na
hamu ya kufuatilia zaidi ligi hiyo na hasa timu yao inaendeleaje.
Asilimia 38 ya mashabiki wa soka wa
England bila ya kujali ni wa timu gani wamesema wamekuwa wakishindwa kujumuika
na familia zao siku za wikiendi hasa wanapokuwa na ‘mtoko’ kwa kuwa lazima
wafuatilie mechi za soka.
Lakini asilimia 52, wamekuwa
wakijitahidi kula kwa mpangilio licha ya kuingia katika mechi za soka, lakini
haohao asilimia 40 wamesema wanaathirika kwa kushindwa kufanya mazoezi kwa kuwa
lazima wafuatilie Ligi Kuu England.
0 COMMENTS:
Post a Comment