September 27, 2013





Na Saleh Ally
Hapa nyumbani, rekodi zinaonyesha soka ndiyo biashara kubwa kuliko nyingine yoyote ile kama utapiga hesabu za mapato ya siku moja.

Inawezekana kabisa, kama kuna biashara inaizidi soka basi itakuwa ni ile ya madini na kama tutajumlisha suala la upatikanaji wake, soka itaendelea kuwa biashara kubwa na yenye faida ya juu zaidi, nitatoa mfano.

Miaka michache iliyopita wakati wa mechi za kwanza za ufunguzi wa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, timu ya taifa, Taifa Stars ilicheza na mapato katika mechi hiyo yakafikia hadi Sh milioni 600.


Unaweza ukatumia mfumo wowote, lakini fedha hizo zilitengenezwa katika mchezo wa saa moja na nusu tu kwa kuwa mashabiki waliofika uwanjani walitaka kushuhudia mchezo kwa saa moja na nusu pekee.

Hakuna mechi nyingine ambayo imewahi kuingiza mapato zaidi ya hayo ukilinganisha na ile ya Yanga dhidi ya Simba ambayo iliingiza Sh milioni 500 na ushee, halafu mapato hayo yakaendelea kuporomoka kila kukicha.

Mapato ya Uwanja wa Taifa yamekuwa yakizidi kuporomoka kila siku zinavyosonga mbele, hali inayoonyesha kuwa wale wanaohusika na usimamizi, sasa wameishajua namna ya ‘kuchukua’ mamilioni yanayopatikana kupitia mechi zinazochezwa.

Hakuna sehemu rahisi kuiba mamilioni kama katika mchezo wa soka kwa kuwa mfumo wake mbovu ndiyo unajenga magugu yanayowalinda wezi.

Ukiangalia hapa, utaona mchezo wa soka unavyokwenda nchini ni kwamba unawafaidisha kwa kiasi kikubwa wale ambao hawavuji jasho, badala yake wajanja ambao wamekaa pembeni.

Viongozi:
Ndani ya klabu hasa za Yanga na Simba ambazo zinaingiza mapato makubwa, kuna viongozi ambao wamekuwa wakishiriki katika masuala ya kuhujumu mapato na mara kadhaa wameingia katika tuhuma na wakati mwingine ikaonekana kila kitu kipo wazi, lakini ‘kubebana’ kunachukua nafasi na hakuna aliyeshitakiwa.

Utaona mapato yanahujumiwa, lakini hali halisi ni kwamba wahujumu wanafanya kazi pamoja na baadhi ya viongozi wa klabu hizo ambao wanakuwa wanawahujumu viongozi wenye nia nzuri.

Anayekataa inawezekana atakuwa ni mhusika, lakini viongozi wanaofanya hujuma hiyo wametengeneza mtandao mkubwa ambao ikitokea kiongozi anataka kuwazuia basi wanamtengenezea zengwe na siku ya mwisho anaonekana ndiye anaihujumu klabu.

Viongozi hao wameugeuza mchezo wa soka wa Tanzania kuwa mradi na hakuna ubishi kuwa wanawanyoya wachezaji na viongozi wakweli ambao wanavuja jasho kuufanya mchezo huo uende kwa mafanikio.

Hawana tofauti na magaidi wanaowalipua raia wema kwa faida zao, hawa wanawalipua wanaolipa viingilio wakijua fedha zao zinatumika kuendeleza mchezo wa soka.

TFF:
Ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumekuwa na watu ambao si waaminifu, wanahusika na uhujumu wa mapato na kuna wakati fulani kuna viongozi na maofisa wake waliwahi kuhusishwa na wizi.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwamba ndani ya shirikisho hilo, tena tokea likijulikana kama Chama cha Soka Tanzania (Fat), kumekuwa na kundi linalofanya kazi za uhujumu wa mapato kwa ajili ya faida ya wachache na si soka kwa jumla.

Vigumu kuwataja majina kwa kuwa ‘mchezo’ wenyewe unafanywa kama shughuli za uzinzi, kunakuwa na siri kubwa. Lakini hakuna ubishi, watu hao wanajulikana na wamekuwa wakiendelea na kazi zao za wizi wa mapato kwenye kila mechi.

Viongozi hao kuhofia kuchafuka, wamewatanguliza watu fulani ambao wamekuwa wakifanya kazi hiyo kama wawakilishi wao. Wengine ni magwiji na wanajulikana kwa kazi hiyo.

