Na Mwandishi Wetu
Mmoja wa makocha bora wa soka wazalendo,
Juma Mwambusi, ameeleza kuumizwa na tabia aliyoionyesha kiungo nyota wa Coastal
Union, Haruna Moshi ‘Boban’.
Mwambusi ambaye amekuwa akifanya vizuri
na kikosi cha Mbeya City, amesema alishangazwa kuona Boban akimshambulia kwa
maneno makali mwamuzi msaidizi, Hamis Chang’walu wakati walipocheza na Coastal
Union juzi na kutoka sare ya bao 1-1 jijini Mbeya.
“Kweli nilisikia Boban akizungumza
maneno ambayo si mazuri kwenye mchezo kwa kuwa ilikuwa karibu kabisa na
nilipokuwa.
“Ninaamini Boban ni mchezaji bora ambaye
hata mimi au kocha mwingine anaweza kutamani kumjumuisha katika kikosi chake.
Tumekuwa tukisikia kwenye vyombo vya habari kwamba amebadilika sana.
“Lakini alichokifanya hakikuwa sahihi,
unajua alikasirishwa na Chang’walu kuinua kibendera cha kuonyesha ameotea,
alichofanya Boban alijaribu kuepuka ‘offside’ lakini ikashindikana. Hapo ndiyo
ukaanza mzozo naye akafanya alichofanya,” alisema Mwambusi.
“Si kwamba ninataka kumsakama, lengo ni
kutoa ushauri kwamba waamuzi wakati mwingine wanaudhi sana. Mfano mimi nimeona
mara tatu tulistahili kupata penalti lakini sikumtukana mwamuzi au kusema
maneno machafu.
“Lakini ajifunze, kama amebadilika iwe
kweli na ikiwezekana basi wajitokeze watu wamsaidie, wamshauri tena na tena,”
aliongeza.
Katika mechi hiyo, kabla ya kulambwa
kadi nyekundu, Boban ndiye aliifungia Coastal Union bao na ‘wabishi’ Mbeya City
wakasawazisha.
0 COMMENTS:
Post a Comment