Hakuna ubishi Ligi Kuu Tanzania Bara ni ngumu zaidi kama utalinganisha
na nyingine katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Inawezekana kukawa na upinzani mkali kutoka DR Congo, lakini hakuna
ligi inayoweza kulinganishwa na ile ya Tanzania Bara hasa kutoka Burundi,
Rwanda, Uganda na hata Kenya ambako ninaweza kusema kuna angalau nafuu kidogo.
Inawezekana kabisa pamoja na utajiri wa baadhi ya timu kama Yanga,
Simba, Azam FC, Coastal Union na nyingine, bado kuna changamoto inayopatikana
na inazidi kuongeza ugumu katika ligi hiyo ya hapa nyumbani.
Katika ligi hiyo yenye timu 14, sita kati yake ni za jeshi ambazo ni
JKT Ruvu, Ruvu Shooting, JKT Oljoro, Mgambo JKT, Prisons na Rhino Rangers.
Kama asilimia zaidi ya 40 ni timu za jeshi, hakuna ubishi ndiyo
zinazoongeza ugumu wa ligi hiyo kama sehemu ya changamoto kubwa kutokana na
ubora wa timu hizo.
Hakuna ubishi timu hizo zimekuwa zikitoa changamoto kubwa ya ushindani
kutokana na zinavyocheza na mara nyingi zinazitoa jasho timu vigogo kwa kuwa
hulazimika kufanya kazi ya ziada kupata ushindi.
Mfano Yanga, Simba, Azam FC au Coastal Union zinatambua ugumu
zinapokutana na timu za jeshi kwamba si lelemama na hulazimika kufanya
maandalizi ya kutosha ili kuhakikisha zinashinda dhidi ya timu hizo.
Hata kama watakuwa hawachezi soka la kuvutia sana, timu hizo za
majeshi zimekuwa fiti sana na zinaongeza ugumu wa ligi hiyo kwa kuwa imekuwa ni
ligi ya wanaume kweli.
Pamoja na yote hayo, ninachotaka kuweka sawa ni namna ambavyo imekuwa
karibu kila msimu ambapo huanza kwa timu za jeshi kuongoza na baada ya hapo
zinaporomoka taratibu.
Siamini kwamba timu hizo za jeshi zinaporomoka na kupoteza mwelekeo
kutokana na kushindwa kuvumilia mikiki ya ligi kwa maana ya uwezo wa mazoezi ya
kutosha au uwezo wa kucheza soka.
Lazima kutakuwa na kasoro nyingine ambazo ni suala la fitna za soka,
pia sumu ya Uyanga na Usimba kuingizwa ndani ya timu hizo.
Ushabiki wa kupindukia wa timu hizo mbili ni sehemu ya sumu inayofanya
maendeleo ya soka nchini kutokuwa na kasi sahihi. Wako ambao hawakubali tena
timu hizo za jeshi zishinde kwa kuwa tu zinacheza na Yanga au Simba. Hili si sahihi!
Najua ushabiki ulivyo na nafasi, lakini si sahihi kushambulia paa la
kibanda unachoishi ili umfurahishe jirani aweze kuwachungulia mnapokuwa mmelala.
Sumu hiyo itupiwe jicho na iepukwe.
Timu za jeshi hazisumbuki kwa njaa ya chakula wala kambi kwani kila
kitu kinapatikana. Maana yake zinapata matunzo ya kutosha na kuna uwezekano wa
kufanya vizuri zaidi, kwani hata kama mishahara yao haitakuwa mikubwa sana, kamwe haichelewi au kuzungushwa.
Hii ni sehemu ya kuonyesha timu hizo zina kila sababu ya kufanya
vizuri zaidi ya ilivyozoeleka. Lakini kwa wale wanaopenda Yanga au Simba halafu
ni waajiriwa wa timu hizo, lazima watazame mbele zaidi kwamba ofisi yao ni
moja, ushabiki unafuatia.
Inawezekana ukaishi bila ya kuwa shabiki wa Yanga au Simba na unaweza
kuchangia maendeleo ya soka nchini bila ya kuzishabikia timu hizo. Wako
wanaoshabikia kwa kufuata mkumbo au imani kuwa lazima uwe shabiki wa njano au
nyekundu. Ukweli ni kwamba mambo
yanakwenda yanabadilika.
Kwa hiyo, walio ndani ya timu za jeshi, wasiue juhudi za wengine kwa makusudi ili kuridhisha nafsi
zao. Wako ambao wanakubali kuwa ‘watumwa’ na kumaliza juhudi za wengine wanaotaka
mafanikio ya timu hizo. Hivyo fanyeni kweli kusaidia kuwepo kwa ushindani
mkubwa zaidi.
Ushindani ukiwa ni wa dhati na wa juu, utasaidia hata bingwa
anayepatikana kuwa imara atakapokwenda kwenye michuano ya Afrika badala ya kuwa
na bingwa aliyepita ‘kimagumashi’ ambapo anakwama katika raundi za awali.
FIN.
0 COMMENTS:
Post a Comment