September 27, 2013




Na Saleh Ally
Uhamisho wa wachezaji wawili, Neymar kutoka Santos ya Brazil kwenda Barcelona na Gareth Bale kutua Madrid akitokea Tottenham, ndiyo umekuwa gumzo zaidi duniani.

Wachezaji hao wawili walikuwa nyota na tegemeo katika timu zao na walipojiunga na Real Madrid na Barcelona walikutana na magwiji wa timu hizo, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.


Wengi walikuwa wanajiuliza namna ambavyo wangeweza kucheza pamoja au wangeweza vipi kutamba zaidi ya wakali hao ambao wamekuwa wachezaji nyota zaidi si katika La Liga pekee, bali duniani kote.

Bale amekuwa gumzo zaidi kutokana na kuweka rekodi ya uhamisho wa pauni milioni 86 (Sh bilioni 224), ndiye mchezaji ghali zaidi duniani. Lakini pamoja na kwamba Neymar alilipiwa pauni milioni 50 ambayo ni zaidi ya Sh bilioni 130 (kutua Barca ambazo si haba, wengi walisubiri ligi itakapoanza.


Watalaamu kadhaa wakiwemo makocha wa zamani walisema ingekuwa vigumu kwa Neymar kucheza na Messi na kung’ara, lakini kuna ambao walisisitiza angeweza na kwa pamoja watafanya vizuri.

Kwa upande wa Ronaldo na Bale, ilionekana wangeweza kufanya kazi pamoja lakini swali lilikuwa hivi: Kati ya wawili hao nani atang’ara zaidi ya mwenzake?

Suala la nani atakuwa zaidi hata kwa upande wa Messi na Neymar lilichukua nafasi, wengi walichambua na kusisitiza Neymar atachukua nafasi kubwa na kuiongoza Barcelona huku ‘mwenyeji’ wake akiporomoka.

Tayari mechi sita kwa kila timu za La Liga zimeishachezwa, uchambuzi na mawazo yaliyotolewa yanaonekana ‘kukosea njia’ kwa kuwa wenyeji Messi na Ronaldo wanaonyesha wao ndiyo wenye ‘nchi’.

Wanaendelea kufanya vizuri zaidi huku Bale na Neymar wakijikongoja kwa dalili ambayo si mbaya, kwamba wana uwezo wa kufanya vizuri, lakini bado wanahitaji muda kwa kuwa La Liga ina wenyewe. 

Mechi sita pekee zinaweza kuwa chache lakini takwimu ndizo zinazoonyesha yupi ni mkali kati ya wenyeji na wageni.

Inawezekana mechi sita zikawa ni chache, huenda wageni wakageuka baadaye, lakini hakuna ubishi, biashara ni asubuhi na kama wameanza hivyo, basi watafika mbali zaidi.

Messi anaongoza katika ufungaji mabao akiwa na saba, Ronaldo anafuatia akiwa na sita na Neymar na Bale kila mmoja wao ana bao moja tu.
Ingawa Bale anaweza kusema hajapata nafasi ya kucheza mechi nyingi kutokana na kuwa majeruhi lakini ukweli unabaki palepale, ana bao moja.
Kitu kingine utaona ni idadi ya mashuti waliyopiga langoni, wanapishana kwa idadi kubwa. Mwenyeji Messi amepiga langoni mashuti 32 wakati mgeni wake Neymar amepiga 15 tu. Ronaldo ana mashuti 48 na Bale mawili tu.
Hali halisi inaonyesha wageni hao yaani Neymar na Bale wanahitaji nguvu na juhudi kuhakikisha wanakuwa washindani sahihi. Angalia takwimu za wanne hao baada ya La Liga kufikisha mechi sita, Barcelona ikiwa kileleni, ikifuatiwa na Atletico Madrid na Real Madrid.
Ukizungumzia kasi ya mabao timu zote mbili zinaonyesha kuwa kwenye kasi lakini Barcelona ndiyo ambayo imekuwa juu zaidi, kwani mpaka sasa imefunga mabao 22 na kufungwa matano wakati Madrid wamefunga 14 na kufungwa sita. Hiyo inaonyesha kazi imeanza kwa mwendo mkali kama ambavyo imekuwa ikifanyika misimu ya hivi karibuni.

  • MESSI
MECHI
  MABAO
  PASI
    MASHUTI
    5
       7
     3
         32

  • NEYMAR
MECHI
  MABAO
  PASI
    MASHUTI
6
    1
    4
     15

  • RONALDO
MECHI
  MABAO
  PASI
    MASHUTI




     6
      6
     1
         48









  • BALE
MECHI
  MABAO
  PASI
    MASHUTI




     1
       1
      0
           2










0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic