October 18, 2013






Na Ismail Aden Rage (Mb)
simbasportsclub@yahoo.com

“KAMA hujafanya utafiti, huna haki ya kuzungumza.”

Nimeanza na nukuu hiyo murua ya hayati Mwenyekiti Mao kuhusu mtu kuwa na haki ya kuzungumza au kuandika unapokuwa umelifanyia utafiti jambo.


Pasipo kufanya utafiti, mtu anakuwa sawa na ndege aina ya kasuku ambaye anachojua ni kuiga tu sauti anazozisikia. Hawezi kufanya utafiti wake. Mao hakutaka Wachina wawe makasuku. Hakutaka kutengeneza taifa la watu wanaobwabwaja tu.

Akiandika katika gazeti hili, toleo la Ijumaa Oktoba 11-13 mwaka huu, mwandishi Saleh Ally, aliandika maoni yake binafsi kupitia safu ya HOJA YANGU iliyokuwa na kichwa cha habari; “Fedha za Emmanuel Okwi ziondoke na kichwa cha mtu Simba.”

Kwa sababu kuna msemo maarufu wa Kiswahili unaoeleza kuwa mwiba hutolewa palepale ulipoingilia, naomba nami nitumie gazeti hili la CHAMPIONI (na Blogu ya Salehjembe), kutoa upande wangu wa maelezo.

Kwa maoni yangu, mwandishi hakuwa na hoja yoyote kwenye makala ile zaidi ya kuonyesha ukasuku wake. Nadhani jina ambalo lingefaa kwa safu hiyo ni ama “Kasuku” au “Ukasuku Wangu.” Nitaeleza.

Takribani mara tatu, kwenye makala hiyo moja,  mwandishi huyo ametumia neno “dalili” kujenga ‘hoja’ zake dhidi yangu binafsi na klabu ya Simba.

Dalili ya kwanza aliitumia akijenga hoja kwamba “Dalili zote Simba inaelekea kupata hasara ya Sh milioni 480.” Kwa maneno yake mwenyewe, Saleh amesema hasara hiyo imetokana na uamuzi wa Fifa kumuidhinisha Okwi aichezee Villa kwa miezi sita. Ameandika Saleh; “Hii ni dalili ya uthibitisho kwamba Simba haitapata fedha zake.”

Akaeleza biashara ya kumuuza Okwi kuwa ni kichaa na kwamba “Ni dalili ya kufungua ukumbi wa viongozi kutohofia makosa yao.”

Mhariri Kiongozi wa gazeti kubwa kama CHAMPIONI anajenga hoja zake kwa kutumia dalili. Kwa ninavyojua mimi, mwandishi wa habari mbobezi hujenga hoja zake kwa kutumia ‘facts’.

Kwa sababu Saleh hana facts, anaamua kutumia dalili kana kwamba yeye ni mganga wa kienyeji au mtu wa Idara ya Hali ya Hewa! Kwa niaba ya wasomaji wa gazeti hili, naomba sasa niweke facts hadharani.

Mosi, Simba ilimuuza Okwi kihalali kwa thamani hiyo ya dola 300,000 na yalikuwa ni mauzo yaliyoweka historia mpya hapa Afrika Mashariki.

Kiwango hicho cha fedha kilifikiwa kutokana na ustadi na uzoefu wangu mkubwa katika masuala ya majadiliano ya kuuza wachezaji. Kwa maslahi ya Simba na taifa, nilihakikisha klabu inapata fedha nyingi kwa kadri inavyowezekana.

Tangu lini biashara ya Sh milioni 480 ikawa kichaa? Kiwango hiki ni zaidi ya mara 15 ya gharama ambazo Simba ilizitumia kumsajili Okwi. Ningemuona Saleh ana hoja endapo angenipa mfano wa biashara yoyote ambayo kitu ulichokinunua kwa Sh 1,000, unakiuza kwa Sh 15,000 na bado ikafuzu kuitwa kichaa.

Nilikwenda Tunisia kuzungumza na Etoile du Sahel (ESS) si kwa sababu za kibinafsi. Nilitumwa na Kamati ya Utendaji ya Simba SC kumalizia suala hilo kama ambavyo ilinituma pia kukamilisha usajili wa Gervais Kago na Amissi Tambwe.

Hivyo, uamuzi wa Simba kumuuza Okwi kwa ESS haukuwa wa Ismail Aden Rage bali wa Kamati ya Utendaji nzima na mimi nilitumwa tu kufanikisha suala hilo.

Ifahamike pia kwamba Simba si klabu pekee ambayo inaidai ESS katika siku za karibuni. Miezi miwili iliyopita, Fifa iliamua mzozo uliokuwepo baina ya klabu hiyo na wakala wa kimataifa wa Senegal, Mamadou Cheriff, kuhusiana na mauzo ya mchezaji kutoka Ghana, Uriah Asante.

Mchezaji huyo sasa amepelekwa kwa mkopo nchini Romania na alisajiliwa miezi michache kabla ya Okwi. Kama Saleh angeamua kufanya utafiti walau kidogo tu, angejua kila kitu !

Ukweli uliopo ni kwamba ESS iko katika matatizo ya kifedha kwa sasa. Hata hivyo, hii ni timu ambayo miezi michache kabla haijaingia kwenye matatizo yake, ilikuwa imetoka kusajili mchezaji kutoka nchini Niger aliyekuwa akicheza nchini Russia katika klabu ya CSKA Moscow.

Kama uongozi wa Simba usingefanya maamuzi ya haraka ya kumuuza Okwi wakati ule, ilikuwepo hatari ya wazi ya kumkosa kwani mkataba wake ulikuwa unakaribia kwisha na angeweza kusubiri mkataba wake uishe na aende kucheza kwenye timu atakayotaka.

Hivi Saleh Ally anafahamu wapenzi na wanachama wa Simba wangeumia kiasi gani kama wangemuona mchezaji wao huyo akichezea Yanga au Azam kwenye Ligi Kuu ya Tanzania?

Mimi kama Mwenyekiti wa Simba, kazi yangu kubwa ni kulinda matarajio na matumaini ya wanachama wangu na tulichofanya kwa Okwi kilikuwa ni uamuzi sahihi kwa wakati ule.

Nimwambie Saleh Ally na watu wengine kwamba Simba itapata haki yake kwenye sakata hili kwa vile ilifuata taratibu na kanuni zote zinazotawala masuala ya usajili wa wachezaji kupitia FIFA.

Ningemshauri pia mdogo wangu Saleh kuachana na uwekaji wa vichwa vya habari vya kutisha. Anapozungumzia kuhusu suala la Okwi kuondoka na kichwa cha mtu alikuwa anamaanisha nini? Kuna lugha nyingi ambazo angeweza kuzitumia lakini akaamua kuweka ya kutisha.

Mpaka sasa uongozi wangu hauna sababu yoyote ya kujiuzulu.

Katika miaka hii mitatu ya uongozi wetu, tumetwaa ubingwa wa Tanzania, tumecheza hatua ya 16 bora ya Kombe la CAF, tumetwaa Kombe la Banc ABC, tumetwaa Kombe la Uhai kwa timu za vijana, tumefunua soko zuri la wachezaji kwa nchi za kimataifa na tumejipambanua kama timu ambayo inatoa fursa kwa wachezaji wake zinapojitokeza.

Tuko mbioni kuanza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Klabu unaotoa dira na mwelekeo wa namna gani klabu hii kongwe inapaswa kuendeshwa miaka mingi baada ya wote wanaosoma makala hii kuwa hawapo duniani.

Oh, na nilisahau, tumemfunga Yanga 5-0! Tujiuzulu kwa kosa lipi? Timu gani nyingine hapa Tanzania inaweza kujisifu kufikia mafanikio hayo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita?

Kwa bahati nzuri, miezi michache ijayo, Simba itafanya uchaguzi wake wa viongozi na wanachama watapata fursa ya kuchagua watu wanaowataka. Wakati huo ukifika, wanachama watazungumza.

Nimeamua kuandika makala hii si kwa lengo la kutaka kulumbana bali kuonyesha ukweli ulivyo. Mimi, pamoja na uenyekiti wangu, ni mwananchi wa Tanzania ambaye Katiba imenipa fursa ya kujieleza kama walivyopewa raia wengine wote.

Ni matumaini yangu kwamba gazeti la CHAMPIONI, ambalo nikiri kwamba huwa nalisoma mara kwa mara, litakuwa na ujasiri wa kuchapa makala hii kama ilivyo na kwa ukubwa wake; kama pia ilivyokuwa na ujasiri wa kuchapa ile iliyoandikwa na Saleh.
Nawatakia kila la heri.
Mwisho

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic