Na Saleh Ally
Keshokutwa Jumapili litapatikana jibu la
nani mbabe katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara ambayo itawakutanisha watani
wa jadi, msimu huu.
Simba watakuwa wenyeji wa Yanga, kila upande
utakuwa unacheza mechi yake ya tisa ya ligi hiyo msimu huu, huku mabingwa
watetezi wakionekana kupania kupanda na Simba kutaka kujichimbia zaidi
kileleni.
Simba ina pointi 18 kileleni wakati Yanga
ina 15 katika nafasi ya nne, iwapo Simba itateleza basi zitalingana pointi.
Takwimu zinaonyesha Simba inafanya vizuri
zaidi hadi sasa lakini zile za uzoefu wa mechi za watani, Yanga wanaonekana
kuwa na kikosi imara zaidi. Inaonyesha lazima ‘mtu atakaa’, lakini si rahisi
kung’amua ni yupi.
Safu ya ulinzi:
Safu ya ulinzi ya Yanga inaonekana ni
maarufu na kubwa zaidi kwa maana ya kuwa na wachezaji wazoefu zaidi na
waliocheza pamoja kwa kipindi kirefu, mfano Athumani Iddi ‘Chuji’, Kelvin
Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Uzoefu wa Mbuyu Twite na ubora wa David
Luhende lakini ndiyo imeruhusu mabao nane katika mechi nane ikiwa ni wastani wa
kufungwa bao moja kila mechi wakati safu ya ulinzi ya Simba imeruhusu mabao
matano.
Tofauti ya mabao matatu ni kubwa na
inaonekana Joseph Owino na Gilbert Kaze ‘Demunga’ wanaanza kuelewana kiasi
fulani ingawa kumekuwa na makosa mengi mara kadhaa. Hakuna ubishi, Simba
watalazimika kumrudisha Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ upande wa kushoto kwa kuwa
kumeyumba.
Kiungo:
Kila upande kuna viungo bora, lakini kwa
Yanga ni wazoefu zaidi, hasa Chuji au Frank Domayo kwenye ulinzi, Haruna
Niyonzima katika ushambuliaji. Hata hivyo bado hawajatengeneza mambo bora zaidi
katika mechi nane za mwanzo.
Kwa upande wa Simba inaonekana Jonas Mkude
amekaa vizuri katika namba sita, lakini namba nane bado haijapata mwenyewe,
kwani wakati mwingine Abdulhalim Humud au kinda mwenye kipaji, Said Ndemla, ambaye hata
hivyo anabadilishwa mara kwa mara, lazima wajipange.
Kwa pembeni, Yanga wana watu wenye kasi kama
Simon Msuva na Kocha Ernie Brandts kama ataamua kumchezesha Mrisho Ngassa
pembeni. Lakini Simba pia wako sawa, Haruna Chanongo ni hatari na ana uwezo wa
kupiga mashuti makali na kulia ni Amri Kiemba au Ramadhani Singano ingawa bado
haina uhakika nani ataanza.
Washambuliaji:
Kwa takwimu, safu ya ulinzi ya Simba ni kali
zaidi kwa kuwa ina mabao 18, mengi zaidi ya Yanga yenye 15 na tegemeo ni
Mrundi, Amissi Tambwe, aliyefunga manane na wamepanga kumbana vilivyo.
Betram Mwombeki wa Simba na Didier Kavumbagu
wa Yanga watakuwa kivutio na tatizo kwa mabeki, lakini kasi ya Ngassa, ujanja
wa Tambwe ni mambo muhimu ya kuangalia na yatawasumbua walinzi wa kila upande.
Mechi nne za mwisho:
SIMBA:- Katika mechi zake nne za mwisho,
Simba ilikusanya pointi nane baada ya kushinda mechi mbili dhidi ya Prisons na
JKT Ruvu na sare mbili dhidi ya Ruvu Shooting na Mbeya City. Prisons 1-0, Ruvu
Shooting 1-1, JKT 2-0, Mbeya City 2-2.
