Rhys Torrington |
Na Saleh
Ally
Gumzo Azam TV limekuwa likipanda kila siku, taarifa za kuanza kwake na mgogoro wake
na Yanga kuhusiana na kuonyesha Ligi Kuu Bara pia ni mambo yanayochukua nafasi
kubwa miongoni mwa mashabiki wa michezo, hasa soka.
Championi
Jumatano liliamua kupiga hodi hadi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media, Rhys
Torrington ambaye anaelezea mambo kadhaa kuhusiana na mgogoro huo, pia mipango
kamili ya Azam TV.
Torrington,
raia wa Uingereza, anasema mgogoro wa Yanga anauona unakwenda kisiasa zaidi,
kitu ambacho anaona si sahihi, akitolea mfano suala la watu waliojiita
mashabiki wa Yanga kutaka kuwashambulia wapigapicha wa Azam TV wakiwazuia
kuonyesha ‘live’ wakati Yanga ikicheza na Mtibwa, Jumapili.
Mgogoro na
Yanga:
Kweli si
kitu kikubwa sana, lakini limekuwa jambo ambalo linakuzwa sana na kuna wakati
nafikiri ule upinzani mkubwa kati ya Yanga na Azam FC katika soka ndiyo
unaosababisha mambo haya.
Lakini kitu
kizuri sisi tumefuata utaratibu unaotakiwa na tumeingia mikataba sahihi na tuna
haki ya kufanya kazi zetu. Ila kwa usalama wa watu wetu, tuliamua kusitisha
kuonyesha mpira.
Angalia,
katika mechi ya kwanza ilikuwa Simba na Ruvu Shooting, tulionyesha kipindi cha
pili tu. Hii ilitokana na makosa ya kibinadamu, kuna mtu alisahau kuchomeka
waya, hivyo hatukuwa hewani.
Mechi ya
Yanga na Mtibwa Sugar, tulijipanga kuanzia kipindi cha kwanza, ikashindikana
kutokana na hizo vurugu hadi askari walipoingia.
Kiungwana
kabisa nahisi hao ni watu wanaojidai mashabiki wa Yanga. Siamini mashabiki wa
kweli wanaweza kufanya hivyo na ingekuwa vizuri kama uongozi wa Yanga ungekemea
ili kuepuka kuchafuliwa.
Lini
mtaanza?
Kwa sasa
tumeingia mkataba wa kirafiki na TBC1, itakuwa kila Jumamosi na Jumapili na wao
wataendelea kuonyesha hadi mwisho wa mzunguko wa kwanza, baada ya hapo kila
kitu kitarudi kwetu.
Ila sisi
tutaanza rasmi Novemba Mosi, itakuwa kabla ya mzunguko wa kwanza kuisha. Maana
yake sisi na TBC1 wote tutaonyesha. Halafu watatuachia wenyewe baada ya kuanza
mzunguko wa pili kama nilivyosema.
Tayari kuna
watu wameshaanza mazoezi ya mambo lukuki hapa, tuna wataalamu kutoka Ujerumani
na Afrika Kusini wanaotoa mafunzo kwa watu wetu. Mfano tuna magari mawili ya OB
Van, dogo litatumika kwa viwanja vidogo na kubwa Uwanja wa Taifa.
Yote hayo
yanahitaji utaalamu na si kitu kidogo, hivyo wataalamu hao wanaendelea kufanya
kazi kuhakikisha mambo yako sawa.
Visimbuzi:
Kweli
tutatumia visimbuzi ambavyo vinatarajiwa kuwa na chaneli takribani 50, mfano
Azam1 itaonekana na lugha ni Kiswahili, chaneli hii ndiyo itakayoonyesha soka
na zaidi ni Ligi Kuu Tanzania Bara.
Lakini Azam2
itakuwa ni Kiingereza, kawaida tutatumia maandishi kama yale ya Zuku au Dstv,
ukilipa kwa mara ya kwanza kunakuwa na chaji kidogo ya fundi.
Kutakuwa na
filamu za sehemu mbalimbali duniani pamoja na zile za Kitanzania. Lakini kuna
chaneli mbalimbali za hapa nyumbani kama Mlimani TV, Clouds TV na TBC1.
ITV vipi?
Hawa ITV
wamekataa katakata kuingia katika kisimbuzi chetu na kutupa haki ili waonekane
kama wengine. Hivyo hatutakuwa nao lakini tunaamini mambo yataendelea vizuri
tu.
Bei ya
Visimbuzi:
Kweli sasa
itakuwa ni siri, ila nakuhakikishia itakuwa ni ile anayoweza kuihimili
mwananchi yeyote. Visimbuzi vyetu havina madaraja ya matajiri na masikini, bei
itakuwa ni moja ili kila mmoja aweze kununua.
Kuna
mawakala 200 kwa nchi nzima ambao watafanya kazi ya kuuza visimbuzi vyetu na hii
ni kutaka kuhakikisha kila mtu anapata.
Visimbuzi vyetu ni kati ya vilivyo bora
kabisa, vinatumia mfumo wa HD na unaweza kurekodi kwa kutumia USB Flash.
Mwisho si
Tanzania:
Tunataka
kuanza na nyumbani kwanza na baada ya hapo tutaendelea kunajitanua hatua kwa
hatua, tutaanzia na Uganda na baadaye Kenya na ikiwezekana hadi mwisho wa mwaka
huu tutakuwa tumeingia sehemu hizi mbili.
Baada ya
hapo, ninaamini itakuwa ni mwakani tutavuka taratibu hadi Rwanda, Burundi na
ikiwezekana Malawi na tunaweza kutulia na kujiimarisha zaidi kabla ya kwenda
Afrika Magharibi, hii ni mipango ya hapo baadaye.
Fin.
0 COMMENTS:
Post a Comment