VALENCIA |
Na Saleh Ally
Mnyama mwenye kasi zaidi kuliko mwingine yoyote duniani ni chui aina ya Cheetah
ambaye anakimbia kasi ya maili 64 au kilomita 104 kwa saa ambayo ni mara mbili
na ushee zaidi ya binadamu mwenye kasi zaidi.
Binadamu mwenye kasi zaidi ni mwanariadha wa Jamaica, Usain Bolt, ambaye
ameweka rekodi ya kukimbia kilomita 37.58 kwa saa. Aliweka rekodi hiyo katika
mashindano ya ubingwa wa dunia hivi karibuni nchini Urusi.
Katika soka pia kuna watu wenye kasi kubwa na Shirikisho la Soka la
Kimataifa (Fifa), limetoa rekodi zake kuonyesha wachezaji gani wana kasi zaidi
ya wengine.
Winga au kiungo wa Manchester United, Antonio Valencia, ndiye aliyeshika nafasi hiyo kutokana na data
za wataalamu wanaofanya tathmini za shirikisho hilo kubwa zaidi la soka duniani.
Valencia ambaye hana sifa kubwa kwa mashabiki lakini amekuwa chachu kubwa
ya ushindi wa Manchester United inapocheza mechi zake, ana kasi ya kilomita
35.1 kwa saa. Ingawa hajamfikia Bolt, lakini hakuna mwanasoka mwingine
anayemfikia.
Gareth Bale ambaye ametua Real Madrid akitokea Tottenham anashika nafasi
ya pili akiwa na kasi ya kilomita 34.7 kwa saa na ndiye mchezaji mwenye kasi
zaidi katika La Liga.
Baada ya hapo ni winga mwenye kasi wa Tottenham, Aaron Lenon, ambaye ana
kasi ya kilomita 33.8 kwa saa akiwa amemzidi Cristiano Ronaldo kwa pointi mbili
tu.
Ronaldo aliyekuwa mchezaji mwenye kasi zaidi La Liga kabla ya kutua Bale,
anashika namba nne katika data hizo za Fifa akiwa na uwezo wa kukimbia kilomita
33.6 kwa saa na Theo Walcott wa Arsenal anafunga tano bora kwa mwendo wa
kilomita 32.7 kwa saa.
Tayari imezua mjadala mkubwa wengi wakiwa hawaamini kama kweli Valencia
ndiye mwenye kasi zaidi, lakini Fifa imeshikilia hilo huku ikitaka watu
wahakikishe kwa utaalamu na si maneno.
Premiership imekuwa ligi yenye wachezaji wengi zaidi wenye kasi duniani
kwa kuwa katika tano bora ina wachezaji watatu na kumi bora inao wanne wakati
La Liga inashika nafasi ya pili kwa kuwa na wawili tano bora na wanne kumi
bora.
Lakini Premiership inaonekana iko juu zaidi kwa kuwa hata wachezaji wenye
kasi zaidi wa La Liga ambao ni Bale na Ronaldo, wote wametokea England.
Bundesliga inashika nafasi ya tatu, haina mchezaji katika tano bora
lakini imeingiza Arjen Robben na Frank Ribery wanaoshika nafasi ya nane na
tisa. Ligi nyingine kubwa za Ufaransa na Italia, hazijaingiza mchezaji katika
hatua ya 10 bora.
Kingine ambacho kinavutia zaidi ni kwamba, 10 bora ya wenyewe inaonyesha
hivi, wote ni washambuliaji au viungo wa pembeni na hakuna beki.
Kama ni hivyo, vipi mabeki, na wanaweza vipi kuwadhibiti wasilete
madhara? Jibu lake ni hili, katika soka, kasi haiwezi kuwa kila kitu na kuna
mbinu na mambo mengi yanayotakiwa zaidi ya kasi pekee.
Kumi bora ya wenye mwendo kasi duniani:
1. Antonio Valencia (Manchester United) 35.1 km / h
2. Gareth Bale (Real Madrid) 34.7 km / h
3. Aaron Lennon (Tottenham Hotspur) 33.8 km / h
4. Cristiano Ronaldo (Real Madrid) 33.6 km / h
5. Theo Walcott (Arsenal FC) 32.7 km / h
6. Lionel Messi (FC Barcelona) 32.5 km / h
7. Wayne Rooney (Manchester United) 31.2 km / h
8. Franck Ribery (Bayern Munich) 30.7 km / h
9. Arjen Robben (Bayern Munich) 30.4 km / h
10. Alexis Sánchez (FC Barcelona) 30.1 km / h
0 COMMENTS:
Post a Comment