YANGA:-Katika mechi nne za mwisho, Yanga
walipata pointi tisa baada ya kufungwa moja dhidi ya Azam FC na kushinda tatu
dhidi ya Kagera, Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting.
Kagera 2-1, Mtibwa 2-0, Ruvu Shooting 1-0,
Azam 2-3.
Uzoefu:
Hiki ndicho kikosi Yanga wanaweza kujivunia
zaidi, kwani wana kikosi kilichokaa pamoja kwa muda mrefu zaidi na wameshacheza
mechi dhidi ya Simba zaidi ya mara mbili.
Upande wa Simba ni kikosi ambacho wachezaji
wengi wanacheza kwa mara ya kwanza dhidi ya Yanga wakiwa na Simba. Hivyo
kutakuwa na ugumu kwao lakini bado haliwezi kuwa tatizo la moja kwa moja kama
watajituma.
Takwimu ni kitu bora kupima kilichotokea,
lakini bado dakika 90 ya kila mechi hujitegemea ili kutengeneza takwimu mpya.
Hivyo itakuwa mechi ngumu ambayo ni vigumu kutabiri mshindi.
Wenye mabao:
Simba:-Wachezaji wenye uchu wa mabao ambao
hakuna ubishi wataipa Yanga shida ni Tambwe ambaye tayari ana mabao nane na ndiye
anaongoza kwa upachikaji mabao hadi sasa.
Chanongo tayari ana mabao matatu, atataka
kuongeza la nne na kuifunga Yanga ni kitu bora kwake, hivyo atakuwa mwiba.
Jonas Mkude, ndiye kiungo mkabaji mwenye
mabao mengi zaidi msimu huu, ana matatu. Moja la penalti lakini bao moja
alilofunga dhidi ya Prisons hadi sasa ndilo bora zaidi na Kocha wa Taifa Stars,
Kim Poulsen amesema hata Ulaya linapatikana kwa shida.
Yanga:- Kavumbagu ndiye anaongoza mabao
Yanga, ana manne na uchu wake uko juu ingawa ana tatizo la kushindwa kumalizia
jirani ya lango.
Hamisi Kiiza, huyu ni hatari zaidi kwa
Simba, mechi ya mwisho alifunga bao zuri katika ya msitu wa mabeki wa Simba,
sasa ana mabao matatu.
Jerry Tegete anaweza asianze, lakini akipata
nafasi pia ni tatizo kwa Simba hasa kwa kuwa wana makosa ya kujisahau kuondosha
mipira haraka langoni mwao au kipa Abel Dhaira kutema mara kwa mara.
Vichwa:
Vichwa viwili vinaweza kuwa ni vya kuchungwa
zaidi, Mwombeki ambaye ni mrefu, akipewa nafasi ya kutoa pasi za vichwa itakuwa
ni tatizo kwa Yanga na Tambwe anaweza kuitumia nafasi hiyo kuwamaliza.
Kavumbagu, mzuri kwa pasi za vichwa pia
kumalizia langoni mipira ya juu, Simba wanamkumbuka walipolala mabao 2-0. Hivyo
lazima kuwe na mwenye uwezo wa kuruka naye juu.
Ligi Kuu Bara
P W D L Pts
1. Simba 8 5 3 0 18
2. Azam 9 4 5 0 17
3. Mbeya City 9 4 5 0 17
4. Yanga 8 4 3 1 15
SIMBA
Kocha: Abdallah Kibaden
Kocha Msaidizi: Jamhuri Kihwelo ‘Julio’
Nahodha: Said Nassor ‘Chollo’
Kambi ilipo: Bamba Beach, Dar
YANGA
Kocha: Ernie Brandts
Kocha Msaidizi: Felix Minziro
Nahodha: Nadir Haroub ‘Cannavaro’
Kambi ilipo: Pemba, Zanzibar
0 COMMENTS:
Post a Comment