Rais wa TFF, Leodeger Tenga hata kama anamaliza muda wake lazima anajua kuna walakini katika suala la mapato. Alishughulikie kwa kuwa soka haikui bila ya fedha na kama fedha inaingia na kubaki mikononi mwa wachache, basi ni tatizo.

Ndiyo maana nasema hilo analijua na anapaswa kulikemea, akikaa kimya maana yake tuingie hofu kwamba huenda anaulea huo mtandao!

Adui anayeweza kukumaliza kirahisi ni yule unayemwamini, uliye karibu naye. Wapenda soka wanawaamini viongozi wa klabu na TFF, pia askari wanaolinda. Lakini wao wanaimaliza soka wanavyotaka kwa kuwa wanaaminiwa.

Jeshi la Polisi:
Wako askari polisi ambao si waaminifu, inawezekana wanashiriki moja kwa moja lakini mara nyingi tu nimewashuhudia wakihusika na kuingiza watu na wao kuchukua fedha kwa faida yao.

Inawezekana hawa wasiwe katika mtandao lakini wakawa wanahusika moja kwa moja kwa kuwa wana nafasi ya kukaa milangoni au sehemu fulani ambazo watu wanaweza wakapita.

Wakati mwingine wanashirikiana na watu kadhaa wasio waaminifu kutoka katika makampuni ya ulinzi ambao pia wanahusika na uhujumu wa mapato.

Mtandao wa wizi wa mapato, wahujumu wa mchezo wa soka ni mkubwa na una nguvu sana. Huenda watu wengi wanawahofia watu hawa kwa kuwa wana nguvu kifedha na hata kwa kuwa na majina makubwa.

Pia, inaonekana hivi, Mtanzania anayesimamia kuzipigania fedha za soka ni sawa na kiherehere kwa kuwa hazimhusu na zinaonekana hazina mwenyewe na kila mmoja anaweza kuchota.

Lakini hali halisi iko hivi, lazima wenye nafasi ya kuzungumza tufanye kazi ikiwezekana kuwaanika wezi na wanyonyaji hao ambao wanauumiza mpira wa Tanzania, ndiyo maana wachezaji wengi hadi wanastaafu wanakuwa hawana kitu na maisha yao ni magumu wakati walistahili kuishi maisha mazuri baada ya kustaafu.

Kama fedha zingekuwa zinapatikana kwa wingi zaidi, klabu zikapata fedha nyingi zaidi. Maana yake wachezaji wangelipwa vizuri zaidi na huenda hata mazingira ya kazi kama viwanja, sehemu za kuishi zingeboreshwa zaidi.

Sasa mambo ni tofauti, hayaendi vizuri kwa kuwa fedha nyingi zinapotelewa kwenye mikono ya wajanja wachache ambao wakati mwingine Yanga au Simba zikifungwa wanalia kwa kisingizio wanazipenda, kumbe ni unafiki tu. Wanalilia mapato ambayo wanajua yatapungua, mapenzi ya kinafiki.

Binafsi hakuna ninayemhofia kwa kuwa sivunji sheria, najua nawaudhi lakini kilio changu ni faida ya wachache. Nasisitiza umefika wakati wa kukata mirija ya wanyonyaji hawa na kuingiza nguvu nyingi katika kuhakikisha mapato ya soka yanakua.

Makundi ya wanyoyaji yanayoongozwa na baadhi viongozi wa klabu, TFF, askari wasio waaminifu yanaweza kufikia tamati. Kama fedha nyingi au faida inayopatikana kutokana na viingilio basi iende kwa wahusika zaidi, wachezaji wasiendelee kustaafu na kufa masikini na wanaotajirika ni matajiri.

Nawaita matajiri kwa kuwa wengi wao wana uwezo kifedha, lakini wanaiba fedha nyingi zinazotolewa na wenye uwezo wa chini zaidi. Wengi wanaokwenda uwanjani ni wale wanaochangisha fedha zao kidogokidogo ili wapate angalau nafasi ya kuona mechi moja kwa wiki.

Wanapotoa fedha hizo, pamoja na kupata burudani wanajua wanacholipa kinasaidia maendeleo ya mchezo huo ili waendelee kuburudika. Sasa matajiri wanazidi kuchota fedha zaidi na kujilimbikizia huku mchezo wa soka ukizidi ‘kukonda’ kutokana na kukabiliwa na umasikini.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic