HII ni kali na ya aina yake, kila pasi ya
mwisho na bao atakalofunga kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Khalfan Ngassa,
litanunuliwa.
Milionea Davis Mosha aliyewahi kuwa
makamu mwenyekiti wa Yanga, ameamua kutangaza ofa hiyo kwa Ngassa kila
atakapofunga akiichezea timu hiyo.
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa, Mosha
tayari amemueleza Ngassa kuhusiana na ofa yake hiyo.
“Unajua katika mechi mbili dhidi ya Ruvu
Shooting na Mtibwa Sugar, Ngassa amefunga bao moja na kutoa pasi mbili. Davis
ameshalipia zote,” kilieleza chanzo na kufafanua zaidi:
“Bao moja amemlipa shilingi milioni moja
na pasi pia amelipa, sijui ni kiasi gani lakini nimeambiwa ni shilingi laki
tano.”
Taarifa zaidi zimeeleza kuwa, pamoja na
Mosha kununua mabao hayo, pia amemtaka Ngassa kuhakikisha anasaidia kupatikana
kwa mabao mengine katika timu hiyo, akisisitiza ataendelea kununua pasi
zilizozaa mabao.
“Unajua Mosha alichangia kwa kiasi
kikubwa kumrudisha Ngassa Yanga, wakati akiwa Azam na hata Simba kwa kumtaka
akipata nafasi ya kutakiwa kurudi Yanga asifanye makosa,” alisema mmoja wa watu
wa karibu na Mosha.
Ngassa, ambaye alikiri kuwepo kwa taarifa hizo huku
akiongeza zaidi kuwa, hata bao alilolifunga juzi dhidi ya Mtibwa, alimpa zawadi
Mosha ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake.
“Ni kweli hizo taarifa ni sahihi,
natambua sana mchango wa Mosha kwangu, tunazungumza mengi lakini naweza kusema
anachangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ninayoyapata katika klabu yangu ya
Yanga.
“Kila ninapofunga au kutoa pasi ananipa
fedha, hiyo ndiyo sababu inayonifanya nijitume kwa kufanya mazoezi mara mbili
mpaka tatu kwa siku ili niwe fiti,” alisema Ngassa.
Kama vile haitoshi, Ngassa juzi alivaa
kiatu cha kisasa aina ya Nike Hypervenom Phantom (FG), kinachotumiwa na
kutangazwa na wachezaji nyota duniani kama Mario Balotelli wa AC Milan, Wayne
Rooney (Man United), Gonzalo Higuain (Napoli) na Neymar wa FC Barcelona.
Kiatu hicho ambacho ni toleo jipya la
Nike mwaka 2013, Ngassa alikipata kutoka Uingereza ikiwa ni zawadi kutoka kwa
rafiki yake.
“Kweli ndicho nilivaa katika mechi dhidi
ya Mtibwa Sugar, rafiki yangu alisafiri kwenda Uingereza nikamuomba aniletee,”
alisema Ngassa.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment